Assalaam
Alaykum!! Ni matarajio yangu nyote mko salama usalimini,nachukua fursa hii kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha siku ya leo,bila kuwasahau ndugu jamaa na
marafiki ambao kwa namna moja ama nyingine wamefanikisha uwepo wangu hadi leo.
Nitakuwa mja
nisiye na shukurani iwapo nitaacha
kuwaombea dua wazazi wangu waliotangulia mbele ya haki ambao kwa kila hali
uwepo wangu ulitokana na wao kuwepo duniani kwa kunizaa na kunilea kisha
kunisomesha kwa tabu na mashaka
wakijidunduliza vijisenti vyao kidogo walivyopata kwa ujasiriamali mdogo.
Walifanya
hivyo kwa nia moja tu ya kunipa mwanga wa kutambua mema na mabaya kwa
kunisaidia nipate elimu ya dini na dunia.
Nilipata
utambuzi wa kujua mema na mabaya kupitia elimu ya dini waliyonipatia kadhalika
nilipata ujuzi wa mambo ya kidunia na kujiendeshea maisha kwa kadri Mungu
alivyonijaalia, na sasa nami nimekuwa mtu mzima, nimekuwa baba, mwenye jumla ya
watoto 7, wake kwa waume, Alhamdulillah.
Jambo moja
adimu na adhimu kwangu ni masikitiko yangu makubwa yaliyonikumba,ambayo ni
matarajio ya wengi kutamani sana kuishi duniani bali inapofikia muda wa
kupungua umri wa kuishi huufurahia na
kusherehekea kwa nderemo na vifijo.
Ningekuwa na
furaha na faraja iwapo ningelikuwa nimejihakikishia mizani ya mema kuliko maovu
niliyoyatenda hapa duniani, nikijipima sijioni kama ni mtukufu wa kuufurahia
umri wa nusu karne nilionao, Mwenyezi Mungu aendelee kuninusuru.
Aghalabu tulio
wengi hufurahia tabia hii ya kimaumbile ya kuongezeka miaka na baadhi yetu
tumekuwa tukiandaa sherehe kubwa tukiadhimisha
na kufurahia tukio kubwa la kihistoria katika uhai wetu, bali kinyume na walio
wengi kwangu ni masikitiko makubwa.
Yapo mambo
ambayo yananifanya nisikitike, jambo moja ni kuwa kadri ninapoongeza miaka
ndivyo ambavyo umri wangu wa kuishi unapungua,natafakari muda wote wa miaka 50
niliyoishi jambo gani nimelifanya ambalo litaniweka katika mikono salama mbele
ya Mwenyezi Mungu.
Natafakari,
ndugu na jamaa nitakaowaacha duniani watarithi mwenendo gani kutoka kwangu,
nitakuwa kiigizo chema ama nitakuwa mfano mbaya usiopaswa kuigwa na wengine,
yote haya ni maswali yaliyojaa kichwani mwangu hata najikuta sijivunii kufikia
umri huu.
Natafakari maisha haya ambayo nimeruzukiwa
hapa duniani kama yatakuwa na manufaa kwa kizazi changu ama wale wanaonizunguka,ni
wangapi wamenikosea nikashindwa kuwasamehe, na wangapi niliwakosea wakashindwa
kunisamehe, wangapi wananidai sijawalipa madeni yao na wangapi ninao wadai
hawajanilipa?
Natafakari mengi zaidi ya haya kwamba mimi ni msafi kwa
kiwango gani hata nikaufurahia umri huu, je! chakula nilacho kina Baraka ama ni
laana kwa tumbo langu? Je! kinatokana na vyanzo halali vya mapato yangu ama
kuna mahala nilikula ama kuchukua cha mtu bila ridhaa yake?
Nainua
mikono juu namuomba Mwenyezi Mungu anijaalie niwe na maisha mepesi na kipato
ambacho kitatokana na riziki halali katika maisha niishiyo ambayo kiukweli ni
magumu na sijui hatima ya maisha haya, kama yanastahili kufurahia na
kuadhimishwa kama wengi wafanyavyo, natafakari nabaini ni majuto na majonzi tu kila
uchao!!
Wakati
mwingine hupata riziki ambayo aidha imetoka kwa wenye mikono inayochuma chumo
halali na mara nyingine hupata riziki kutoka kwa watu ambao nina mashaka nao,
hata hivyo wapo wengine kwa macho yangu ya yakini naona kabisa nimefanya kazi
zao halali lakini malipo yao sijui yanatokana na vyanzo vipi.
