Ads (728x90)

Mkulima wa kijiji cha Jojo Esther Mboma akipanda maharage katika shamba lake ambalo awali lilikuwa ni shamba la pareto, ameamua kung'oa pareto kwa madai kuwa zao hilo limeingiliwa na walanguzi na hivyo kusababisha kukosa tija kwa kilimo cha pareto.
Mchungaji wa Kanisa la Jeshi la Wokovu la kijiji cha Pashungu Johnson Nyamuhanga  akionesha shamba la hekari mbili la pareto la kanisa hilo ambalo limetelekezwa bila kuchumwa maua kutokana na kile alichoeleza kukosekana kwa soko la uhakika kwa zao hilo msimu huu.

Shamba la pareto lililotelekezwa bila kuchumwa

Mwandishi wa Blog hii akishuhudia wakulima wa kijiji cha Nsheha wilaya ya Mbeya waking'oa pareto iliyotelekezwa kwa ajili ya kupanda viazi, wakidai kuwa pareto kwa sasa haina manufaa kwao kutokana na kukosa ushindani wa soko.
Wakulima wa kijiji cha Nsheha wakilima kuondoa maua ya pareto yaliyotelekezwa ili kupanda maharage



Mwenyekiti wa kijiji cha Pashungu Akson James akonesha shamba la Viazi ambalo hapo mwanzo lilikuwa ni shamba la Pareto


Eneo la shamba la viazi upande mmoja na maharage upande wa pili, awali shamba hili lilikuwa ni shamba la pareto mmiliki wa shamba hili katika kijiji cha Pashungu wilayani Mbeya ameamua kufanya mabadiliko baada ya zao la pareto kutokuwa na tija




KATIKA hali isiyo ya kawaida baadhi ya wakulima wa zao la Pareto katika vijiji vilivyopo kata ya Santiliya, Isuto na Itawa wilayani Mbeya wameamua kutelekeza mashamba ya pareto kwa kung’oa maua yaliyopo kwa ajili ya kulima mazao mengine ya kibiashara ya maharage na Viazi mviringo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wakulima katika vijiji vya Nsheha,Jojo na Pashungu kata za Santiliya na Itawa waking’oa pareto mashambani kwa madai kuwa zao hilo kwa sasa limekosa soko.
Wakizungumza katika maeneo mbalimbali ya mashamba kwenye vitongoji vya Pashungu,Idunda na Sakukwa katika kata ya Itawa na vitongoji vya Jojo a Shigamba katika vijiji cha Jojo na Shigamba kata ya Santiliya baadhi ya wakulima hao walisema kuwa kwa sasa zao hilo limeingiliwa na matapeli wanaochukua pareto yao bila kuwalipa.
‘’Tunalima kwa gharama zetu, maua yakiwa tayari wanakuja matapeli wanaokopa maua bila kulipa, hatujalipwa maua yetu kwa zaidi ya miezi nane,’’alisema  Ezekiel Satiel mkulima mkazi wa kijiji cha Pashungu.
Alisema kuwa serikali ndiyo iliyosababisha wakulima waamue kung’oa pareto na kulima mazao mengine biashara, tulijitokeza kulima kwa wingi zao la pareto, msimu uliopita sasa hivi kila nyumba ya mwanakijiji wamekumbwa na njaa,pareto imechukuliwa kwa mkopo bila kulipwa,’’alisema Satiel.
Naye Bahati Sifuku mkulima wa Pashungu alisema kuwa alikopesha pareto yake kwa kampuni moja kubwa (jina linahifadhiwa kwa sasa) lakini hadi sasa imepita miezi minne hajalipwa fedha yake na kuwa kutokana na hali hiyo shamba lake la pareto ameamua kulima maharage badala ya pareto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Pashungu Akson James alisema kuwa eneo kubwa lililokuwa linalimwa pareto kwa sasa yamelimwa mazao mengine ya Viazi na maharage na baadhi ya mashamba ya pareto yametelekezwa na kuota majani bila kupaliliwa.
Alitaja moja ya shamba la hekari mbili ambalo limetelekezwa kuwa ni shamba la Umoja wa kanisa la Jeshi la Wokovu la kijiji hicho, ambapo kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Johson Nyamuhanga alisema kuwa wameamua kulitelekeza shamba hilo bila kuvuna kutokana na kukosekana kwa soko.
‘’Shamba letu ni hekari mbili tumeamua kuacha pareto iharibike kwa kuwa hakuna pa kuiuza, waumini wapo kwenye mashamba yao wanang’oa pareto na kulima viazi,hata tungechuma hakuna pa kupeleka tumeamua kuliacha kama lilivyo,’’alisema Mchungaji Nyamuhanga.
Mchungaji Nyamuhanga alisema kuwa makadirio ya ukubwa wa shamba hilo wangeweza kuvuna gunia sita ambazo ni sawa na kgm 300 ambazo wangeuza kiasi cha sh.600,000 kwa bei y ash.2000 kwa kilo moja ya pareto.
Naye Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Jojo kilichopo kata ya Santilya Anderson Yamaliha alisema kuwa zaidi ya vijana ambao ni nguvu kazi ya kijiji wapatao 600 wamejikuta wakiachana na kilimo cha pareto na kulima mazao mengine ya biashara kama vile viazi na maharage ili waweze kujiongezea uchumi.
Alisema kuwa moja ya sababu zilizowafanya waachane na kilimo cha pareto limetokana na kushuka kwa ghafla kwa bei kutoka sh.2400 hadi sh.1800 kutokana na kuwepo kwa ukiritimba wa ununuzi wa zao hilo.
Alisema kuwa msimu uliopita wakulima waliongeza kilimo cha zao hilo baada ya bei kupanda hadi kufikia 2500 lakini baada ya kukosekana ushindani wa ununuzi kwa makampuni mengi limebaki kampuni moja ambalo linawakopa wakulima  kwa sh. 2000 na malipo huja baada ya miezi kadhaa.



Post a Comment