Simon Shonde, Diwani wa Iyula akionesha hisia zake za kutaka kuwawajibisha watendaji wanaokiuka taratibu za kiutumishi. |
Diwani wa Halungu Samson Simkoko akielezea utaratibu aliouita mbovu wa serikali wa kuwalinda watumishi wanaoshindwa kuwajibika kwenye Halmashari. |
Diwani wa Kata ya Ihanda Joel Kasebele akichangia hoja ya kutokuwa na imani kwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo. |
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi |
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Allan Mgullah akisisitiza kutokuwa na imani na Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo |
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi limesimamia
nia yake ya kumtaka Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Zabron Lulandala kuachia
nafasi yake kutokana na kile walichodai kuwa ameshindwa kuwawajibisha watendaji
walioshindwa kuwatumikia wananchi.
Kauli hiyo ya Baraza la Madiwani iliibuka katika kikao cha
Baraza hilo baada ya Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Ezekiah Kilemile kuwataka madiwani kuangalia aina ya adhabu wanazopaswa kutoa kwa
kile alichodai kuwa adhabu zingine zinaweza kuigharimu Halmashauri iwapo
watumishi wataamua kuchukua hatua za kisheria.
Kilemile alisema kuwa kitendo cha kutoa adhabu au kumhamisha
mtumishi kunapaswa kuzingatia taratibu za kisheria na kwamba hali hiyo
itasababisha watumishi wafanye kazi kwa woga kutokana na maazimio ya Madiwani
ambayo yanahatarisha ajira zao.
Mara baada ya kauli hiyo ambayo ilionesha kama vile imewasha
moto Madiwani hao walisimama kwa pamoja wakitaka kutoa hoja ya kupinga kauli
hiyo ya Mwakilishi wa Katibu Tawala wakidai kuwa hana nia njema na Halmashauri hiyo.
‘’…Mfumo wa TAMISEMI unawakinga wanaokosea, watendaji
wanaoharibu katika maeneo yetu wanatetewa na Mkoa, sisi ndio tunaojua utendaji
wao, mfumo wa TAMISEMI ni mbovu tumechoka kuendeshwa kwa mfumo huu, tuachieni
wenyewe tuchukue hatua sio kubembelezana,’’alisema Samson Simkoko Diwani wa
kata ya Halungu.
Naye Diwani wa Kata ya Ihanda Joel Kasebele alidai kuwa
Ofisi ya Mkoa imekuwa ni chanzo cha matatizo kwa watumishi kwa kuwa wanapowajibishwa
baada ya kushinda kuwajibika ofisi hiyo imekuwa ikisimamia kuwatetea na kwamba
maazimio yanayotolewa katika vikao vya Baraza la Halmashauri yanavunjwa na
watendaji wa Mkoa.
Alisema kuwa iwapo Ofisi ya Katibu Tawala inaona Ofisa
Utumishi huyo bado anafaa ni bora ahamishiwe kituo kingine cha kazi kwa kuwa
baada ya kuazimiwa na Madiwani utendaji wake umezidi kudorora na kuwa amekuwa
hatoi ushirikiano wowote kwa Madiwani.
‘’Tunaomba huyu mtu uondoke naye, hapa pamekuwa si mahala
salama kwa utendaji wake, hata ukimwacha hawezi tena kuwatumikia wananchi kwa
ufanisi,’’alisema Julius Simbeye Diwani wa Kata ya Nyimbili.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Allan
Mgullah alisema kuwa ni vyema Ofisa Utumishi huyo angeondoka na kwamba mbali na
kukosa imani naye katika utendaji amekuwa akitoa majibu mabaya kwa madiwani na
hivyo kuendelea kukosa imani naye katika kuitumikia Halmashauri hiyo.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elick Ambakisye
alielezea baadhi ya mapungufu ya Ofisa Utumishi huyo ambayo yalibainika katika
kikao kilichopita ni pamoja na kutowasimamia baadhi ya watendaji wa vijiji na
kata ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakifanya ubadhirifu na kutumia
vibaya fedha zinazokusanywa katika maeneo hayo.
Alisema miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kutosoma
mapato na matumizi ya vijiji, kutumia stakabadhi za kughushi, kutumia vibaya
ruzuku ya mbolea iliyogawanywa na serikali kwa wakulima na kuwahamisha
watendaji walioharibu kijiji kimoja na kuwapeleka katika vijiji vingine hali
ambayo inamuondolea sifa ya uwajibikaji ndani ya Halmashauri hiyo.
Post a Comment