Ads (728x90)

Waendesha Bodaboda 37 watuhumiwa wa Vurugu wakiwa katika mahakama ya Mwanzo ya Jiji la Mbeya leo jioni






Baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakamani hapo jioni hii kutaka kuwachukulia dhamana ndugu zao hata hivyo dhamana kwa washitakiwa imekataliwa

Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda Jiji la Mbeya Vicent Mwashoma akiwa katika mahakama ya mwanzo mara baada ya kesi ya waendesha bodaboda kuahirishwa leo jioni

Picha hizi za (Mbeya yetu Blog) zikionesha namna ambavyo barabara ilifungwa wakati wa vurugu hizo na harakati za Jeshi la Polisi kudhibiti vurugu hizo Jijini Mbeya leo asubuhi

`Baadhi ya  ndugu wa washitakiwa wa vurugu wakilia baada ya ndugu zao kunyimwa dhamana
Waendesha bodaboda 37, wanaodaiwa kufanya vurugu leo asubuhi Jijini Mbeya wamepandishwa kizimbani saa 11:30 jioni katika mahakama ya Mwanzo ya Mjini.

Wakisomewa mashtaka mahakamani hapo leo jioni mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Asha Njovu,washtakiwa  hao ambao ni waendesha bodaboda wanadaiwa kufanya vurugu kwa kupiga mawe magari ya polisi, kufunga barabara kwa mawe na magogo na kuchoma matairi.

Hakimu Njovu alisema kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria za kanuni ya adhabu kifungu namba 80 ambapo mshitakiwa Msumba Mdesa na wenzie 36 wanadaiwa wote kwa pamoja kutenda kosa hilo katika eneo la Iyela Jijini Mbeya majira ya saa nne na nusu.

Washitakiwa hao wote kwa pamoja walikana mashtaka yao na kurejeshwa rumande hadi April 14 baada ya kuzuiwa kupewa dhamana kwa kile alichoeleza mwendesha mashtaka wa polisi aliyejitambulisha mahakamani hapo kwa jina la PC Hamis kwamba washitakiwa hawapaswi kuwa nje kwa dhamana kwa kuwa kuna mashtaka mengine mawili bado hayajafunguliwa dhidi yao.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria nje ya mahakama hiyo walionekana kububujikwa na machozi huku wakielezea nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi iliyotumika kuwadhibiti waendesha bodaboda hao ambao baadhi yao walionekana wakichechemea kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walipigwa sana na polisi.

Awali leo asubuhi waendesha bodaboda hao waliandamana baada ya mwenzao mmoja aliyefahamika kwa jina la Siza Mwambenja kuuawa na mtu anayedaiwa kuwa alitumwa na mkewe kufanya mauaji hayo.

Ilielezwa kuwa marehemu aliachana na mkewe ambapo mke inadaiwa alimtumia watu wamdhuru mumewe kwa kile kilichoelezwa kuwa mwanaume huyo aliamua kuachana na mkewe na kuishi sehemu nyingine kutokana na madai kutoelewana katika ndoa yao kwa mmoja kati yao kukosa uaminifu ndani ya ndoa.

Baada ya tukio hilo la mauaji kutokea, inadaiwa kuwa mtuhumiwa ambaye ni mke wa marehemu alikamatwa na polisi ndipo waendesha bodaboda walielekea katika eneo hilo na kutaka kuchukua sheria mkononi kumnyang'anya mtuhumiwa aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi ili wamuadhibu.

Kitendo hicho kilisababisha kuibuka kwa tafrani baina ya Jeshi la Polisi na waendesha boda boda ambao walikuwa wakihitaji kumchukua mtuhumiwa ambapo walifuatilia gari la polisi hadi kituo cha Polisi na baadaye kufunga barabara kwa kuweka mawe, ndipo mabomu yalipoanza kurushwa na kuibuka kwa vurugu katika maeneo ya Mafiat, Oilcom, Magorofani na Iyela.

Akizungumza tukio hilo Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda Jiji la Mbeya Vicent Mwashoma alisema kuwa tukio hilo limewachanganya sana na kwamba yeye kama kiongozi alipata taarifa za kuibuka kwa vurugu wakati polisi wamekwisha anza kurusha mabomu.

Alisema kuwa hata hivyo Jeshi la Polisi lilipaswa kuwasiliana na uongozi wa waendesha bodaboda ili kufanya mazungumzo kabla ya kuchukua hatua hizo ambazo zimesababisha madhara kwa watu wengine ambao hawakuhusika katika tukio hilo.

Post a Comment