Ads (728x90)

Sheikh Ponda Issa Ponda

Waumini wa dini ya Kiislamu wakifurahia kuachiwa kwa Sheikh Ponda hii ilikuwa mwaka 2014(Picha Maktaba)

Na Bloga Wetu, Morogoro.
MACHOZI ya furaha na sauti za kumtukuza Mwenyezi Mungu za Takbir!!! Allahu Akbar!! Zilihanikiza viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro baada ya mahakama hiyo kumwachia huru Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kuachiwa huru kwa Sheikh Ponda aliyekaa mahabusu takribani miaka miwili kumefuatia upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ambayo yalifunguliwa dhidi yake.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Mary Moyo alitoa uamuzi huo huku Sheikh Ponda akitokea rumande alikokuwa amekaa kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na dhamana yake kuzuiwa na mkurugenzi wa mashtaka DPP kwa kile kilichoelezwa kuwa maslahi ya Taifa.
Mara baada ya kuachiwa huru Sheikh Ponda aliishukuru Mahakama kwa kutenda haki ingawa pia aliilaumu kwa kuchelewa kutenda haki hiyo mapema kutokana na dhamana yake kuzuiwa.
Sheikh Ponda alikuwa akikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kudaiwa kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini ikiwa ni pamoja na kutoa ushawishi wa watu kutenda kosa, makosa ambayo alidaiwa kuyatenda Agosti 10, 2013 kwenye viwanja vya shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.

Kwa upande wa mashtaka kesi hiyo iliwakilishwa na wakili wa serikali Mwandamizi Bernard Kongola,George Mbalassa na Sunday Hyera ambapo upande wa utetezi uliwakilishwa na wakili Juma Nassoro,Bathoromeo Tarimo na Abubakar Salim.






Post a Comment