Ads (728x90)TANZIA!!!
Rais Dkt Magufuli akiweka saini kitabu cha Maombolezo kifo cha Mke wa Dkt Mwakyembe

 
Kulia ni Mke wa Dkt. Mwakyembe Linna George Mwakyembe enzi za uhai wakeRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison George Mwakyembe kufuatia kifo cha mkewe Bi. Linah George Mwakyembe kilichotokea usiku wa tarehe 15 Julai, 2017.
Bi. Linah George Mwakyembe amefariki dunia katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kushtushwa na kusikitishwa na kifo hicho, na amesema yeye na familia yake wanaungana na familia ya Dkt. Mwakyembe katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Nakupa pole sana Dkt. Mwakyembe kwa kuondokewa na mkeo mpendwa Bi. Linah, natambua hisia za maumivu ulizonazo wewe na familia nzima, nyote nawaombea Mwenyezi Mungu awatie nguvu, awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Namuombea Marehemu Linah George Mwakyembe apumzishwe mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amesali Ibada ya Jumapili ya 15 ya mwaka wa Kanisa iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato Mkoani Geita na ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.
Katika harambee hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amefanikiwa kuchangisha fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni 13, ahadi Shilingi 920,000/=, mifuko ya saruji 33 na malori 2 ya mchanga.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza waumini wa Parokia ya Chato kwa hatua kubwa waliyopiga katika ujenzi wa kanisa kuu la Parokia hiyo na amewataka kuendelea kujitolea kukamilisha hatua za mwisho za ujenzi huo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita

Post a Comment