Ads (728x90)

 Na Ahmed Z.Msangi
Kwa miaka mingi sasa tangu taifa letu liingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kumekuwa na mabadiliko yaliyoletwa na taratibu na kanuni za uendeshaji wa mfumo huu wa vyama vingi vya kisiasa. Mfumo wa Vyama vingi katika nchi umekuwa ukitoa fursa ya kidemokrasia kwa kila mwananchi aliefikisha umri wa miaka 18 kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa serikali kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na mabadiliko haya katika nchi yetu, kwa sasa tumekuwa na vyama vingi vya siasa kama vile CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na vingine vingi. Vyama hivi vimekuwa vikitoa wagombea katika nafasi mbalimbali kama vile Wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani, wabunge na urais. Sanjali na hilo, vyama hivi vimekuwa na kipindi cha kufanya kampeni kwa lengo la kutoa ushawishi kwa Wananchi ili wawachague viongozi wa vyama vyao.
Kwa mwaka huu 2014 taifa lipo katika mchakato wa kufanya uchaguzi wa viongozi wa serikali katika ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa Tarehe 14.12.2014. Katika kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa mafanikio ikiwa na maana linafanyika kwa amani na utulivu, idara na taasisi mbalimbali ushirikiana kwa pamoja katika kusimamia na kuratibu shughuli mbalimbali za uchaguzi kuanzia uandikishwaji wapiga kura, kampeni, upigaji kura na hatimaye zoezi zima la utangazaji wa matokeo yenyewe.
Suala la msingi la kujiuliza, je ni nani mwenye wajibu wa kuhakikisha shughuli za uchaguzi zinafanyika kwa amani na utulivu bila kuwepo kwa vitendo vitakavyo pelekea uvunjifu wa amani? Ni wajibu wetu sote kwa nafasi tuliyonayo kutambua sheria, kanuni na taratibu za mchakato wa uchaguzi kwani vitendo vyovyote vya uvunjwaji wa sheria kabla na baada ya uchaguzi, ni uhalifu. Sheria haina udhuru, inachukua mkondo wake mara moja endapo tu ukiukwaji umefanyika.
Katika mchakato huu kuelekea uchaguzi mara kwa mara tumekuwa tukishuhudia vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu hasa katika Kampeni na siku ya uchaguzi. Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya watu kujiona wenye nguvu na kusababisha kuchochea vitendo visivyo vya kiungwana. Katika kipindi kama hiki tumeona idara, tume na taasisi zikifanya jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa vipeperushi, maandiko, vipindi maalum vya redio pamoja na mikutano.
Kwa kuelewa vizuri taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi ni hakika kila mmoja atashiriki zoezi la upigaji kura bila kuwepo vitendo vya uvunjifu wa amani. Miongoni mwa idara zilizopewa jukumu la kulinda amani na usalama wa raia ni Jeshi la Polisi. Polisi kama chombo cha umma, hakitumikii chama chochote cha siasa bali ni chombo kinachowajibika kutenda kwa haki na usawa bila upendeleo katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Polisi pamoja na wajibu wa kulinda amani na usalama wa raia wote, katika kipindi cha uchaguzi utekelezaji wa majukumu unaweka mkazo katika yafuatayo, kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika na kumalizika salama, kuhakikisha kwamba zoezi la upigaji kura linaenda sawa, bila vikwazo au bughudha, kuhakikisha kwamba vifaa vya kupigia kura viko salama yaani haviibiwi, havitekwi wala kughushiwa na watu wenye nia mbaya, kuhakikisha mchakato wa kupiga kura, kuhesabu na kutangazwa matokeo unakuwa huru na haki pamoja na kuhakikisha amani, usalama na utulivu vinadumu kabla na baada ya matokeo kutangazwa.
Ieleweke kuwa, kupiga kura ni haki ya msingi ya kila Mtanzania aliyetimiza umri unaokubalika Kisheria. Haki ya kupiga kura inaambatana na wajibu mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kujielimisha mambo ya sheria na taratibu zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi kwani kisingizio cha kutokujua sheria iliyovunjwa siyo sababu ya kutokamatwa na kushitakiwa. Hivyo kutii sheria na taratibu za uchaguzi ni wajibu.
Ni wajibu wetu sote kuendelea kuelimishana kwa kupeana elimu ya uchaguzi ili kuepuka makosa hama uhalifu kabla na baada ya uchaguzi. Wagombea, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Dini na waandishi wa habari kwa pamoja na kwa nafasi zao wanayo nafasi ya kuwaelimisha wananchi kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi ili kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Ulinzi na Usalama wetu siku zote unaanza na mimi, wewe na sisi sote” kwa ushirikiano, nguvu na nia ya pamoja ni hakika uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utafanyika kwa amani na utulivu, kila mmoja atimize wajibu wake kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za uchaguzi.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA  KAMISHNA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z.MSANGI



Post a Comment