Na,
MwanaFasihi Wetu Mbozi
SHEREHE za
kuukaribisha mwaka mpya 2012 zilizoenda sanjari na maadhimisho ya siku ya Mwanamke
zilizoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake wilayani Mbozi (WADF
Mbozi) iliingia dosari mwishoni mwa wiki baada ya mgeni rasmi aliyealikwa
kujisaidia haja ndogo ukumbini.
Sherehe hizo
ambazo zimefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Kanisa katoliki wa
‘Mkonongo’ ziliwahusisha viongozi mbalimbali wa chama tawala na serikali ambapo
Mgeni rasmi aliingia ukumbini humo huku akiwa amelewa chakari akiwa amevaa
suruali aina ya Cool Dry.
Kiongozi
huyo wa juu serikalini aliyeonekana akiwa na dalili za kupata kilevi aliingia
ukumbini majira ya saa 1:30 na kupita moja kwa moja kwenye meza kuu na kuungana
na viongozi wengine waliokuwa wakiendelea kufurahia sherehe hiyo ya akina mama.
Muda mfupi
baadaye kiongozi huyo alionekana akiwashika shika akina mama walioketi meza kuu
sehemu mbalimbali za miili yao
na kusababisha kero miongoni mwa waalikwa wa sherehe hizo ambapo baadaye
alisimama kwa ajili ya kuelekea msalani huku eneo aliloketi likiwa limelowa
maji.
Bwana mkubwa
kabla hajafika katika mlango wa kuelekea msalani alijikuta akimalizia haja zake
aliposimama na kuongeza ubichibichi katika suruali yake aliyovaa huku baadhi ya
viongozi walioketi meza kuu wakitaharuki kuona namna ambavyo mwakilishi huyo wa
wilaya akiwa katika hali ya ajabu.
Baadhi ya
waalikwa na viongozi wengine wa serikali na chama tawala walistaajabishwa na
kitendo cha kiongozi huyo na kujikuta wakifumba macho kwani kila hatua
aliyotembea iliacha alama za maji maji yaliyendelea kuchuruzika katika suruali
yake na kufanya ukumbi mzima kushika tama kutokana na heshima aliyokuwa nayo
kwa wananchi kiongozi huyo.
Wakizungumzia
tukio hilo baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo walisema kuwa tabia za
kiongozi huyo zimewatia aibu wanawake waliomualika na kuwa hafai kuwa kiongozi
kwani ameonesha dalili za utovu wa nidhamu na kutojiheshimu.
Akizungumzia
lengo la sherehe hizo Mratibu wa taasisi hiyo ya wanawake wilayani Mbozi Bi. Happiness
Kwilabya alisema kuwa waliamua kufanya sherehe hizo ikiwa hitimisho la shughuli
mbalimbali za kijamii ambazo wamekuwa wakizifanya tangu mwaka mpya uanze.
Alisema kuwa
awali walitembelea vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima na kula nao chakula,walifanya
shughuli mbalimbali za usafi katika maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo
hospitali ya wilaya ya Mbozi pamoja na kuwatembelea wagonjwa na kuwapa
matumaini.
Post a Comment