Ads (728x90)

Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Swila Martin Shadrack Kebesho ambaye anadaiwa kutoweka shuleni baada ya kutandikwa viboko 45
Wanahabari na viongozi wa shule wakiwa nje ya shule ya sekondari Swila ambako mwanafunzi Martin alikuwa akisoma
Shule ya sekondari Swila
Mkuu wa shule ya sekondari Swila Charles Kibona
Wanafunzi wa shule ya sekondari Swila waiwa katika ofisi ya Mkuu wa shule wakitoa ushuhuda namna ambavyo mwanafunzi mwenzao alivyotoweka shuleni
Mwanafunzi Ali Mohamed akizungumza na waandishi wa habari juu ya sakata la kutoweka kwa mwanafunzi mwenzao baada ya madai ya kuadhibiwa na mwalimu kwa kutandikwa bakora 45
Mkuu wa Shule Mwalimu Kibona akiwasiliana na Mmiliki wa shule juu ya ujio wa waandishi wa habari shuleni hapo
Nje ya geti la shule ya sekondari ya Swila kabla ya waandishi wa habari hawajaingia shuleni
Walezi wa mwanafunzi Martin Agusta John na Erasto Jackson wakihaha kumtafuta mtoto wao katika hospitali Teule ya Ifisi baada ya kuhangaika bila mafanikio kujua alipo.
Viunga vya shule ya sekondari Swila
Walezi wa mwanafunzi Martin wakizungumza na Diwani wa kata ya Nsalala juu ya kutoweka kwa mwanafunzi katika shule ya Swila iliyopo kata ya Nsalala wilaya ya Mbeya.

ZIKIWA zimetimia wiki  tatu bado kuna utata uliogubikwa juu ya mahala alipo Mwanafunzi  wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Swila wilayani Mbeya mkoani hapa Martin Shadrack Kebesho(16) ambaye walezi wake wamekuwa wakimtafuta bila mafanikio baada ya kutoweka kwa mazingira tata kwa kile kilichodaiwa kuwa aliadhibiwa viboko zaidi ya 40 na walimu wake.

Matukio ya aina hii yamekuwa yakiendelea huku kukiwa na jitihada mbalimbali za taasisi zisizo za kiserikali kupiga vita ukatili wa kijinsia, ambapo chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimekuwa kikitoa elimu kupinga ukatili katika mradi wake wa GEWE-11  wanahabari wameendelea kujengewa uwezo wa kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Sababu za kuadhibiwa mtoto huyo zinaelezwa kuwa zimetokana na mwanafunzi huyo kupata alama chini ya 50 za somo la kompyuta adhabu ambayo ilitolewa kwa wanafunzi kadhaa wa kidato cha pili na mwalimu wa somo hilo aliyefahamika kwa jina moja la Patrick akichangiwa na mwalimu aliyefahamika kwa jina la Given ambaye anadaiwa kuwa ni Mwalimu wa somo la Kiswahili.

Ilielezwa kuwa Mwanafunzi huyo alitoweka March 15 baada ya adhabu aliyopewa March 14 na kwamba kabla ya kupewa adhabu hiyo, wanafunzi wenzie waliadhibiwa mstarini kwa kutandikwa fimbo nne kila mmoja wakati yeye akiwa hayupo.

Kwa mujibu wa maelezo kutoka shuleni hapo ni kwamba Mwalimu wa somo la kompyuta aliwaita wanafunzi kwa ajili ya kutekeleza adhabu hiyo lakini mwanafunzi Martin hakuwepo mstarini ambapo siku ya pili alipofika walimu walimchangia kwa kumpiga viboko mfulululizo na kumsababishia maumivu makali.

Taarifa zaidi zinadai kuwa Mwalimu Patrick alimpiga kibao mwanafunzi huyo na kisha kumburuta hadi ofisini ambako huko akaanza kuadhibiwa kwa kuchangiwa na walimu wawili kwa idadi ya viboko vinavyoelezwa kuwa ni 45.

