Ads (728x90)


MWALIMU WA SHULE YA MSINGI YA UHURU ILIYOPO TUNDUMA WILAYA YA MOMBA MKOANI MBEYA ADELA MTWEVE AKIONESHA NAMNA AMBAVYO WANAFUNZI WA DARASA LA PILI KATIKA SHULE YA MSINGI UHURU WANAVYOKETI WANAPOKUWA DARASANI

MWANDISHI WA HABARI WA STAR TV AMINA SAIDI AKIJARIBU KUKETI KATIKA TOFARI KUJARIBU KUANDIKA KAMA AMBAVYO WANAFUNZI WA DARASA LA PILI WA SHULE YA MSINGI UHURU WANAVYOANDIKA


KILIO CHA SHULE HIYO KIMEANZA KUSIKILIZWA NA WADAU ZIKIWEMO TAASISI MBALIMBALI ZA KIFEDDHA AMBAPO BENKI YA POSTA TANZANIA ILIJITOLEA MIFUKO 100 KWA AJILI YA KUSAIDIA UJENZI WA SHULE HIYO.








Na, Rashid Mkwinda, Tunduma
WANAFUNZI 129  wanaosoma katika  shule ya msingi ya Uhuru iliyopo Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya wamelazimika kuketi sakafuni kutokana na shule hiyo kuwa na madawati matano yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi 20 kati ya wanafunzi 149 wa shule hiyo.
Shule hiyo yenye jumla ya madarasa matatu na walimu watatu ambayo ilianzishwa kutokana na msongamano wa wanafun zi katika shule za msingi za Mkombozi,Umoja, Migombani na Sogea ambazo zilifurika wanafunzi kiasi cha kuwa na uwiano wa mkondo mmoja wanafunzi 100.
Waandishi wa habari walitembelea shule hiyo mwishoni mwa wiki na kukuta vyumba vitatu ambavyo ndani yake kumepangwa matofari ambayo kwa mujibu wa mwalimu wa darasa la pili Bi. Adela Mtweve ni kwamba matofari hayo yanatumiwa na wanafunzi kama madawati.
Bi. Mtweve alisema kuwa darasa moja lenye wanafunzi 50 lina madawati matatu ambapo wanafunzi wanaobaki wanakalia matofari na kusababisha kushindwa kuandika vizuri.
‘’Hapa ndipo wanapoketi wanafunzi na kuandika,anaweka daftari lake juu ya tofari na yeye anakalia tofari jingine,’’alisema Mwalimu Mtweve huku akionesha namna ambavyo wanafunzi hao wanaketi.
Akizungumzia tatizo hilo Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Juni Mwandambo alisema kuwa shule hiyo ina upungufu wa madawati, walimu na nyumba za walimu hali ambayo inasababisha kudorora kwa taaluma.
Alisema kuwa baadhi ya wazazi wanaotembelea shuleni hapo hulazimika kuwahamisha watoto wao na kuwapeleka katika shule nyingine na kwamba wakati shule hiyo inaanzishwa ilikuwa na jumla ya wanafunzi  175 ambapo kwa sasa wamebaki wanafunzi 149.
‘’Takribani wanafunzi 30 wamehamishwa na wazazi wao baada ya kuona mazingira yaliyopo, wanafunzi wanaketi kwenye vumbi, ni hatari kwa afya ya wanafunzi,’’alisema Mwalimu Mwandambo.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo mapya ambako shule hiyo ipo Bw.Lugano Mwakiboge alisema kuwa, baada ya kuona kuna msingamano wa wanafunzi katika shule zilizopo katikati ya mji wa Tunduma wananchi walihamasishwa kujenga shule hiyo.
Alisema kuwa wazazi walichangia ujenzi na halmashauri ya mji wa Tunduma ilichangia mabati ambapo kwa sasa wanatafuta ufadhili kutoka taasisi mbalimbali ili kusaidia ujenzi wa shule hiyo.
Bw.Mwakiboge alisema kuwa Benki ya Posta Tawi la Tunduma ilitoa jumla ya mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya zaidi y ash. milioni 1.7 ambayo itasaidia kusakafia madarasa ya shule hiyo ambapo kwa sasa wanafunzi wanaketi kwenye vumbi.
Akizungumzia msaada huo wa saruji kwa shule ya msingi Uhuru, Mhasibu wa Benki hiyo Bw. Felix Mapunda ambaye alikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa benki ya Posta nchini Bw.Sabasaba Moshingi alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya huduma za kibenki.
Alisema kuwa faida itokanayo na huduma za kibenki za inarejeshwa kwenye maendeleo ya wananchi ikiwemo ambazo ni huduma za kijamii kama vile, elimu, afya na maji.



Post a Comment