TATIZO la
ununuzi wa kahawa mbivu Red Cherry limeendelea kushika kasi wilayani Mbozi huku
baadhi ya wakulima wakilalamika kuibiwa kahawa yao ikiwa shambani na watu
wasiofahamika.
Taarifa
kutoka kwa baadhi ya wakulima katika vijiji vya Hatelele, Isansa, Itaka,Igamba,
Bara na Mtunduru zinadai kuwa kutokana na wakulima kutokubali kuwauzia wachuuzi
kahawa mbivu hivi sasa kuna kundi la watu wanaovamia mashamba nyakati za usiku
na kuvuna kahawa hiyo.
Imedaiwa
kuwa kahawa hiyo huvuna na kuiuzia kampuni mmoja iliyopewa leseni ya kununua
kahawa mbivu huku serikali ya wilaya na Mkoa vikipinga kuwepo kwa ununuzi wa
kahawa hiyo kwa kuwa unamnyonya mkulima.
‘’Ununuzi wa
kahawa mbivu unasababisha mkulima apate hasara, mkulima anayeuza kahawa kavu
hupata faida kubwa kuliko yule anayeuza kahawa mbivu, huyu anamnufaisha
mnunuzi, tunapinga vikali ununuzi wa kahawa mbivu,’’anasema Bw. Adam Kalonge
mkulima wa Kahawa katika kijiji cha Hatelele.
Sakata hili
la ununuzi wa kahawa mbivu limekuwa ni mwiba mchungu kwa viongozi wa serikali
ya wilaya ya Mbeya na mkoa huku taarifa hizo zikijikanganya baada ya baadhi ya viongozi
wa wizara kudaiwa kukubali ununuzi wa kahawa mbivu kutokana na maslahi binafsi.
Katika kikao
cha Bunge kinachoendelea, Mbunge wa jimbo la Mbozi Mashariki Bw. Godfery Zambi
alimnyooshea kidole aliyekuwa Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Profesa Jumanne
Maghembe kwamba anahusika moja kwa moja katika kuidhinisha ununuzi wa kahawa
mbivu kwa baadhi ya makampuni ilhali anajua wazi kuwa kitendo hicho ni
kumdhulumu Mkulima.
Profesa
Maghembe aliwahi kukutana na wadau wa kahawa mkoani Mbeya katika kikao
kilichoketi wilayani Mbozi ambapo wakulima walitoa msimamo wao wa kupinga
kutolewa kwa leseni ya ununuzi wa kahawa mbivu ambapo katika kikao hicho,
Profesa Maghembe alishutumiwa na wakulima na viongozi wa chama cha Mapinduzi
kuhusika moja kwa moja na tatizo hilo.
Post a Comment