Ads (728x90)Mashabiki wa Mbeya City wakiingia kwa mbwembwe
 


 
LIGI kuu ya Vodacom imeendelea katika dimba la Sokoine Jijini Mbeya kwa kuwakutanisha mahasimu wawili  wenyeji wa Mbeya timu ya Jeshi la Magereza Prison na Mbeya City na kutoka sare ya bao 2-2.
Prison iliyokuwa katika hali mbaya kwenye msimamo wa ligi ambayo kabla ya mchezo huo ilikuwa na jumla ya pointi 9 huku wenzao Mbeya City wakiwa na pointi 11 ndiyo ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Mbeya City katioka dakika ya 5.
Goli hilo la Prison lililofungwa na Boniface Hau liliwachanganya wachezaji wa Mbeya City na kucheza bila kuelewana katika dakika hizo za mwanzo za mchezo.
Hau aliyevalia jezi nambari 3 mgongoni aliambaa ambaa na mpira upande wa kulia na kuwatoka walinzi wa Mbeya City Paul Nonga na Boniface Fred na hatimaye kupiga shuti lililomwacha golikipa wa Mbeya City David Burhan akichupa bilaa mafanikio.
Goli hilo la Prison liliamsha hisia mpya kwa mashabiki wa Prison huku wenzao wa Mbeya City ambao waliingia uwanjani kwa mbwembwe wakibaki kimya wakiwa wamelowa mithili ya waliomwagiwa na maji.
Kwa kipindi chote cha mchezo dakika za mwanzo Prison walionekana wakisakata kambumbu safi wakitoa mashambulizi kwa zamu ilhali wachezaji wa Mbeya City wakijaribu kuchomoa mashuti yaliyokuwa yakielekezwa golini kwao.
Mbeya City walikuwa wakipeleka mashambulizi machache katika lango la Prison lakini ambapo katika dakika ya 42 Paul Nonga wa Mbeya City aliipatia timu yake bao la kusawazisha baada ya wachezaji wa Prison kuzubaa na kutitumia fursa hiyo kufunga bao ambalo golikipa wa Prison Mohamed Yusuf aliudaka kisha akautema.
Bao hilo liliamsha nderemo na vifijo kwa mashabiki wa Mbeya City huku wenzao wa Prison wakitaharuki wasiamini kuingia kwa bao hilo.
Hadi mapumziko timu zote zilitoka uwanjani kwa kufungana bao 1-1.
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza kwa kasi hukun wachezaji wa Mbeya City wakionyesha uchu wa kupata bao la kuongeza ambapo katika dakika ya 48 ya mchezo mchezaji aliyevalia jezi nambari 7 mgongoni Themi Felix aliwainua tena mashabiki wa Mbeya City kwa kufunga bao baada ya wachezaji wa Prison kujisahau kwenye safu ya ulinzi.
Felix alifunga bao hilo huku akisindikizwa na walinzi wa Prison ambapo alipiga shuti la mbali lililotinga wavuni upande wa kushoto ambapo golikipa Mohamed Yusuf alichupa bila mafanikio.
Baada ya kuingia kwa goli hilo wachezaji wa Mbeya City walionekana wakiwa wamepata ari mpya ingawa dakika kadhaa zilikuwa zikipotezwa bure na golikipa wa Mbeya City David Burhani aliyekuwa akiudaka mpira na kulala chini muda mrefu.
Kunako dakika ya 55 ya mchezo Meshack Seleman nusura alipatia timu yake bao la kusawazisha baada ya kubaki yeye na golikipa David Burhani lakini alipiga mpira uliotoka juu ya goli.
Wakati Mbeya City wakiwa na matumaini ya ushindi wa mchezo huo kutokana na kupoteza muda, wenzao wa Prison waliongeza spidi ili kujipatia bao la kusawazisha ambapo zikiwa zimesalia dakika 3 mpira kumalizika mchezaji wa Prison Nurdin Chona aliipatia bao safi timu yake.
Goli hilo liliingia baada ya kumhadaa golikipa na walinzi wa Mbeya City na kuupiga mpira uliopenya katikati ya mikono na kichwa cha golikipa na kutinga wavuni.
Hata hivyo kabla ya kupuliza kipyenga cha kuumaliza mpira mwamuzi wa mchezo huo Simon Mbelwa(PWANI) alimzawadia kadi nyekundu mchezaji wa Prison Hamis Maingo baada ya kupigana na mchezaji wa timu ya Mbeya City Juma Nyoso hali ambayo ilizusha tafrani miongoni mwa wachezaji wa Prison wakidai kuwa kadi hiyo imetolewa kwa uonevu.
Hadi mpira unaishi timu zote zimetoka nguvu sawa kwa bao 2-2


Post a Comment