Ads (728x90)





HALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi imepanga kumburuza mahakamani mwandishi na gazeti moja linalochapishwa kila wiki kutokana na kile kilichoelezwa kuandika habari za uzushi ambazo hazijawahi kujadiliwa na kikao chochote cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya kuandikwa kwa habari zenye kichwa cha habari Ufisadi Waibuliwa Halmashauri ya Mbozi ambapo katika habari hizo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ametajwa kuiba jumla ya sh milioni 32 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya miradi ya mabwawa kata ya Isansa na Halungu.

Akizungumza katika kikao na waandishi wa habari, hivi karibuni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Elick Ambakisye alisema kuwa taarifa hizo ni za uzushi kwa kuwa hakuna kikao chochote cha Baraza kilichojadili tuhuma za wizi wala kuundwa tume kama lilivyoandika gazeti hilo.

‘’Hatujawahi kukaa kujadili tuhuma za aina hiyo katika kikao cha baraza la Madiwani, wala hatukumualika mwandishi huyo wala gazeti hilo kuhudhuria kikao hicho, taarifa hizi ni za kupikwa, tunatafakari kulichukulia hatua gazeti pamoja na mwandishi’’alisema Bw. Ambakisye.

Alisema kuwa pamoja na kuandAika habari hizo mwandishi hakutoa nafasi kwa Mkurugenzi ambaye amemtaja katika aya ya kwanza kuhusika na wizi huo jambo ambalo wanahisi alidhamiria kuichafua halmashauri na hivyo kupunguza ari ya wananchi kushiriki katika maendeleo.

Aidha Bw. Ambakisye alisema kuwa miradi ya mabwawa iliyotajwa katika kata za Isansa na Halungu thamani  yake ni zaidi ya fedha zilizotajwa na mwandishi huyo kwa kuwa miradi hiyo yote kwa pamoja ina thamani ya sh milioni  61.6 ambapo mradi wa Halungu una thamani ya sh milioni 35.6 na Isansa milioni 25.

Alisema kuwa ipo miradi mingine mitano ambayo kati yake hakuna mradi wenye thamani ya zaidi ya milioni 28 na kuwa kilichoandikwa katika gazeti hilo kililenga kuchafua utendaji wa halmashauri ya Mbozi.

‘’Huyu mwandishi alipiga simu na kujieleza kuwa yeye amekuja hapa amelala na kula anapaswa kulipwa kwa kuwa ana bomu la kuilipua halmashauri,tulitafakari kwa kina tukaona ni aina ya baadhi ya waandishi kuhitaji fedha kwa njia za rushwa..tulimpuuzia, kilichotokea tunaamini ndiyo dhamira aliyokusudia tunao ushahidi wa sms alizotutumia,’’alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Bw.Levison Chillewa alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya halmashauri hiyo inapitia mchakato wa kamati za baraza la madiwani na kwamba hakuna kinachofichwa katika utekelezaji wake.

Post a Comment