Ads (728x90)

Washtakiwa wa kesi ya kukutwa na nyara za serikali pembe za Faru, raia wa China wakiwa nje ya mahakama ya Hakimu Mkazi mfawidhi mkoa wa Mbeya kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, kutoka kushoto ni Song Lei, Xian Shaodan, Chen Jian Liang na Hu Lian


Wachina wa pembe za Faru wakisindikizwa mahakamani ya hakimu mkazi mkoa wa Mbeya kusomewa hukumu ya kesi inayowakabili ya kukuitwa na nyara za serikali pembe 11 za Faru
 


 

Gari iliyotumiwa na wachina kusafirisha pembe za Faru kutokea nchini Malawi


MAHAKAMA ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Mbeya imewahukumu kwenda jela miaka 20 watalii  wanne raia wa  nchini China ambao wamekutwa na nyara za serikali pembe za Faru 11 zenye thamani ya dola za kimarekani 418,000 zenye uzito wa kgm 53.3 kinyume cha sheria.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takribani saa 4 kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 9:45 alasiri Hakimu wa mahakama ya hakimu mfawidhi mkoa wa Mbeya Michael Mtaite alisema kuwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 20 inakwenda pamoja na kulipa faini zaidi ya dola 800.
Hakimu Mtaite amesema kuwa washitakiwa hao  Song Lei(32)Xiao Shaodan(29)Chen Jianlian(33)na Hu Liang kwa pamoja walikutwa na nyara hizo pembe za Faru Novemba 6 kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi, Kasumulu wilayani Kyela wakati wakijaribu kuvuka mpaka kuingia nazo nchini.
Amesema washitakiwa hao ambao walikuwa na gari aina ya Toyota Hilux Surf yenye namba za usajili T 103 DER ambapo katika gari hilo walitengeneza sanduku maalumu la chuma chenye kufuri na bawaba na kuhifadhi pembe hizo kwa nia ya kuziingiza nchini.
Hakimu Mtaite ambaye alikuwa akisoma hukumu hiyo kwa Kiswahili huku ikitafsiriwa kwa lugha ya Kichina na mkalimani Mtanzania Manifred Lyoto amesema kuwa raia hao wa China wanatiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Aidha amesema kuwa mahakama imezingatia kiini cha kosa na kujiridhisha kuwa washatikiwa walipanga kutekeleza kosa la jinai kwa kuingiza nchini nyara za serikali pembe 11 za Faru bila kibali,kutekeleza kuingiza pembe hizo nchini na kukutwa nazo wakizimiliki bila kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyama pori.
Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo wakili wa serikali Wankyo Simon ameitaka mahakama hiyo kutoan adhabu kali dhidi ya washtakiwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu na ujangiri dhidi ya wanyama pori walio hatarini kutoweka.
Wakili Simon amesema kuwa kitendo cha washtakiwa hao pia kinakiuka mkataba wa Kimataifa unaolinda na kuhifadhi wanyama walio mbioni kutoweka ikiwa ni pamoja na  sheria za Uhujumu uchumi na kuitaka mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa raia wengine wanaosingizia kuingia nchini kwa ajili ya utalii.
Amesema raia hao waliingia nchini kwa nia ya kufanya utalii na kuwa badala yake wamekuja kufanya uhalifu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa kuwa ni mfano kwa adhabu kali ambayo mahakama inapaswa kutoa dhidi ya washtakiwa.
Naye Wakili wa upande wa utetezi Ladslaus Rwekaza amesema kuwa mahakama iangalie uwezekano wa kuwapunguzia adhabu hasa ikiangaliwa mahusiano ya urafiki baina ya Tanzania na China na kuwa kutokana na kosa hilo kuwa ni la kwanza na kutokuwa na historia ya makosa ya aina hiyo kwa washtakiwa, mahakama itoe adhabu kwa jicho la huruma.

Hata hivyo Hakimu Mtaite ambaye aliahirisha hukumu hiyo kwa saa nzima amesema mahakama inawahukumu jumla ya miaka 38 jela kwa makosa matatu ambapo adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja na kutumikia jumla ya miaka 20 jela huku wakitakiwa kulipa faini ya dola zaidi ya 800,000.

Post a Comment