Wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) upande wa Tanzania
kituo cha Mbeya wameitisha mgomo baridi kwa kutofanya kazi wala kuendesha
mitambo hadi pale watakapolipwa mishahara yao ya miezi mitano wanayolidai Shirika
hilo.
Wafanyakazi
hao takribani 40 ambao wanadai
kuwawakilisha wenzao zaidi ya 1000 wanaofanyakazi katika Reli hiyo kati ya
Tunduma na Kurasini walitoa msimamo huo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya
mjini Joseph Mbilinyi huku wakimuomba kukifikisha kilio chao Wizara ya
Uchukuzi.
‘’Tunakuomba
Mheshimiwa Mbunge, tufikishie kilio chetu Wizarani,
tuko hoi tunakufa na njaa, tunadaiwa kodi za nyumba ,karo za
shule watoto wamefukuzwa, maisha yanazidi kuwa magumu siku hadi
siku,’’alisema Ramadhani Mohamed aliyejitaja kuwa ni Karani Mwandamizi
wa
Shirika hilo.
Naye Chrisant
Amani aliyejitaja kuwa ni Dereva wa Treni alisema kuwa mazingira magumu
waliyonayo yamewasababisha kushindwa kuendesha Treni na kuwa hawezi kuendesha
Treni katika mazingira aina hiyo hadi hapo atakapohakikishiwa amelipwa
mishahara yake anayolidai Shirika.
‘’Mimi ni
Dereva wa Treni, siwezi kuendesha treni nikiwa na mawazo na mazingira magumu
huku nikiwa nimebeba roho za watu,ninaweza kusinzia kwa njaa nikapoteza
mwelekeo, ni hatari kufanya kazi katika hali hii,’’alisema Amani.
Kwa upande
wake Hilda Mtaya ambaye anafanya kazi ya Kufungua Njia, ‘Point Man’ alisema
kuwa watoto wake wamefukuzwa shule na nyumba aliyopanga kafukuzwa anaishi kwa
rafiki yake hivyo anahitaji kulipwa mshahara wake ili atatue matatizo yake
vinginevyo ataendelea na mgomo hadi atakapothibitishiwa malipo yake.
Mtaya
alisema kuwa Shirika hilo ni la Tanzania na Zambia lakini wafanyakazi
na kuwa hali ya kipato kati ya wafanyakazi wa pande hizi hailingani kwa
kuwa wenzao wa Zambia wana maisha mazuri kuliko wao wa upande wa
Tanzania.
Akizungumza
juu ya sakata hilo Mbunge wa Mbeya mjini, Mbilinyi alisema kuwa amesikia kilio chao na
kuahidi kulifikisha suala hilo Wizarani na kuenda mbali zaidi kwa kubainisha
kuwa watendaji wa wizara hiyo akiwemo Waziri anayehusika hawana nia ya dhati
kutafutia ufumbuzi tatizo hilo.
''Huu
ni ubabaishaji, wafanyakazi wanafikisha hadi miezi mitano Wizara
haishituki, wamekaa maofisini hawajui matatizo ya wafanyakazi wao, hii
inasikitisha,''alisema.
Mbilinyi
alisisitiza kuwa matatizo mengi yaliyopo katika Reli ya TAZARA yanatokana na
watendaji kuwa na maslahi binafsi hali ambayo inaleta hisia kuwa wapo baadhi ya
viongozi(hakufafanua ni viongozi gani)
ni wamiliki wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo nje ya nchi hivyo
kufilisika kwa Shirika hilo kuna maslahi kwao.
Alisema
kuwa
amekuwa akipigia kelele suala la uboreshaji wa reli hiyo kwa muda mrefu
ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa Bandari ya Nchi Kavu iliyopo
Iyunga jijini Mbeya ambayo anaamini ingesaidia kupunguza kero na
kuboresha utendaji wa Shirika hilo lakini
hadi sasa hakuna kinachoendelea.
Gazeti
hili
liliwasiliana kwa njia ya simu na Meneja mkuu wa TAZARA upande wa
Tanzania Abdallah Shekimweri
ili kuzungumzia tatizo la wafanyakazi hao na kusema kuwa mtoa taarifa wa
Shirika hilo ni Ofisa Uhusiano aliyemtaja kwa jina la Regina Tarimo
ambaye
alipotafutwa alidai kuwa analifanyia kazi jambo hilo na atapiga simu kwa
mwandishi wa habari hizi baadaye
ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
|
Post a Comment