Bado
natafakari aina hii ya maisha,wapo
wanaonilaumu kwa utendaji wangu wa kazi pia wapo wanaonipongeza kwa kazi nzuri,
kioo changu ni jamii inayonizunguka, sijijui ila wananijua, wanayaona makosa
yangu?, nikosoeni ningali hai, ili nijijue nilipokosea niwaombe radhi, msisubiri
nikifa ndipo mnisimange na kuniteta kwa makosa ambayo ningeweza kujirekebisha
kwayo.
Leo March
12, 2015 nimetimiza miaka 50, ni nusu karne, sikutuma maombi kwa Mwenyezi Mungu
anifikishe umri huu ambao kiukweli sijivunii sana kwa kuwa sijui kiwango changu
cha mema kama kinaweza kuyafuta maovu niliyowahi kutenda ikiwa nimetenda kwa
bahati mbaya ama nimetenda kwa kukusudia.
Natimiza
umri huu ilhali wapo kundi la watu na ndugu wanaonihusu niliokuwa nikiwategemea wakiwa wametangulia
mbele ya haki, baadhi yao hawakufikisha umri huu walitangulia, wangependa
waishi na wafikie umri kama huu nilionao, Mwenyezi Mungu awarehemu, niliwapenda
lakini Mungu aliwapenda zaidi.
Nililia sana
hadi machozi yalikauka nilipowapoteza ndugu zangu kwa matukio mbalimbali ya
kutisha na wengine wakidhulumiwa haki yao ya kuishi kwa kuuawa na wengine kwa
ajali na wengine kwa maradhi mbalimbali, mimi sijui aina ya kifo changu kitakavyokuwa
ni Mungu pekee ajuaye hatima yangu.
Najiuliza
nitakufaje? Nimejiandaaje na kifo hicho, nitakufa usingizini ama nitakufa
barabarani, ama nitakufa kwa maradhi? Yote ni maswali ambayo katu siwezi kupata
majibu yake sasa.
Wapo
watakaoumizwa na kifo changu wakitafakari mengi, kwamba walipenda niwe nao siku
zote duniani ama walipenda ucheshi wangu na wengine walikuwa tu na mapenzi ya
kibinadamu, bali watalia kwa uchungu kwa kuondokewa na kipenzi chao.
Wapo pia
watakaofurahia kifo changu ijapo hawatajionesha hadharani kuwa wamefurahia, watajitokeza
wakijifanya wana uchungu,wakipaza sauti za kilio huku wakigaragara chini kumbe
moyoni wana lao jambo, haya ndiyo maisha ya binadamu na namna ambavyo tulivyo roho
zetu.
Natimiza
miaka 50 nikiwa na historia ndefu ya maisha na magumu mengi niliyopitia, ila
jambo moja nililojifunza sipaswi kumpenda sana rafiki yangu kwani kuna siku
anaweza kuwa adui kadhalika pia nimejifunza kuwa sipaswi kumchukia sana adui
yangu kwani iko siku anaweza kuwa rafiki yangu.
Nitaendelea
kuwapenda na kuwathamini enyi ndugu na marafiki zangu, sina lolote ninaloweza
kuwalipa kwa wema mliowahi kunitendea bali ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye
uwezo wa kuwakirimu kutokana na wema mlionifanyia, ninawaombea kwa Mungu
awajaalie mpate riziki halali na yenye manufaa
‘’Metimiza Hamsini, Mola amenijaalia,
Japo sioni
thamani, umuri kufurahia,
Namshukuru
manani,na wangu wazazi pia,
Mola
amenijaalia, sasa myaka hamsini.
Sasa myaka
hamsini, Mola amenijaalia,
Nimefikwa
mitihani,mingi ilonipitia,
Bado
ninajithamini,ngawa sijafurahia,
Mola
amenijalia, sasa myaka hamsini.
Mwisho
nimeufikia, shukurani naitoa,
Leo
nimetimizia, myaka hamsini si mia,
Umuri
umeshapea, Uzee nakimbilia
Mola
amenijalia, Sasa myaka hamsini.
Mashaallah! Mwenyezi Mungu akupe umri mrefu wenye manufaa
ReplyDeleteAamin Barakallahu
ReplyDelete