SAKATA la
kuzomewa kwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Bw.Shamsi Vuai Nahodha limetolewa
ufafanuzi na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa limetokana na
kero mbalimbali za kiusalama ambazo zinaigusa jamii ya wakazi wa Tunduma ambazo
zimeshindwa kutatuliwa.
Akizungumzia
tukio hilo Mwenyekiti wa CHADEMA wa mji mdogo wa Tunduma Bw.Herode Jivava
alisema kuwa,CCM inapaswa kujilaumu kumtuma kiongozi mtendaji mwenye dhamana ya
usalama wa raia kwenye mambo ya kisiasa ilhali yapo mambo ya msingi ambayo
Waziri alipaswa kuyapata kutoka kwa wananchi wa mji huo wa mpakani.
‘’Wapo
viongozi wa chama ambao wangeweza kutembelea wanaCCM wenzao…huyu ni Waziri
ambaye tunaamini kuwa anasimamia katiba ya Jamhuri ya Muungano katika wajibu
wake bila kupendelea chama cha siasa… ni haki yake kuzomewa kwa kuwa amekuja na
wanasiasa huku akitumia rasilimali za serikali’’,alisema Bw.Jivava.
Alifafanua
kuwa CCM ni chama kinachojitosheleza katika uongozi angeweza kuja Katibu Mkuu
au Katibu Itikadi na Uenezi ambao wangeweza kukutana na wanachama wenzao na kujadili
mipango yao ya chama, kitendo cha kumtuma Waziri wa mambo ya ndani kufanya
mikutano ya kisiasa badala ya kusikiliza kero za wananchi ndiyo sababu ya
kuzomewa kwake.
Alisema kuwa
CHADEMA imejenga imani kuwa kuanzia sasa askari polisi wote wataanza kutumika
kunyanyasa vyama vya upinzani kutokana na kiongozi wao kukubali kutumika
kisiasa kwa maslahi ya chama kimoja.
‘’Tunayo
matatizo mengi hapa mpakani, pamekuwa ndiyo njia kuu ya kusafirisha bidhaa
haramu kama dawa za kulevya,biashara ya
kuuza binadamu,wakimbizi ambao wanatumia njia hii kuvuka nje ya nchi na mengi
ambayo tungemweleza, anaacha mambo haya ya msingi anakuja kwa ajili ya chama
akisindikizwa na magari ya serikali?… ni halali yake kabisa
kuzomewa,’’alisisitiza Bw. Jivava.
Bw.Jivava
alisema kuwa alichokifanya Waziri Nahodha kimedhihirisha namna ambavyo viongozi
wakuu wanavyoamua kuikanyaga demokrasia kwa kukipendelea chama tawala na kuwa
amejipandia mwenyewe mbegu ya chuki miongoni mwa wananchi wa Tunduma jambo
ambalo hapaswi kuwalaumu waliozomea bali waliomtuma kufanya ziara ya kisiasa
badala ya ziara ya utendaji.
Katika hatua
nyingine Bw.Jivava alikanusha taarifa iliyotolewa na CCM kuwa kuna wanachama 96
waliojiunga na CCM kutokea CHADEMA na kusema kuwa wanachojua ni mwanachama mmoja
tu ambaye alitimuliwa CHADEMA kwa kukiuka taratibu za kiuongozi ndio aliyerejea
CCM ambaye ni aliyewahi kukaimu nafasi ya Katibu Kata wakati wa uchaguzi mkuu
Bw. Julius Ndindilile.
Alisema
tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu CHADEMA imepokea jumla ya wanachama wapya
132 ambapo wawili kati yao wametokea
chama cha TLP na 130 wametokea CCM.
Waziri
Nahodha juzi alikumbana na zahama ya kuzomewa alipofika katika eneo maarufu la
wafanyabiashara vijana wanaobadilisha fedha ambapo kundi la vijana waliosimama
barabarani huku wakiwa na bendera za CHADEMA walisikika wakiuzomea msafara huo
huku wakipeperusha bendera za chama chao.
Post a Comment