Ads (728x90)


Baadhi ya waumini wa Kiislamu wilaya ya Namtumbo wakishiriki kwa pamoja kulima shamba kwa ajili ya kupanda Ufuta na Mbaazi



Baadhi ya akina mama wa Kiislamu wakiandaa chakula cha mchana wakiwa shambani wanakoshiriki kwa pamoja kilimo cha Ufuta na Mbaazi.


(Kutoka kushoto)Katibu wa BAKWATA wilaya ya Namtumbo Ustadhi Yassin Kinonono,Imamu wa msikiti wa Najaat Shekhe Said Makunguru na Imamu wa msikiti wa Nurullah Shekhe Juma Nalunya, wakizungumza na mwandishi wa blogu hii wakiwa shambani ambako wanalima kwa pamoja shamba kwa ajili ya kupanda Ufuta Mbaazi ili kuondokana na utegemezi


WAUMINI wa dini ya Kiislamu wanaofuata Itikadi za Answar na wale wanaofuata itikadi za BAKWATA wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameungana na kuwa kitu kimoja kwa kulima shamba la Ufuta na Mbaazi ili kujikwamua kiuchumi.
Waislamu hao kutoka katika msikiti wa Najaat na msikiti wa Nurullahi yote iliyopo kata ya Rwinga wilayani humo wamejitokeza kwa wingi kulima shamba lenye ukubwa wa hekari 3 kwa nia ya kulima mazao ya Ufuta na Mbaazi.
Wakizungumza shambani hapo maimamu wa misikiti hiyo wamesema kuwa wanaunganishwa na imani ya dini yao na kuweka kando itikadi zao ambazo hata hivyo haziathiri Umoja wao wa Kiislamu unaolindwa na maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyomo kwenye kitabu cha Koran Tukufu na hadithi za Mtume Muhammad(SAW).
Imamu wa BAKWATA mtaa wa Rwinga Shekhe Juma Nalunya amesema kuwa wameungana na waislamu wenzao wa msikiti wa Najaat kwa ajili ya kulima shamba hilo kwa nia yaa kujikwamua kiuchumi na mahitaji mbalimbali wanayokumbana nayo kila siku.
Naye Imamu wa msikiti wa Najaat uliopo chini ya Taasisi ya Dhiynurain Sheikh Said Makunguru amesema kuwa awali waislamu wa maeneo hayo walipandikizwa chuki na kugawanywa makundi kutokana na itikadi na uelewa na kuwa kwa sasa hali hiyo imeanza kutoweka baada ya kuwepo kwa ushirikiano kwa kila jambo linalowahusu waislamu.
Amesema kuwa jambo kubwa linalowapaswa waislamu ni kushikamana katika njia ya Mwenyezi Mungu bila kufarakana kwa kuwa mfarakano unasababisha waislamu wazidi kudidimia kiuchumi na kifikra.
Kwa upande wake Katibu wa BAKWATA wilaya ya Namtumbo Yassin Kinonono amesema kuwa ushirikiano uliooneshwa na waumini hawa unapaswa kuambukizwa katika maenep mengine kwa kuwa kukosekana kwa umoja ndiko kunakosababisha mgongano na migogoro katika Uislamu.
Amesema kuwa Umoja huu wa waislamu wa kata hii utakuwa ni mfano kwa waislamu wa wilaya nzima ya Namtumbo na kuwa wao wameonesha njia nzuri ambayo BAKATWA inapaswa kuwaunga mkono na kutoa elimu ya mshikamano kwa waislamu wote ili wawe kitu kimoja.
Shamba hilo la hekari tatu lipo katika kijiji cha Migelegele  kata ya Rwinga wilaya ya Namtumbo ambalo waislamu wamedhamiria kulima mazao ya biashara ya Ufuta na Mbaazi.


Post a Comment