Ads (728x90)

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mazingira wakiwemo viongozi wa Baraza la Taifa la Mazingira NEMC wakuu wa wilaya na waandishi wa habari













JUMLA ya miradi 124 imekaguliwa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika mikoa mitatu ya Nyanda za Juu kusini ya Mbeya, Rukwa na Katavi kwa kipindi cha miezi miwili ya Julai na Agosti mwaka huu. 

Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Migodi 42,Viwanda 13,Vituo vya Mafuta 56, Hoteli 2, Mashamba 3 na miradi mingine ipatayo 8 ambayo ni mchanganyiko wa shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza wakati wa mkutano wa NEMC na wadau wa mazingira kwenye ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mazingira nchini Mhandisi Bonaventure Baya alisema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kufuatilia utunzaji wa mazingira katika miradi mbalimbali ya uzalishaji na maendeleo.
Alisema Baraza la Mazingira liliunda vikosi kazi ili kufuatilia  kwa kina utekelezaji wa shughuli za mazingira  kwa lengo la kubaini viwango vya uzingatiaji wa sheria ya mazingira pamoja na kanuni mbalimbali za uendeshaji wa miradi.
Mhandisi Baya alisema kuwa vikosi kazi hivyo vilifanya ukaguzi wa kina katika mikoa ya kanda ya Ziwa, baadhi ya  miradi katika mkoa wa Dar es salaam, kanda ya Mashariki na kaskazini na kuwa ukaguzi huo wa miradi ya mazingira umekusudiwa kuwa endelevu kwa kuhusisha kanda zote nchini.
Alisema kuwa miradi iliyokaguliwa imegawanyika katika makundi matatu ambayo itatekelezwa kwa kufuata matakwa ya sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa mazingira, miradi iliyokuwa ikijitahidi kufuata sheria na taratibu za mazingira na miradi isiyokuwa na mpango madhubuti wa hifadhi ya mazingira.
Alibainisha kuwa miradi isiyokuwa na mpango madhubuti wa hifadhi imesababisha kuvunja sheria, kanuni na taratibu za usimamizi na utunzaji wa mazingira na kuwa kati ya miradi 124 ni asilimia mbili tu ya miradi ndiyo iliyotekelezwa kwa kufuata sheria za mazingira.
Baya alisema kuwa asilimia 11 ya miradi ina vibali vya mazingira lakini haikuzingatia utekelezaji wa sheria na mpango wa kutunza mazingira(EMP) ambapo asilimia 87 ya miradi iliyopo inatekelezwa bila vyeti.
Awali akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali za kijamii kushiriki kwa pamoja katika uhifadhi wa mazingira ili kuweka mustakabali mzuri wa maisha ya binadamu na maendeleo yake.
‘’Jukumu la utunzaji wa mazingira ni letu sote tunapaswa kuwa wakereketwa wa mazingira kwa maslahi yetu na vizazi vijavyo,’’alisema Kandoro.
Alifafanua kuwa upo uwiano mkubwa katika ya afya za binadamu na uhifadhi wa mazingira na kuwa iwapo mazingira yataharibiwa afya za binadamu nazo zitakuwa hatarini.

Post a Comment