Ads (728x90)Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu(katikati) akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya ziara ya Mwenyekiti wa Taifa CHADEMA Freeman Mbowe katika mikoa ya Mbeya na Njombe,wengine katika picha ni Ofisa Habari wa CHADEMA Tumaini Makene(kushoto) na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya Joseph China Mwachemba
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda na Kiongozi wa Kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe watafanya ziara mkoani Mbeya kila mmoja kwa dhamira yake na malengo yake kwa ajili ya kuimarisha chama chake.
Wakati Waziri Mkuu anatarajia kuanza ziara yake kuanzia Februari 23 itakayodumu kwa wiki moja, Mbowe ameanza ziara yake jana ambayo itadumu kwa siku nne na kumalizia mkoani Njombe.
Akizungumzia ziara ya Mbowe Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar Salum Mwalimu alisema kuwa ziara ya Mbowe imelenga kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura Oktoba mwaka huu.
Aidha Mwalimu alisema kuwa Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA) umeendeleea kuelezea azma yake ya kususia zoezi la upigaji kura wa ajili ya kupitisha Katiba iliyopendezwa kwa madai kuwa Katiba hiyo haina tija kwa Watanzania na itadumu kwa muda wa miezi minne tu.
Mwalimu alisema kuwa mustakabali wa KATIBA na uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu unategemea kupigiwa kura na wananchi na kuwa wao wataendelea kususia na kuwahamisisha wananchi kutopigia kura katiba hiyo kwa kuwa haina tija kwa wananchi.
 ‘’KATIBA inayotaka kupigiwa kura ni ya serikali ya CCM sisi tumeikataa na tutaendelea kuikataa, itadumu kwa miezi minne tu kwa kuwa Novemba Mosi Rais wa UKAWA ataingia Ikulu na kuapishwa,’’alisema Mwalimu.
Mwalimu ambaye pia alitoa ratiba ya ziara ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe alisema dhamira ya UKAWA na upinzani kwa ujumla ni kuona wananchi wananufaika na KATIBA yao hivyo si vyema kuburuzwa kutokana na mahitaji na umuhimu wa katiba hiyo kwa miongo mingi ijayo.
Alisema kuwa Mbowe atafanya ziara ya siku nne katika mikoa ya Mbeya na Njombe kwa ajili ya uzinduzi na uhamasishaji wa uandikishaji wapiga kura na kuwa lengo ni kuona wananchi wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kutumia haki zao za msingi za upigaji kura ifikapo Oktoba mwaka huu.
Akielezea kuchelewa kutangaza mgombea wa UKAWA kama kuna uhusiano wowote wa kusubiri mgombea atakayeachwa na CCM kwenye kura za maoni, Mwalimu alisema kuwa katika wagombea wanaotajwa kuwania urais ndani ya CCM hakuna hata mmoja mwenye sifa ya kushindana na Mgombea wa UKAWA.
Alisema taratibu za UKAWA zinaendelea huku mchakato wa kila chama ukiendelea bila kuathiri mipango waliojiwekea na kuwa wananchi watarajie kumpata mgombea bora kutoka UKAWA ambaye atazima kilio cha muda mrefu cha kumpata rais bora wa Tanzania.
Wakati huo huo taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa vyombo vya habari imeleeza kuwa Waziri Mkuu Pinda anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika Halmashauri 7 za mkoa huo kwa ajili ya kutembelea miradi na mikutano ya hadhara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri Pinda atatembelea  Halmashauri ya Jiji la Mbeya,Halmashauri ya wilaya ya Mbeya,Kyela, Busokelo, Rungwe, Chunya na Mbozi ambapo atakagua miradi na kuweka mawe ya msingi ikiwa ni pamoja na kuzindua miradi katika elimu, afya, ujenzi, barabara na kilimo.

Post a Comment