Makazi ya Mfanyabiashara Elfansi Sanga eneo la Airport Iyela Jijini Mbeya yanayowatioa udenda askari polisi na kumtapeli mamilioni ya fedha |
Mfanyabiashara wa Mwanjelwa Elfansi Sanga anayedaiwa kutapeliwa na watu wanaojiita askari polisi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi |
Mfanyabiashara Elfansi Sanga akiwa katika shughuli zake za utengenezaji wa mifuko |
Rola la karatasi linalotumika kutengeneza mifuko midogo ya kuhifadhia karanga na korosho |
Karatasi zinazotumika kutengeneza mifuko |
Vijana wakiwa kazini kutengeneza mifuko ya kuhifadhia karanga na korosho |
Leseni za biashara na vibali vya kuendesha biashara hiyo |
Watoto wanaodaiwa kufungiwa ndani kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 9 alasiri na watu wanaodaiwa kuwa ni askari |
Sehemu ya nyumba ya Mfanyabiashara huyo iliyopo Mtaa wa Airport Iyela Jijini Mbeya |
Mazingira ya makazi ya Mfanyabiashara Elifansi Sanga(41) yamewashawishi watu wanaojiita ni askari polisi na maofisa Usalama wa Taifa kufika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo mara kwa mara na kumtapeli fedha kwa gia ya kumtuhumu kuwa anajihusisha na ujambazi.
Mfanyabiashara huyo ambaye amekuwa akiuza mifuko ya rambo kwa zaidi ya miaka 20 na kumudu kujenga nyumba kubwa ya kifahari kumewalazimisha baadhi ya watu kuvaa uhusika wa uaskari polisi na kufika dukani kwake na kumtishia kuwa anajihuisisha na ujambazi kwa nia ya kumlazimisha atoe fedha.
Utapeli huo unaelezwa kufanywa kati ya Februari mwaka jana na Januari mwaka huu ambapo kwa nyakati tofauti watu waliojiita askari polisi, maofisa Usalama, maofisa wa TRA na TBS wamekuwa wakifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo na kumtishia na hatimaye kuchukua fedha.
Imedaiwa kuwa Februari mwaka jana watu watatu walifika dukani kwa mfanyabiashara huyo maeneo ya Mwanjelwa kisha walimtaka wafanye ukaguzi juu ya biashara zake na kiwanda ambacho amekuwa akitumia kufunga vifungashio kwa ajili ya matumizi ya kuhifadhia karanga na korosho kisha kumueleza kuwa shughuli aliyokuwa akiifanya haina baraka za TRA na TBS hivyo anatakiwa kulipia.
Hata hivyo inaelezwa kuwa baada ya kumueleza hivyo walimtaka atoe sh.600,000 ili wamfanyie utaratibu wa kulipia uendeshaji wa shughuli hizo na baadaye jamaa hao waliondoka bila kuleta mrejesho wa malipo aliyoyatoa mfanyabiashara huyo.
Akizungumzia tukio hilo Mfanyabiashara huyo Sanga alisema kuwa jamaa walichukua kiasi cha sh.600,000 kwa ahadi kuwa wanaenda kumshughulikia namna ya kupata vibali vya kuendesha shughuli hizo lakini hata hivyo hawakurejea tena ndipo mwezi Juni walikuja watu wengine ambao nao walijifanya kuwa ni maofisa wakaguzi wa viwanda ambao walimtishia mkewe na kumlazimisha kutoa kiasi cha sh. milioni 2 na kisha kutokomea.
Alisema kuwa matukio hayo mawili aliyaona ni kama utapeli uliofanywa dhidi yake hivyo akaamua kufuatilia Mamlaka ya Mapato(TRA) ili aone kama kuna mahala anakosea katika uendeshaji wa shughuli zake ambapo alielezwa kuwa kiwango cha shughuli zake bado hazijafikia kulipia Mapato na kwamba hata hivyo aliwataka wamkadirie mapato kutokana na baadhi ya watu kufika kwake wakimtishia kuwa anakiuka taratibu za Mapato.
Sanga alisema kuwa TRA walimkadiria mapato kulingana na shughuli anazofanya na kukata leseni ya biashara ambapo pia alienda kwenye chama cha Wafanyabiashara na Wakulima TCCIA ambako walisaidia kujisajili na chama hicho na kukata vibali vya uendeshaji wa shughuli zake.
Alisema kuwa baada ya kukamilisha taratibu hizo akawa anaendelea na shughuli zake kama kawaida akijua kuwa hakuna tatizo jingine linaloweza kumtokea ndipo Januari Mosi mwaka huu walifika watu wengine wanne ambao walijiita kuwa ni Askari Polisi, Maofisa Usalama na watu wa TRA ambao walimfuata kijana wake aitwaye Norasko Mtega anayeuza dukani na kumfunga pingu wakimtaka amuoneshe tajiri yake yeye(Sanga) kwa kuwa ni jambazi anayemiliki silaha.
