CUF tumefanya vibaya sana katika uchaguzi mdogo wa Igunga
Lazima nikiri kuwa washindani wetu wakubwa CCM na CHADEMA wametushinda katika uchaguzi mdogo wa Igunga.
Kwa matokeo ambayo nimeyashayapokea kutoka kwenye asilimia 88 ya vituo kwa ujumla tumefanya vibaya sana. Japokuwa tumekuwa na mgombea mzuri sana na tumemnadi kwa kutumia uwezo wetu wote ambao kwa hakika kila mtu ameuona, lakini matokeo hatuwezi kuyageuza.
Ninachojifunza zaidi ni kuwa wapiga kura wengi ndani ya Tanzania bado wanaamini zaidi propaganda kuliko hali halisi ya mazingira yanayowakabili na hii ikizidi kushabikiwa ndivyo ambavyo wananchi watakosa fursa bora siku za mbele.
Ikiwa hali hii itaendelea hivi ina maana bado nchi ina safari ndefu ya kufikia demokrasia ya kweli na maendeleo yatakayoonekana kwa macho.
Katika uchaguzi huu wa Igunga CUF tumepambana na changamoto kubwa ya kujibu propaganda zilezile kuwa eti "Sisi ni CCM B", kila tulikoenda tumekutana na kikwazo hiki, tumejaribu kwa dhati kuwaelimisha wananchi bila mafanikio na muda umekuwa ukikimbia kuliko upepo.
Hata hivyo bado naamini kuwa tutapata fursa kubwa ya kuwaelimisha wananchi siku za usoni. Mimi na wenzangu hatutakata tamaa kwani MAFANIKIO KATIKA NYANJA YA SIASA huhitaji mioyo migumu.
Natambua kuwa uongozi ni dhamana nzito inayohitaji kujipanga zaidi na zaidi, Na CUF itazidi kujipanga zaidi na zaidi na kila tutakapoanguka tutanyanyuka na kuanza safari, hakika TUTAFIKA.
Chama changu kinakabiliwa na changamoto kubwa sana mbele ya safari na kwa hakika inahitaji tuzidi kujipanga na kujiimarisha. Kama chama hatutajilaumu kamwe, tumeonesha uwezo mkubwa na kufanya kampeni sahihi tukiwa na mgombea wa kiwango kizuri kwa mpiga kura yeyote anayehitaji kiongozi. Lakini kusimamisha mgombea mzuri na kufanya kampeni nzuri wakati mwingine siyo sababu ya kufanya vizuri. Maamuzi ya nani awe mbunge, ni mzuri au mbaya, anafaa au hafai yako kwa wananchi.
Wananchi wa Igunga tunawashukuru kwa namna walivyotuunga mkono na tunawaomba wawe kitu kimoja katika kuiendeleza Igunga yao kwani mshindi akishatangazwa yeye ni mbunge wa wananchi wote. Vyama vyetu hivi vipo ili kuisaidia jamii kupata kiongozi mzuri tu, nasi kama chama tumetimiza wajibu wetu.
Mimi kama kiongozi wa ngazi ya juu wa CUF - Tanzania Bara(Bila kujali nimekuwa kiongozi wa ngazi ya juu miezi minne tu iliyopita tu) nabeba dhamana kwa matokeo yote tuliyopita, najitwika mzigo wa kusimama imara kuiimarisha CUF. Sitatoka CUF na kukimbilia kwenye vyama vyenye nguvu Tanzania bara kama CHADEMA n.k. eti kwa sababu tu CUF imefanya vibaya kwenye uchaguzi. Ninaamini katika CUF na nitaisaidia Tanzania yangu nikiwa CUF, ninaamini siku moja wakati CUF imeimarika nitatajwa kati ya watu ambao hawakukata tamaa na hawakuyumbishwa na magumu yaliyowakabili na walisimama kidete kwenda mbele.
Tunawashukuru wale wote waliotuunga mkono katika uchaguzi huu na wale wanaotuunga mkono siku zote na wale watakaotuunga mkono siku zijazo. Kwa hakika wote tunawashukuru sana na CUF itasimama imara.
Mungu awabariki sana.
"HAKI SAWA KWA WOTE"
Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi - CUF,
Tanzania Bara,
02 Oktoba 2011,
Igunga - Tabora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment