KUUNGUA KWA
MABWENI YA SEKONDARI YA IYUNGA
- Mamilioni
yadaiwa kutafunwa kwa harambee hewa
-RC kutumbua majipu April 5
-Mkurugenzi
akataa kuelezea undani wa sakata hilo
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makalla |
Mkuu wa wilaya ya Mbeya Nyerembe Munassa |
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dkt Samwel Lazaro |
Hotel ya Ubungo Plaza jijini Dar |
Ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya |
Na Rashid
Mkwinda,Mbeya
KUUNGUA kwa
Mabweni ya Shule ya Sekondari Iyunga Jijini Mbeya kumeibua kashfa kwa viongozi
wa serikali jijini humo wakiwemo Mkuu wa wilaya ya Mbeya Nyerembe Munassa na
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dkt. Samwel Lazaro wanaodaiwa kuratibu
harambee Jijini Dar es salaam na kutapanya zaidi ya milioni 50 kwa maandalizi.
Hata hivyo
harambee hiyo iliyopangwa kufanyika Ubungo Plaza March 19 iliahirishwa ghafla
huku ikidaiwa kuwa na maandalizi yanayodaiwa kugharimu zaidi ya sh. mil 50
fedha ambazo zingeweza kusaidia ukarabati mkubwa wa majengo ya shule hiyo
ambayo ina umri wa miaka 90 tangu ianzishwe.
Kiasi hicho
cha fedha ambazo ni sehemu ya maandalizi zimedaiwa kutokana na kukodi ukumbi wa
kufanyia harambee hiyo Ubungo Plaza,gharama za kuwasafirisha watendaji wa
halmashauri na waandishi wa habari na malazi yao jijini Dar es salaam kwa siku
tano pamoja na maandalizi ya Chakula ukumbini.
Gharama za
ukumbi na chakula Ubungo Plaza zinakadiriwa
kila mtu mmoja anayehudumiwa hotelini hapo ni kiasi cha Sh 77,000 malipo ambayo
hufanyika kabla ya kupewa huduma na kuwa kulingana na idadi ya watu 300 walioalikwa
kwa ajili ya kushiriki harambee hiyo jumla ya sh. Mil 23.1 zilitumika.
Gharama
nyingine zinazoelezwa kutumika kwa maandalizi hayo ni pamoja na posho kwa maafisa
wa halmashauri hiyo ambao wanadaiwa kulipwa jumla ya sh mil 9 ikiwa ni takwimu
za hesabu za posho na malazi ya Sh120,000
mara siku 5 na waandishi wa habari pamoja na madereva watatu na magari ambapo inadaiwa kila
gari moja matengenezo na mafuta kwa safari
ya Dar es salaam ni sh milioni 1.
Hali
iliyoibua maswali kutoka kwa wadau mbalimbali mkoani Mbeya ni kitendo cha viongozi hao wa serikali kutumia
mamilioni ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya harambee ya kuchangisha fedha
kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza Jijini Dar es salaam badala ya harambee hiyo
kufanyika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.
‘’Hizi ni
mbinu tu za kutafuna fedha za walipa kodi, kutokea kwa janga la moto imekuwa
sababu za watu kutafuta mwanya wa kulamba fedha hakuna mantiki ya harambee
kwenda kufanyika Dar es salaam badala ya kufanyika hapa Mbeya huu ni ufisadi wa
namna yake’’, alisema mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye aliomba ahifadhiwe
jina lake kwa kuwa anaishi jirani na shule hiyo.
Mkazi huyo
alimuomba Rais John Magufuli kuwawajibisha wote waliohusika kwa namna moja ama
nyingine katika sakata hilo kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na ubadhirifu wa
wazi ulioandaliwa na watendaji wa serikali kutengeneza fursa ya kula mamilioni
ya walipa kodi.
Mbunge wa
jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi alipoulizwa juu ya sakata hili alikiri
kuwa yeye alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria ukumbi wa Ubungo Plaza kwa
ajili ya harambee iliyoandaliwa na viongozi wa serikali ya jiji la Mbeya na
kuwa hata hivyo harambee hiyo iliahirishwa katika hali ya utata.
‘’Mimi ni kati ya waalikwa waliohudhuria
kwenye harambee hiyo,watu wengi walijitokeza ukumbini Mkuu wa wilaya ya Mbeya alijitokeza
ukumbini na kuahirisha harambee hiyo,’’alisema Mbunge wa Mbeya mjini Joseph
Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.
‘’Mimi sio
msemaji, wasemaji ni waandaaji ambao ni serikali ya Jiji la Mbeya, mimi na
wenzangu tulihudhuria kama waalikwa maandalizi yote ya harambee yalifanywa na
Viongozi wa Jiji na Mkuu wa wilaya,’’alisema Mbilinyi.
Naye
Mwenyekiti wa kamati ya Maafa Marcel Ipini akizungumzia suala hilo alisema kuwa
mara baada ya mabweni ya shule ya sekondari Iyunga kuteketea kwa moto iliundwa
kamati ya maafa ambayo yeye ndiye Mwenyekiti na kuwa hata hivyo taarifa za
kuwepo kwa harambee Jijini Dar es salaam alizisikia kwenye vyombo vya habari
tu.
‘’Mimi kama
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa sikuwa na taarifa za harambee ya Ubungo Plaza,
harambee niliyoijua ilikuwa ifanyike Machi 23 ukumbi wa Mkapa, taarifa za
harambee za Ubungo Plaza ambayo tulisikia kuwa mgeni rasmi atakuwa Waziri mkuu
nimeisikia kupitia vyombo vya habari,’’alisema Ipini.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari Iyunga Stephen Mwakajumilo alisema kuwa hakuhusishwa
na harambee iliyopangwa kufanyika Ubungo Plaza na kuwa bodi ya shule hiyo
ilikuwa na mpango wa muda mrefu kwa kuwahusisha wanafunzi wote waliosoma
shuleni hapo kusaidia uboreshaji wa miundo mbinu tangu mwaka 2014.
‘’Sisi
tulianza mkakati wa maboresho ya miundo mbinu ya shule hiyo tangu mwaka 2014,
tulilenga wanafunzi waliowahi kusoma Iyunga popote walipo, lengo letu lilikuwa
ni kufanya Fund Rising ilikuwa bado hatujaandaa, lilipotokea janga hili, Mkuu
wa wilaya ya Mbeya na Mkurugenzi wa Jiji wakaamua kufanya harambee Jijini Dar
es salaam ambayo sisi hatukuhusishwa’’alisema.
Aidha kwa
mujibu wa msimamizi wa ufyatuaji tofali za shule hiyo Mchungaji Thomas Kabigi
alisema kuwa bweni moja linachukua takribani tofali 6,500 ambapo gharama ya
tofali moja inafikia sh.300 na kuwa kutokana na hesabu hiyo ya msimamizi wa
ufyatuaji wa matofali bweni moja linaweza kumalizika kwa tofali zenye gharama
ya sh milioni 1.95.
Kutokana na
hesabu hizo kiasi hicho cha fedha jumla ya sh.mil 50 zinazoelezwa kuwa huenda
zilitumika kwa ajili ya maandalizi ya harambee iliyoshindwa kufanyika zingeweza
kufyatua matofali mengi zaidi ambayo
yangekidhi kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo kongwe nchini.
Kulingana na taarifa za awali kupitia
matangazo yaliyokuwa yakitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini ni
kuwa jumla ya sh.mil 700 zilikuwa zikihitajika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni
ya shule hiyo ambazo zingeweza kupatikana kutokana na harambee iliyotakiwa
kufanyika Ubungo Plaza.
Ofisa Elimu
wa Mkoa wa Mbeya Charles Mwakalila alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema
kuwa maandalizi yote ya harambee hiyo yalikuwa yakifanywa na Mkuu wa wilaya na
Mkurugenzi wa Jiji na kwamba kwa sasa shule hiyo mwajiri wake ni TAMISEMI baada
ya kugatuliwa kwa madaraka kutoka serikali kuu.
‘’Kwa sasa
shule hiyo iko chini ya Halmashauri ya Jiji kwa kila jambo,maandalizi na mambo
yote yanayoihusu shule hiyo yapo chini ya Serikali za Mitaa, mkoa hauhusiki na
lolote,’’alisema Mwakalila.
Kaimu
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dkt Samwel Lazaro alipotakiwa kuelezea sakata hilo
baada ya kupigiwa simu yake ya kiganjani alikataa kuelezea lolote juu ya suala
hilo na kumtaka mwandishi kuwaeleza wengine wanaofuatilia jambo hilo kuwa yeye
hana jibu lolote kwa sasa.
‘’Tafadhali
naomba msiniulize jambo lolote kuhusiana na harambee, waambie na wenzio
wanaofuatilia jambo hilo sina lolote ninaloweza kulizungumzia,’’alijibu Dkt
Lazaro na kukata simu yake baada ya kupigiwa simu kutoa ufafanuzi juu ya sakata
hilo.
Naye Mkuu wa
wilaya ya Mbeya Nyerembe Munassa alipozungumza na gazeti hili alidai kuwa
mazingira ya kuahirishwa kwa harambee hiyo yaligubikwa na utata, ‘’harambee
iliahirishwa dakika za mwisho lazima tuwe honest tutajipanga vizuri,ukiambiwa
uahirishe, unaahirisha,tuliambiwa kulikuwa na uchaguzi Zanzibar viongozi
hawawezi kuwepo,’’alisema Munassa.
Taarifa za
kiuchunguzi ambazo gazeti hili inazo zinaeleza kuwa kuahirishwa kwa harambee
hiyo kumetokana na mambo ya kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kudaiwa kutaka
kupatia umaarufu tatizo la Iyunga na hivyo njia pekee bila kujali hasara
iliyokuwepo ilikuwa ni kuzuia harambee hiyo isifanyike.
‘’Kufanyika
kwa harambee hii kungewapaisha watu kisiasa, unajua sasa hivi watu wako njia
panda ukifanya kitendo kimoja tu kizuri kinaweza kukupaisha na ukifanya kitendo
kimoja tu kibovu kinaweza kukushusha kwa sakata hili watu watashushwa
tu,’’alisema mdau mmoja wa elimu ambaye naye hakupenda kutajwa jina lake kwa
madai ya kuwa ana maslahi katika shule ya Iyunga.
Naye Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya Amos Makalla ambaye alikuwa akifuatilia mjadala wa sakata hilo
kupitia mtandao wa Facebook kutokana na kichwa kilichosema Amos Makala
akaribishwa kwa skendo mkoani Mbeya alisema kuwa amefuatilia kwa makini sakata
hilo na kuwa kwa sasa yupo nje ya mkoa bali atakuwa na ziara April 5 shuleni
hapo.
‘’Nina ziara
ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya hapo Iyunga Sekondari nitatumbua hilo jipu siku hiyo ya tarehe
5,’’alisema Makalla.
Post a Comment