Akizungumzia tukio hilo Norasko alisema kuwa siku hiyo alifuatwa na watu wanne dukani wakamtaka awaelekeze alipo Sanga ndipo walipofika nyumbani huku akiwa amefungwa pingu na baadaye wakampigioa simu tajiri yake ambaye alifika nyumbani kisha wakamfungua pingu na kumfunga yeye.
''Walinichukua dukani, wakanitaka niwaelekeze nyumbani, tulifika nyumbani nikawapa namba ya Baba wakampigia akafika, wakanifungua pingu wakamfunga Baba, mmoja akaniambia niende ndani nikalale, wakati huo ilikuwa majira ya saa tatu asubuhi,''alisema Norasko.
Aliendelea kusema kuwa waliwafungia ndani watu wote waliouwepo pale kuanzia saa 3:00asubuhi hadi saa 9:00 mchana.
''Tulikaa ndani huku wao wakiwa nje hatukujua kinachoendelea huko, tulifunguliwa saa tisa mchana, wakaondoka,''alisema.
Kwa upande wake Sanga alisema kuwa mara baada ya kumfunga pingu alilazimishwa kupiga magoti na kulala chini wakimlazimisha kutoa fedha na kwamba iwapo ataleta ubishi wowote wanaweza kumdhuru na kwamba alijitahidi kuwaeleza kuwa hakuna na fedha walianza kupekua ndani na kumuita mkewe ili wasaidie kupekua vyumbani ndipo alipokuta fedha katika kabati moja wakachukua na kuondoka nazo.
''Walipekua ndani katika kabati la nguo nilikuwa na fedha kiasi cha Sh. Milioni 5 ambazo nilipanga kwenda kufunga mzigo Dar es salaam, wakazichukua, wakanifungua pingu na kuondoka nazo,''alisema Sanga.
Naye mke wa Sanga aliyejitambulisha kwa jina la Mona Sanga akisimulia tukio hilo alisema kuwa, siku hiyo ambayo ilikuwa ni ya Mwaka mpya alijihimu kuelekea kanisani aliporudi alikuta watoto wamefungiwa chumbani alipouliza kuna nini kimetokea akaaambiwa kuwa baba yao amefungwa pingu amelazwa chini na askari, ndipo na yeye akaingia ndani kujifungia kwa hofu.
Alisema kuwa baadaye waliingia watu chumbani kwake na kupekua makabati na kuchukua hela kiasi cha Sh. Milioni 5 ambazo mumewe alitakiwa kwenda kufungia mzigo Dar es salaam.
Kwa upande wake mtoto wa Sanga aliyejitambulisha kwa jina la Neema(9) anayesoma darasa la 5 katika shule ya Msingi Airport alisema kuwa siku hiyo alikuja watu wanne, wakawaambia wajifungie chumbani wasitoke nje na kwamba walishinda na njaa bila kula chochote siku hiyo.
''Walikuja wababa wanne wakatuambia tukajifungie chumbani tusitoke nje, tulikaa ndani, njaa ilituuma hadi saa tisa ndio tukatoka nje,''alisema mtoto Neema.
Aidha mara baada ya tukio hilo Sanga alisema alijaribu kuwafahamisha jamaa mbalimbali juu ya matukio ya utapeli yanayotokea ndipo alipoambiwa na Makamu Mwenyekiti wa TCCIA Said Mohamed ambaye pia ni Mwenyekiti wa Haki za Binadamu mkoa wa Mbeya kuwa iwapo kuna siku watafika tena watu wa aina hiyo ampigie simu na kumjulisha.
Alisema kuwa Mei 10 walifika tena jamaa wa aina hiyo wakiwa ndani ya gari la serikali STK 8264 ndani ya gari hiyo walikuwemo watu wanne akiwemo askari polisi aliyevaa sare za polisi FFU na kwamba mara baada ya kufika shemeji yake alimpigia simu Ofisa Mtendaji wa Mtaa na Mwenyekiti wa Haki za Binadamu ambao walifika nyumbani wakati jamaa hao wakiwa ndani.
Alisema kuwa mara baada ya kufika Ofisa Mtendaji na Mwenyekiti wa Haki za Binadamu jamaa hao waliaga na kuondoka kisha wakamwita nje na kumuonya kwa kumtishia kwa nini amewaita watu hao.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa amepata taarifa hizo ambapo aliwaita askari walioenda eneo hilo ambao walijieleza kuwa walifika hapo baada ya kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo vyao kuwa Mfanyabiashara huyo anajihusisha na ujambazi na kuwa baada ya kubaini kuwa hakukuwa na ukweli juu ya tuhuma hizo waliondoka zao.
''Ndio ni kweli askari walifika eneo hilo, wamenieleza kuwa baada ya kufanya upelelezi wao walibaini hakuna ukweli wowote juu ya tuhuma hizo, waliondoka na walisema hawakuchukua kitu chochote eneo hilo,alisema Kamanda Msangi.
Post a Comment