Ads (728x90)

Kikosi cha Mbeya City kikishangiliabaada ya ushindi katika moja ya mechi zake za ligi kuu
USIA WANGU KWA VIJANA WA MBEYA CITY
LIGI kuu ya Vodacom imemalizika, Mbeya City timu ambayo imejizolea umaarufu wa aina yake katika ligi hii imemalizika ikiwa imeshika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC na Yanga zote za Dar es salaam.
Ni wazi kuwa ligi hii imekuwa na changamoto za kipekee kwa timu ngeni hususani Mbeya City ambayo mbali na kuwa ngeni katika ligi hii bali imeibua hisia mpya za hamasa kutoka kwa mashabiki ambao awali kabla ya kupanda kwa timu hiyo, wengi wao walikuwa wamejikita katika hamasa na ushabiki wa mambo ya kisiasa.
Historia ya soka mkoani Mbeya haiwezi kukamilika bila kuzitaja timu ambazo zimewahi kufanya vizuri katika ligi hiyo nchini kama vile, Tukuyu Stars,Mecco,Tiger na Prison ambazo zote kwa nyakati tofauti zilikuwemo katika ligi hiyo  na kutoa hamasa ya mchezo wa soka mkoani Mbeya.
Kwa msimu huu wa ligi chini ya kocha Juma Mwambusi Mbeya City imeweza kugangamala na kuzitoa jasho timu kongwe katika ligi hiyo na kuonesha njia ya matumaini ya kufanya vyema katika ligi hii kama ilivyokuwa kwa kaka zao Tukuyu Stars ambayo kwa mara ya kwanza ilipanda daraja mwaka 1986 na mwaka huo huo kuchukua kombe.
Ilikuwa ni historia ya kutumainiwa kwa kizazi kipya cha soka nchini kwa mwaka ule wa 1986 ambapo chini ya ufadhili Ramnik Patel (Kaka)timu ya Tukuyu Stars ambayo ilikuwa ni maarufu kwa jina la utani la ‘’Banyambala’’ iliweza kupanda daraja na kutwaa ubingwa na kuonesha maajabu ya timu za mikoani kuzichachafya timu za Dar es salaam.
 Ili kuweka vyema historia ya soka mkoani Mbeya ni vyema nikakitaja kikosi cha Tukuyu Stars ambacho kilivunja mwiko na kuiweka Mbeya katika ramani ya soka nchini baada ya kutwaa kombe na kufanikiwa kushiriki klabu bingwa bara la Afrika na klabu bingwa Afrika Mashariki mwaka 1987 na kuweza kutoka sare ya bao 1-1 na timu ngumu ya AFC ya kampala ambayo awali ilikuwa ikifahamika kwa jina la Abaluya.
Wachezaji waliounda kikosi cha Tukuyu Stars chini ya kocha Athuman Juma, walikuwa ni mlinda mlango Mbwana Makata,walinzi wa kati Ali Chimwaga na Daniel Chundu, Walinzi wa pembeni Godwin Aswile,Suleiman Mathew na Aston Pardon(marehemu).
Viungo wa ulinzi Yusuf Kamba na Peter Mwakibibi, viungo wa ushambuliaji, Richard Lumumba(marehemu) na Kevin Haule,Viungo wa pembeni,Karabi Mrisho na Suleiman Mwankenja.
Baada ya kuonekana kufanya vizuri katika ligi hiyo timu hiyo iliimarisha zaidi usajili wake kwa mwaka uliofuata na kuongeza wachezaji mahiri kama vile akina Asanga Aswile,Ali Mrisho, Salum Kabunda, Justin Mtekele(marehemu),Golikipa Joshua Kilale,Salum Kussi,Michael Kidilu, Jimmy Mored na Steven Mussa(Marehemu).
Pamoja na mafanikio hayo Tukuyu Stars ilikumbana na changamoto nyingi za wachezaji wake kuhamia katika timu kubwa za Yanga na Simba ambapo timu hiyo ilishuhudia wachezaji wake mahiri kama vile akina Godwin Aswile, Suleiman Mathew,Salum Kabunda,Steven Mussa na wengineo wakihama timu hiyo.
Ikumbukwe kuwa Tukuyu Stars ilikuwa ni mwiba mchungu kwa timu ya Yanga ambayo wakati ule ilipofanikiwa kupanda ligi kuu na kuchukua  ubingwa timu ya Yanga ilishindwa kuwatambia wageni hao ambapo kwa michezo yote miwili ilifungwa na timu hiyo kwa bao 1-0 mechi iliyochdezwa mjini Mbeya na 2-1 katika mechi ya marudiano Jijini Dar es salaam.
Kutokana na historia hiyo ya Tukuyu Stars ambayo ilishuka daraja mwaka 2008 ikiwa chini ya kocha wa sasa wa Mbeya City Juma Mwambusi, kuna mambo ya msingi ambayo inapaswa kuzingatia ili kujihakikishia kuwa inadumu katika medani ya ligi kuu kwa miaka mingi ijayo na hata kutwaa ubingwa.
Pamoja na mafanikio iliyoonesha Mbeya City kwa msimu wa ligi iliyomalizika jana yapo mapungufu mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na kuiweka timu hiyo katika mafanikio ya ligi kwa msimu ujao.
Katika jumla mechi 26 ilizocheza timu ya Mbeya City imeshinda mechi 13 imetoka sare mechi 10 imepoteza michezo 3, imefungwa jumla ya magoli 32 na kufunga magoli 21 na kujikusanyia jumla ya pointi 49 ikishikilia nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi hiyo.
