Ads (728x90)


Na Ismail Jussa
Tarehe 5 Novemba, 2009 daima itakumbukwa kuwa ni siku ambayo nchi yetu iliandika historia mpya pale viongozi wawili wazalendo na mashujaa, Dr. Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, walipowaongoza Wazanzibari kufikia MARIDHIANO.
Haikuwa kazi rahisi lakini kwa kuongozwa na hisia za uzalendo na mapenzi kwa nchi yao na wananchi wenzao, Dr. Karume na Maalim Seif waliamua kujitolea kuongoza enzi mpya za siasa. Walijua kwamba katika vyama vyao viwili, CUF na CCM, wapo watu ambao wasingewaunga mkono na pengine wangeyatumia MARIDHIANO yale kutaka kuwahujumu kisiasa viongozi hao. Na kweli walikuwapo watu wa aina hiyo na wapo hadi leo.
Kwa kutambua kuwa watu waovu wasiopendelea umoja na masikilizano miongoni mwa Wazanzibari watakuja kusema kuwa MARIDHIANO hayo yalikuwa ni maamuzi ya watu wawili tu na hayawakilishi matakwa ya watu, Dr. Karume alipendekeza kwa Maalim Seif kukubali rai ya kufanya kura ya maoni ili kupata ridhaa ya Wazanzibari kuhusiana na mwelekeo huo mpya wa siasa na hasa kuhusu haja ya kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tarehe 31 Julai, 2010 ikafanyika kura ya maoni ya kwanza katika historia ya Zanzibar. Asilimia 66.4 ya Wazanzibari wakapiga kura ya NDIYO kuchagua MARIDHIANO na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baada ya maamuzi hayo ya Wazanzibari ndipo Baraza la Wawakilishi likafanya Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar na kuingiza muundo huo ndani ya Katiba.
Maamuzi hayo ya Wazanzibari yalikuwa na maana kubwa sana kwa nchi yetu na watu wake. Kwa kupiga kura ya NDIYO, Wazanzibari tulichagua maridhiano na kukataa mfarakano, tulichagua umoja na kukataa mgawanyiko, tulichagua upendo na kukataa chuki, tulichagua matumaini na kukataa khofu, tulichagua amani na kukataa fujo.
Inasikitisha kwamba miaka sita baadaye wale waovu miongoni mwetu ambao hawakutaka MARIDHIANO (wakiwemo wale ambao kwa dhahiri walijionesha kuyaunga mkono kwa sababu tu walitaka kulinda ulwa wao kwa kumridhisha Rais aliyekuwa madarakani lakini kwa siri wakiyapinga) wameturudisha kule kule kwenye mfarakano, mgawanyiko, chuki, khofu na fujo.
Lakini pamoja na juhudi hizo ovu za kuturudisha tulikotoka, ukweli mmoja unabaki kwamba Wazanzibari wengi hawako tayari kurudishwa huko. Wazanzibari wameona faida ya siasa za MARIDHIANO, UMOJA, UPENDO, MATUMAINI NA AMANI.
Binafsi, bado naamini kwamba MARIDHIANO, UMOJA, UPENDO, MATUMAINI NA AMANI vitashinda. Wazanzibari ni watu wema. Kutokana na wema wao, watachagua WEMA dhidi ya UOVU.
Kwa sababu hizo basi, NATOA NASAHA ZANGU KWA WAZANZIBARI WENZANGU kwamba tukatae njama zote za kuturudisha tulikotoka. Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na watu WAOVU ambao wamekuwa wakiandika maneno ya ovyo na matusi katika mitandao ya kijamii. Wengine ni watu wazima ambao ungetegemea kwa umri wao wangeonesha mfano mwema kwa kizazi cha leo. Bahati mbaya, baadhi ya vijana wameingia kwenye mtego wa WAOVU hao na kujibizana nao kwa matusi na lugha zinazoturudisha kwenye mfarakano, mgawanyiko, chuki na ubaguzi, mambo ambayo tukiyakataa kupitia kura ya maoni ya tarehe 31 Julai, 2010.
Nawapa NASAHA ndugu zangu tukatae kuingia katika mtego huo. Tuoneshe kama SISI NI TOFAUTI NA WAO. Tusijibu lugha zao za matusi, chuki na ubaguzi na sisi tukaandika lugha za matusi, chuki na ubaguzi. Haitoonekana tofauti kati yetu. Tuithamini na kuilinda kazi kubwa iliyofanywa na Dr. Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.
TUNAYOPITIA SASA NI MAJARIBU TU. TUSIKUBALI KUSHINDWA TUKARUDISHWA TULIKOTOKA. TUWAONESHE WAOVU KWAMBA SISI NI WEMA. NA WEMA SIKU ZOTE HUUSHINDA UOVU.

Post a Comment