Ads (728x90)
KIONGOZI dini ya Kiislamu kutoka msikiti mtakatifu wa Mecca nchini Saudia Shekhe Mohamad Al-Hazmi amevunja ukimya na kueleza kuwa waislamu wanaojiua au kuua nafsi za wengine kinyume na haki wanafanya dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Shekhe Al-Hazmi ambaye anafanya ziara katika mikoa ya Dar es salaam,Mbeya, Iringa, Arusha na Kilimanjaro alifafanua kuwa ni haramu kwa waislamu kujitoa mhanga kwa kujiua kwa madai ya kuipigania dini ya Kiislamu.

Akiwa ameambatana katika ziara hiyo na Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Dhiynureyn Fondation Shekhe Said Bin Abri,na kutembelea katika msikiti wa Baraa Bin Azb Isanga jijini Mbeya Shekhe Al-Hazmi alisema hakuna sheria katika uislamu inayoruhusu mtu kujiua.

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na waumini wa msikiti huo baada ya swala ya tarawehe ambao walitaka kujua iwapo baadhi ya watu wenye itikadi ya dini  ya Kiislamu huamua kujiua kwa kujitoa mhanga kwa madai kuwa wanachokifanya ni kuinusuru dini.

Shekhe Al-Hazmi alisema kuwa upo mgongano miongoni mwa mashekhe wakubwa juu ya suala hilo na kwamba hata hivyo ni haramu kwa muislamu yoyote kujiua au kuua nafsi nyingine na kwamba kitendo hicho sio katika maagizo ya dini ya kiislamu.
Alisema kuwa katika zama za Mtume Mussa suala la kujiua lilikuwa ni sehemu ya kafara ya madhambi lakini katika zama hizi ni haramu mtu yoyote kujiua na kwamba kwa kufanya hivyo anakuwa amemkosea Mwenyezi Mungu.
Shekhe Al Hazmi ambaye alikuwa akizungumza kwa lugha ya kiarabu kupitia mkalimani Shekhe Ibrahimu Bombo aliongeza kuwa yapo mazingira katika zama hizi ambapo kuna baadhi ya watu wanaamua kujitoa mhanga na kwamba suala hilo ni gumu kulielezea kwa kuwa lina hitilafu kwa mashekhe wakubwa wa kiislamu duniani.

 ‘’Mazingira ya jambo hili ni mazito yanahitaji ufafanuzi wa mashekhe, uislamu umezungukwa na mambo mengi kwa sasa,’’alisema Shekhe Al-Hazmi ambaye ni miongoni mwa maimamu kutoka katika msikiti mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia.
Post a Comment

  1. Hii itasaidia dhana mbaya inayopewa dini ya kiislam

    ReplyDelete