Hadi inamaliza mzunguko wa kwanza timu hiyo kama ilivyokuwa kwa timu mabingwa wa msimu huu wa ligi Azam ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo hata mmoja.
Katika mzunguko wa pili wa ligi timu hiyo kama vile iliyoanza kulewa sifa ikajikuta ikipoteza mechi tatu, ilifungwa na Yanga ambayo katika mzunguko wa kwanza iliweza kugangamala na kutoka nayo suluhu,ikafungwa na Coastal Union Jijini Tanga na baadaye kupoteza mechi muhimu ya kutumainiwa iliyowapa ubingwa Azam katika uwanja wa nyumbani wa Sokoine.
Yapo mengi yaliyoibuka katika mechi hiyo ikiwemo minong’ono iliyoibuka hata kabla ya mechi hiyo kwamba Mbeya City imeiuza mechi hiyo na kwamba kwa hali ilivyo ni lazima timu ya Azam itashinda mechi hiyo na kujihakikishia ubingwa kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
Kama zilivyokuwa fununu za mwanzo Mbeya City iliingia uwanjani na kuonekana ikicheza chini ya kiwango huku washambuliaji wake wakishindwa kulisogelea lango la Azam na kusababisha katika kipindi chote cha kwanza mpira ukichezwa nusu uwanja.
Ni mara chache wachezaji wa Mbeya City walionekana kulikaribia lango la Azam hali ambayo baadhi ya mashabiki walianza kuingiwa na hofu kuwa huenda timu hiyo inaweza kufungwa na Azam ambapo dakika moja kabla ya kwenda mapumziko mchezaji Gaudence Mwaikimba wa Azam alifanikiwa kuandika bao la kuongoza kwa timu yake.
Kipindi cha pili kilianza kwa kuonekana uhai kwa timu ya Mbeya City, maelekezo ya mwalimu yalianza kuonesha matumaini ya timu hiyo kurejesha matumaini kwa mashabiki na hatimaye dakika 70 mchezaji wa Mbeya City Mwagane Yeya alifanikiwa kusawazisha bao hilo kwa tiktaka.
Matarajio ya kufanya vizuri kwa kikosi hicho yalianza kuingia na dosari ya mwamuzi wa mechi hiyo Nathan Lazaro wa Kilimanjaro aliyedaiwa kuibeba timu ya Azam akisaidiwa na washika vibendera wake Abdallah Uhako na  Godfrey Kihwili wote kutoka Jijini Arusha.
Matokeo ya mchezo huo yalisababisha vurugu kwa mashabiki hata baadhi ya wachezaji walionekana kumzonga mwamuzi, hata hivyo kuna mambo mengi ya kujifunza kwa timu hiyo kutokana na mtiririko mzima wa ligi hiyo na jinsi ilivyomalizika.
Zipo lawama za moja kwa moja ambazo Mbeya City haipaswi kuzikwepa, kujisahau baada ya kuona imeanza kupata umaarufu,kucheza chini ya kiwango na kuipa Azam ushindi na kutwaa kombe kabla ya kumalizika kwa ligi.
Mbeya City bado haijavunja rekodi iliyowekwa na kaka zao wa Tukuyu Stars, inapaswa kujiwekea mikakati mbadala ya kuimarisha kikosi kwa kuenzi jitihada za wadau wa soka wa mkoa wa Mbeya na kwingineko ambao kwa namna moja ama nyingine walikuwa wakiitakia mafanikio timu hiyo kwa hali na mali.
Kama mdau wa soka na mwandishi wa habari za michezo sitaacha kuyasema haya ili iwe chachu ya maendeleo ya klabu hii ambayo mbali na kurejesha hamasa za soka Jijini Mbeya imesaidia kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Jiji hilo ambapo mbali na viingilio vinavyopatikana milangoni, wageni wengi kutoka mikoa ya jirani huja kuishangilia timu hiyo.
Mbeya City inatakiwa ijifunze kwa watangulizi wake ambao hadi sasa wanaonekana kusuasua katika ligi hii, ikumbukwe pia timu ya Prison iliyodumu katika ligi hii muda mrefu ilishuka daraja mwaka 2011 ikiwa chini ya kocha ambaye kwa sasa ndiye kocha wa Mbeya City Juma Mwambusi.
Hadi sasa bado inaendelea kupumulia mashine kwa kila msimu kunusurika kushuka daraja ambapo kwa msimu huu almanusura ishuke daraja ambapo imemaliza ligi hiyo ikiwa na jumla ya pointi 28 ikiwa na jumla ya michezo 26 na kufungwa jumla ya magoli 25 huku ikiwa imeshinda mechi 6 na kutoa sare mechi 10 na kupoteza mechi 10.
Timu ya Mbeya City inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambapo imepanda daraja msimu huu wa ligi.
Kikosi cha Mbeya City kiliongozwa na kocha Juma Mwambusi na wachezaji  David Burhani/Geofrey Julius,Hassan Mwasapili/Mohamed Kijuso,Hamad Kibobile,Yusuf Abdallah,Yohana Morris,Christian Sembuli,Hamid Mohamed,Kenny Ally,Saad Kipanga,Mwagane Yeya,Deus Kaseke,Aziz Sibo,Antony Matogolo,Yusuf Wilson,Francis Castor na Jeremiah John.
  

Post a Comment