Ads (728x90)



Mzimu wa tuhuma dhidi ya jeshi la polisi mkoani Mbeya umeendelea kuliandama jeshi hilo baada ya kuwepo kwa taarifa zingine za askari polisi wa wilayani Vwawa(mwenye namba G8I..jina linahifadhiwa) kuhusishwa na kashfa za kusambaza noti bandia.

Askari huyo anadaiwa kujihusisha na vitendo hivyo maeneo kadhaa kwa kununua bidhaa mbalimbali ambapo amedaiwa kufanya vitendo hivyo katika maeneo ya Ichenjezya aliponunua vocha ya muda wa maongezi y ash.10,000 ambayo baadaye ilibainika kuwa ni feki.

Imeelezwa kuwa alipotakiwa kueleza alikopata noti hiyo alijitetea kwa kudai kuwa aliipata kwa njia ambayo haifahamu katika ununuzi wa mahitaji yake ya kila siku.

Katika tukio la pili Disemba 7 hadi 10 inaelezwa kuwa askari huyo akiwa katika mji mdogo wa Mlowo aliingiza kiasi cha sh.100,000 kwenye huduma ya M-Pesa ambapo baadaye alishitukiwa.

Baadaye wakala wa duka ambalo askari huyo alipata huduma alitoa taarifa kituo cha Polisi Mlowo ambapo askari wenzie walimweka chini ya ulinzi na kumpekua na kukutwa na kiasi cha fedha zipatazo 400,000 za noti ya 10,000 ambazo pia zilikuwa ni bandia.

Katika hali inayoonesha kulindana ndani ya jeshi hilo askari wa kituo cha Mlowo inadaiwa walifanya usuluhishi baina ya wakala wa M-pesa na askari huyo alirejesha kiasi hicho cha fedha kwa wakala.Kufuatia hali hiyo askari hao walitoa ripoti ya tukio hilo kwa viongozi wake katika kituo cha Vwawa ambako ndiko kilipo kituo chake cha kazi.

Baada ya taarifa za tukio hilo kufikishwa kwa wakubwa wake wa kazi alienda kupekuliwa nyumbani kwake ambako alikutwa na fedha nyingine bandia zipatazo 100,000.

Alipotakiwa kueleza alikozipata fedha hizo inadaiwa  alidai kuwa aliziiba katika fedha ambazo ni vidhibiti ambavyo vimekamatwa na askari katika matukio mbalimbali.


Inadaiwa kuwa kufuatia tukio hilo taarifa hizo zimefikishwa makao makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dar es salaam ambao wameagizwa uchunguzi ufanyike na hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Advocate Nyombi alipotakiwa kuelezea tukio hilo alisema kuwa bado hajapata taarifa hizo na kwamba apewe muda ili atolee ufafanuzi baada ya kupata taarifa kutoka wilayani Mbozi.

Post a Comment