Ads (728x90)



TMF yatoa 780m/- kwa mashirika ya habari
JUMLA ya mashirika ya habari 12 yatanufaika na ruzuku ya shilingi 780m/- kutoka katika Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa ajili ya kuyajengea uwezo, uelewa na uhamasishaji.
Mashirika yaliyonufaika ni pamoja na vyombo vya habari 10 na makampuni mawili ya kutengeneza habari. Haya ni pamoja na Afya Radio kutoka Mwanza, Iringa Municipal Television, Moshi Radio FM, Kilimanjaro Film Institute na Radio Habari Njema kutoka mkoa wa Manyara.
Mengine ni Free Media Limited, New Habari Corporation (2006) Ltd, Dhamira Communicating Artist Company Limited, Radio Upendo FM, Uhuru Publishers Limited na Zenj Radio FM.
Hii inafanya idadi ya mashirika yaliyopata ruzuku kutoka TMF kufikia 58 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huu mwaka 2008 wenye lengo la kukuza ubora wa uandishi wa habari nchini Tanzania.
Akiongea katika hafla fupi ya kuingia mikataba na mashirika hayo katika ofisi za TMF jijini Dar es Salaam hivi karibuni,
Mkuu wa TMF, Ernest Sungura alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mikataba na utekelezaji mzuri wa miradi yao.
“Sasa ni wakati wa kutekeleza maombi ya miradi yenu kwa vitendo kwa kuzingatia mipango kazi yenu na kuheshimu mikataba mliyoingia leo na TMF” alisema Sungura.
Mhariri wa gazeti la ‘The African’ (New Habari Corporation), Shermarx Ngahemera alisema ruzuku hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika “kunoa ujuzi wa waandishi wake, hususan katika uandishi wa habari za uchunguzi. Tunabahati pia kwamba tutapata kompyuta ndogo nane ambazo zitarahisisha kazi yetu.”
Bi Agathe Lema, Mkurugenzi wa Radio Upendo FM, alisema ruzuku hiyo ni msaada mkubwa katika kuwajengea uwezo watangazaji wake katika uandaaji bora wa vipindi.
“Radio yetu ilianzishwa miaka saba iliyopita na muda wote tunajitahidi kukuza ubora wa vipindi vyetu kwa kuwajengea uwezo watangazaji wetu. Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania umetusaidia sana katika jitihada hizo ambazo zinalenga pia kuongeza idadi ya wasikilizaji wa Radio yetu,” alisema Bi Lema.
Mbali na kutoa ruzuku kwa mashirika ya habari na waandishi binafsi, TMF pia inatoa mafunzo kwa kutumia waandishi wakongwe kuwanoa waandishi binafsi na mashirika ya habari.
TMF kwa sasa inakamilisha mipango ya kuzindua awamu ya pili ya utendaji kazi wake hapo  Aprili, mwaka huu. Awamu hiyo itadumu kwa miaka mitano.(TAARIFA HII KWA HISANI YA TANZANIA MEDIA FUND)

Post a Comment