''Baada ya kuadhibiwa alibaki bwenini hakurudi mstarini, tulipofika bwenini tulimkuta akiwa hoi hajiwezi, alituomba tukamchukulie Chai, tulipoileta hakuweza kuinywa,nilijaribu kumkanda mguu wake uliokuwa umevimba kwa maji ya moto,''alisema mmoja wa wanafunzi hao (ambaye tunalihifadhi jina lake kwa sababu maalumu).

Alisema kuwa siku ya pili wakiwa mstarini walimu walimuuliziaMartin na kujibiwa kuwa yupo bwenini anaumwa baadaye waliamriwa kumfuata na kumleta mstarini huku wakiwa wamembeba  na baadaye walimrejesha bwenini baada ya kuona hali yake ikiwa mbaya.

''Tulimrejesha bwenini akiwa hoi, tuliporudi baadaye hatukumkuta, hatukujua ni wapi ameenda akiwa katika hali ile ya maumivu makali,''alisema mwanafunzi mwingine kati ya wanafunzi nane waliohojiwa tukio la kipigo cha mwanafunzi huyo.

Mara baada ya kupata  taarifa hizi mwandishi wa habari hizi aliwafuatilia wazazi wake waishio eneo la Magereza Jijini Mbeya na kukutana na walezi wa mtoto huyo ambao ni mama yake mkubwa Agusta John na baba yake mlezi ambaye ni Ofisa ya Jeshi la Magereza Erasto Jackson.

Wakizungumza kwa kupokezana wakiwa katika hali ya majonzi wazazi hao walisema kuwa, hawajui alipo mtoto wao na kwamba wamemtafuta katika maeneo yote muhimu kuanzia hospitali zilizopo katika jiji la Mbeya na Chumba cha kuhifadhia maiti bila mafanikio.

'' Tarehe 17 March nilipigiwa simu kutoka shuleni kuwa Martin hayupo, nikajiuliza ni kwa nini hayupo, mimi na mama yake mkubwa tukafuatilia shuleni kujua sababu za kutoweka kwa mtoto huyo,''alisema Jackson.

Alifafanua kuwa walipofika shuleni walikutana na walimu ambao walisema kuwa mwanafunzi huyo ametoweka na kwamba mara baada ya kutoweka walitoa taarifa kituo cha polisi.

''Tuliamua kuwauliza baadhi ya wanafunzi wanaosoma na Martin sababu za kutoweka kwa mwenzao, walisema kuwa Mwalimu Patrick na Given walimchangia kwa kumpiga viboko 45, na kuwa alipata maumivu makali yaliyomsababisha ashindwe kufanya mtihani,''alisema Agusta Mama mkubwa wa Martin.

Alisema kuwa walitatanishwa na kauli hizo zinazopishana kati ya walimu na wanafunzi ambapo walimu wanasema mwanafunzi ametoroka ilhali wanafunzi wenzie wakisema kuwa mwenzao alipigwa viboko zaidi ya 40 kwa kuchangiwa na walimu wawili.

Agusta alisema kuwa hata hivyo walimu walipaswa kufuata taratibu za adhabu kwa mtoto ikiwa ni pamoja na kuitisha kamati na kusaini katika daftari jeusi iwapo mtoto anapaswa kupigwa viboko ambavyo hutolewa na Mkuu wa shule au mwalimu mwingine kwa idhini ya Mkuu wa shule.

Alisema kuwa walijaribu kuwauliza walimu kama taratibu hizo zilifuatwa na kushindwa kutoa maelezo ya kueleweka ndipo walipoenda kufungua jalada la kutoweka kwa mwanafunzi baada ya kipigo katika kituo cha Polisi cha Kati cha Jijini Mbeya kwa namba MB/IR/2432/2014.

Katika kufuatilia tukio hilo mwandishi wa habari hizi alikutana na Mwenyekiti wa mtaa wa Kanani ilipo shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Bahati Nyalile ambaye alisema kuwa hajapata taarifa zozote za kutoweka kwa mtoto huyo na kwamba kwa hatua hiyo alilazimika kufuatana na waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio hilo hadi shuleni.

