Ads (728x90)

VIONGOZI waandamizi wa Chama Cha Demokrasia na Mendeleo CHADEMA pamoja na wanachama 15 wa chama hicho wanatarajia kujiunga na Chama Cha NCCR Mageuzi kesho katika ukumbi wa Hotel ya Double J jijini Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho zilizotumwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kwa wanahabari imedaiwa kuwa viongozi hao wa CHADEMA watakutana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi na mshauri wa mambo ya kisiasa Danda Juju ambaye atamwakilisha, mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho James Mbatia.
Juju ambaye tayari amewasili mkoani Mbeya kwa shughuli hiyo maalum anatarajia kuwapokea viongozi hao wa CHADEMA ikiwa ni hatua za awali zinazodaiwa kukisambaratisha CHADEMA.
Hivi karibuni aliyewahi kuwa Katibu wa Mkoa wa CHADEMA Eddo Makata alitangaza kujiunga na NCCR-Mageuzi baada ya kujiuzulu kutoka CHADEMA ambapo hata hivyo viongozi wa CHADEMA walidai kuwa walimtimua uongozi na uanachama.
Wimbi la mpasuko ndani ya CHADEMA limeanza kuibuka baada ya madai ya kutimuliwa kwa viongozi na wanachama wa chama hicho akiwemo, Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana la Chadema Taifa (BAVICHA)Juliana Shonza na aliyewahi kugombea Ubunge jimbo la Mbozi Mashariki Mtera Mwampamba. 


Post a Comment