Ads (728x90)



Lori lililosababisha ajali na kuua mwanafunzi na kusababisha wanafunzi wa shule za msingi Tunduma kulala barabarani wakishinikiza kuwekwa kwa matuta.

Hali ilivyokuwa katika mji wa Tunduma leo asubuhi

Askari wa usalama Barabarani mjini Tunduma akipewa maelezo ya hali ya mtoto aliyejeruhiwa katika ajali hiyo Jackson Sichalwe(7) kutoka kwa baba yake Mzazi Norbert Siichalwe,Mtoto Jackson  amelazwa katika hospitali ya serikali mjini Tunduma baada ya kugongwa na gari ambalo pia lilisababisha kifo cha Emmanuel Sichalwe mwanafunzi wa shule ya msingi Umoja ya mjini Tunduma.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za Msingi Umoja,Mlimani na Tunduma za mjini Tunduma wakiandamana kushinikiza kuwekwa matuta kwenye inayoelekea Sumbawanga kutokana na ajali za mara kwa mara zinazosababishwa na mwendo kasi wa madereva.
Wanafunzi wakiwa wamekaa barabarani mjini Tunduma

Mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Tunduma wakiwa katika mkusanyiko kufuatia taharukii iliyoibuka mjini Tunduma leo asubuhi
Diwani wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka akizungumza na wanaanchi baada ya kutokea tafrani iliyosababisha wanafunzi wafunge barabara kwa kushinikiza kuwekwa matuta.

 Na Bloga Wetu Tunduma

 SAUTI zilizochanganyika na hisia na majonzi kutoka kwa wanafunzi wa shule tatu za Msingi, Umoja,Mlimani na Tunduma zilisikika hewani na kutoa ujumbe ulioashiria kupata ufumbuzi wa tatizo la ajali za mara kwa mara katika barabara kuu iendayo Sumbawanga kutokea mjini Tunduma.
Ijapokuwa zilikuwa ni sauti za watoto bali zilibeba ujumbe mzito wenye shinikizo la uchungu uliofuatia kufariki kwa mtoto mwenzao Emmanuel Sichalwe(7) ambaye aligongwa na Lori na kufariki hapo hapo baada ya kukanyagwa na kupasuka kichwa.
Haikuwa rahisi kuhisi machungu ya watoto hao ambao ni kilio cha muda mrefu kutoka kwa wazazi na wananchi waishio maeneo ya barabara kuu ya kuelekea Sumbawanga ambapo takribani watu 18 wakiwemo watoto 10 na watu wazima 8 hali ambayo imekuwa ikijenga hofu miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Wanafunzi hao walifunga barabara na kulala barabarani kuanzia saa 12:30 alfajiri huku wakihanikiza sauti zao hewani kwa maneno yaliyosikika,’’ Tunataka!!, Matuta Magari!! Yanatumaliza!!!’’ sauti hizo zilikarIriwa mara kwa mara huku baadhi yao wakionesha mabango.
Baadhi ya mabango yalisomeka wakimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro afike hapo kutoa kauli juu ya tatizo la wanafunzi na baadhi ya watu kugongwa mara kwa mara katika barabara hiyo ya Tunduma-Sumbawanga.
Aidha wanafunzi hao walionekana wakiranda katika barabara hiyo huku wengine wakiweka madaftari yao barabarani na kuandika kama vile wako madarasani na baadaye kuelekea hadi kwenye gari ambalo lilimgonga mwenzao na kusimama hapo wakiimba kwa sauti za kushinikiza kuwekwa kwa matuta barabara hiyo.
Maandamano ya wanafunzi hao ambayo yalikuja kukatishwa kwa muda na askari polisi waliokuwemo kwenye magari mawili aina ya Defender ambao waliwataka wanafunzi hao warejee madarasani na wanafunzi hao kushikinikiza kuhitaji uongozi wa juu wa serikali ufike eneo la tukio ili kilio chao kisikilizwe.
Baadaye kundi hilo la wanafunzi wanaokaribia 4,000 walielekea moja kwa moja hadi kwenye kituo cha Polisi Tunduma na kukizunguka kituo hicho huku wakiimba nyimbo za kushinikiza kuwekwa matuta barabarani na baadaye kukaa barabarani na kufunga barabara.
Hali hiyo ilisababisha magari yatokayo Mbeya kuelekea Sumbawanga na yale ya Sumbawanga kuelekea Mbeya kusimama kwa zaidi ya saa tano hadi pale alipofika mkuu wa wilaya ya Momba Abihudi Saideya na baadhi ya viongozi wengine wa serikali akiwemo Diwani wa kata ya Tunduma Frank Mwakajoka.
Akizungumza katika mkutano huo ambao uliokatishwa kwa kelele za hapa na pale kutoka kwa wanafunzi hao Saideya alisema kuwa kilio chao kitapatiwa ufumbuzi ambapo amewasiliana na viongozi wa Mawakala wa barabara TANROAD ili yawekwe matuta katika barabara hiyo.
Kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda wa tukio hilo ni kwamba ajali hiyo ilitokea Februari 16 majira ya saa 10:00 alasiri ambapo Lori Lenye Trela aina ya Scania lenye namba za usajili T 120 BRA na Trela lenye namba T 705 CGG lilimgonga mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya Msingi Umoja Emmanuel Sichwale(7) aliyefariki papo hapo.
Aidha kwa mujibu wa mashuhuda wengine waliogongwa na gari hilo ni pamoja na  Betiel Mwafu(32) ambaye alikanyagwa miguu na kufariki baadaye alipokuwa akipatiwa matibabu na mtoto mwanafunzi wa shule ya Msingi Umoja anayesoma darasa la kwanza Jackson Sichalwe(7)anayepatiwa matibabu katika hospitali ya serikali ya mjini Tunduma.
Inaelezwa kuwa mara baada ya gari hilo kugonga mwanafunzi huyo dereva wa gari hilo ambaye hakufahamika alishuka katika gari hilo na kukimbia na kulitekeleza gari hilo ambapo mmoja wa watu wasiofahamika akaingia katika gari hilo na kupangua Breki ya  Mkono(Hand Break) ambapo gari hilo lilianza kuporomoka na kugonga watu wengine wawili.
‘’Gari lilianza kutembea bila mpangilio likashuka kwa kasi na kuwagonga wengine wawili na baadaye kuanguka upande wa kushoto,’’alisema Ndegeulaya Simwanza mkazi wa mjini Tunduma.
Hata hivyo taharuki hiyo ilimalizika majira ya saa 5:00 asubuhi baada ya Diwani wa Kata hiyo Mwakajoka kusisitiza kuwa kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya hiyo barabara hiyo itaanza kuwekwa matuta kuanzia jana ili kumaliza tatizo la ajali eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mwakajoka katika eneo hilo jumla ya watu 18 wamegongwa gari wakiwemo wanafunzi 10 kwa kipindi cha mwaka mmoja na kuwa tatizo hilo limekuwa halitafutiwi ufumbuzi hali ambayo imekuwa ikiacha majonzi kwa wananchi wa mji huo.

Post a Comment