Baada ya kufika shuleni na kukutana na Mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Charles Kibona alikanusha kupigwa kwa mwanafunzi huyo na kudai kuwa mwanafunzi huyo alitoroka shuleni hapo akikwepa aibu kwa kisingizio cha kupigwa viboko na walimu.

Mkuu wa shule aliwaita baadhi ya wanafunzi wanaodaiwa kusoma na Martin, Ali Mohamed na Jovin Vitalis(sio waliohojiwa mara ya kwanza) ambao walidai kuwa mwanafunzi mwenzao alitoroka shuleni kwa kuruka ukuta huku wakimsaidia kumbebea begi lake wakati anatoroka.

Kwa upande wao walezi wa mwanafunzi huyo walidai kuwa kauli hiyo si ya ukweli kwa kuwa inapingana na kauli ya mwanzo ya Mkuu wa shule ambaye aliongea kupitia kinasa sauti huku akiwabembeleza wazazi kushirikiana kumtafuta mwanafunzi huyo.

Aidha katika hali isiyo ya kawaida askari polisi waliotumwa kupeleleza kesi hiyo(majina tunayo) waliwataka walezi wa mtoto huyo watoke nje ya ofisi ya Mkuu wa shule na baadaye mazungumzo yao yaliyonaswa katika kinasa sauti yakionesha askari hao wakiwapa maelekezo walimu namna ya kukwepa tuhuma hizo.

''Jazeni katika Log Book kwamba mmeidhinisha kupigwa kwa mwanafunzi huyo kisha gonga mhuri, mkifanya hivyo mmemaliza kila kitu,,,''ilisikika sauti ya mmoja wa askari akitoa maelekezo yaliyoambatana na vicheko katika ofisi ya Mkuu wa shule.

''Lakini hebu tueleze ukweli ''how many stick do you stick that young Boy....(vicheko) tueleze ulimpiga viboko sita!! kumi au vingapi, sasa fanyeni hivyo ili kurekebisha hili tatizo,''ilisikika sauti hiyo ikisisitiza.

Taarifa za kutopatikana kwa mwanafunzi huyo zimetoa mtazamo tofauti katika familia hiyo na kubaki njia panda huku wakisema kuwa wanashindwa kuweka matanga ya msiba kwa kuwa hadi sasa wako katika kitendawili cha kutojua ni wapi alipo mtoto wao.

''Angekuwa na tabia mbaya tungemjua kwani nimemlea mwenyewe tangu akiwa mdogo hadi alipoanza elimu ya msingi na sekondari, ni mtoto wa mdogo wangu amezaliwa nyumbani kwangu, baba yake alifariki siku nyingi! ni yatima'' alisema Agusta mama mkubwa wa mtoto huyo.

Mwandishi wa habari hizi alifanya jitihada zaidi kumtafuta  Mkurugenzi wa shule hiyo Happy Swilla ili aweze kuelezea tamko la shule juu ya sakata hili hakuweza kupokea  simu yake ambayo iliita na kupokelewa ambapo alipoelezwa kuwa anaongea na mwandishi wa habari anayefuatilia tukio la kupotea kwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo, simu yake ilikatwa na kuendelea kuita bila kupokelewa.

Kwa upande wake Jeshi la Polisi kupitia kwa  Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Barakael Masaki alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa hana taarifa nalo na kueleza kuwa atalifuatilia kujua undani wake na wapi lilipoishia.


Post a Comment

  1. Alikuja kupatikana? Haya mambo ni ya kawaida sana huku Tanzania na yanatokana na kukosekana kwa ustaarabu (UshenzI). Ni wazi kuwa psychology ya huyo aliyetoweka ilipelekea yeye kufanya hivyo, kama ni yatima ataona kuwa hakuna anayemjali na labda uonevu umetokana na hiyo hali yake. Safari ya Maendeleo ya Tanzania ni ndefu, na ni ndefu kuliko tunavyofikiri, huu ni ushahidi tosha. Maendeleo si uchumi tu bali na jamii pia (Universal Civilization). Kuna wale wano tetea African Civilization, labda niulize kwani mwafrika ana mahitaji tofauti na mzungu au oriental?

    ReplyDelete