Ads (728x90)

BIBI SOMOE ISSA AJUZA ALIYETISHIA GESI KUGEUKA MAJI

MHARIRI WA BLOG YA KUSINI AKIANGALIA MABAKI YA GARI LILILOCHOMWA MOTO NA WANANCHI KIJIJI CHA MSIMBATI

BAADHI YA WANANCHI WA MSIMBATI WAKIANGALIA MABAKI YA GARI LILILOCHOMWA MOTO

AISHA HAMISI MTOTO WA AJUZA ALIYETISHIA GESI KUGEUKA MAJI





Na, Waandishi wetu Mtwara
SAKATA la gesi ya Mtwara limechukua sura mpya bada ya Ajuza mwenye umri wa miaka 90 kutishia kuwa iwapo gesi hiyo itasafirishwa kuelekea Jijini Dar es salaam itageuka maji.
Ajuza huyo mkazi wa Msimbati Mtwara inakotokea gesi hiyo Somoe Issa(90) ambaye ametambulishwa kuwa ni mkuu wa kaya ya Msimbati inadaiwa kuwa mara baada ya kutamka maneno hayo alianza kufuatiliwa na viongozi wa serikali.

Taarifa zaidi zinadai kuwa bi mkubwa huyo aliandaliwa safari ya kuondoka kijijini hapo kwa gari maalumu hali ambayo iliibua hofu kwa wanakijiji ya kwamba huenda  bibi huyo angetoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ni kwamba kijiji hicho cha Msimbati ndicho a,mbacho miradi ya uvunaji wa gesi hiyo asilia ilipo na kwamba mtu mmoja anayedaiwa kuwa ana asili ya kijiji hicho aliwasili kijijini hapo akiwa na gari ndogo aina ya Mark II kwa nia ya kwenda nyumbani kwa shangazi yake .
Inaelezwa kuwa majira ya saa mbili usiku alikwenda nyumbani kwa bibi Mtiti akiwa na gari hiyo kwa maelezo kuwa alikuwa akienda kwa shangazi yake aliyetambulika kwa jina la Fatuma Said Tom.

Hata hivyo imedaiwa kuwa wakazi wa kijiji hicho wameweka ulinzi kwa bibi huyo kwa madai kuwa kufuatia taarifa alizotoa juu ya tishio la gesi hiyo kugeuka maji kwamba amekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kwa nia ya kupotezwa katika mazingira ya kutatanisha.
Mkazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Juma Ayoub alisema kuwa wakazi wa maeneo hayo walilifuatilia gari hilo kwa karibu mara walipoliona nyakati za usiku.Naye Asha Hamisi alisema kuwa yapata majira ya saa mbili usiku walikuja watu wawili ambao walihitaji kuongea na Bibi huyo wakidai kuwa wanataka kwenda naye Mtwara.
Alisema kuwa watu hao walidai kuwa wametumwa na Rais Kikwete na Hawa Ghasia wazungumze na bibi huyo kuhusu mambo ya gesi na kwamba iwapo bibi huyo yupo tayari watamfuata jumanne ijayo ili waondoke naye.

Hata hivyo anasema kuwa wakiwa katika majadiliano hayo ghafla alipochungulia nje aliona umati wa watu wamekusanyika.

Naye Manzi Mohamed Faki ambaye ni motto wa tano wa bibi huyo anasimulia kuwa walimfuata jamaa huyo kwamba aondoke eneo hilo na afute wazo alilojia na kwamba walimsihi kwa muda mrefu aondoke lakini hakuwasikiliza na kwamba kadri muda ulivyozidi kusonga ndivyo ambavyo watu waliendelea kujaa eneo hilo na kuanza kumrushia mawe ambapo alikimbia na kutelekeza gari lake ambalo na hatimaye liliteketezwa kwa moto.

Kwa upande wake shangazi wa kijana huyo ambaye gari lake liliteketezwa kwa moto Fatuma Tom alisema kuwa alimpokea mwanaye ambaye alimuomba amsindikize kwa bibi huyo ambapo alisema kuwa yeye ametumwa na wakubwa wake wa kazi amchukue bibi huyo aende naye Dar es salaam.

 ‘’Huyu ni mwanangu mtoto wa kaka yangu anaishi Dar es salaam anafanya kazi usalama wa Taifa’’ alisema Bibi Tom.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Salum Tostao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini alisema kuwa ofisi yake haina taarifa ya kumpokea mgeni wa kiserikali na kwamba gari lililoteketea kwa moto ni mali ya Mussa Babu lenye namba za usajili T 609 BXG.Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Maria Nzuki amedai kuwa hana taarifa za tukio hilo kwa madai kuwa hakuna mtu aliyelalamika kuchomewa moto gari lake.(taarifa hizi ni kwa hisani ya Hassan Samli wa Mtwara na blogu ya kusini zilizotolewa kwenye mtandao wa jamii forums)





Post a Comment