Ads (728x90)





-->
Hatimaye Dereva Aden Mwampyate(55) aliyenusurika kifo Januari 19 baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongwa na lori na yeye kubanwa katika msukano huku akiwa amejeruhiwa vibaya amesema kuwa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumnsuru na kifo.
Bw. ambaye amelazwa katika hospitali teule ya Ifisi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya anasema kuwa hakutarajia kupona kutokana na mazingira ya ajali yalivyokuwa na kuwa kutokana na eneo alilopatia ajali anawashukuru wasamaria waliojitokeza kuokoa maisha yake.
‘’Sikujitambua kabisa nilikuwa nasikia sauti kwa mbali hakuna niliyeweza kumtambua siku hiyo nawashukuru sana ndugu zangu,’’alisema Bw. Mwampyate.
Aidha Mwampyate anasema kuwa taarifa zaq tukio la ajali yake zilikuwa zinafuatiliwa na ndugu yake aliyoko nchini Marekani aliyemtambulisha kwa jina la Ambakisye Mwakyusa ambaye alifuatilia blogi hii na kuwajulisha ndugu na jamaa wa hapa nchini.
‘’Ambakisye aliangalia moja kwa moja kupitia mtandao hatua kwa hatua tangu nimepata ajali hadi nafikishwa hospitali, akaanza kuwajulisha ndugu na jamaa nakushukuru sana ndugu yangu umenisaidia kuwajulisha ndugu zangu kupitia mtandao wako, Mungu akubariki sana,’’anasema Mwampyate akimshukuru mwandishi wa blogu hii.
Naye mke wa Mwampyate aliyejitambulisha kwa jina la Jenifer anasema kuwa alipata taarifa kupitia simu ya mkononi ya  mwandishi wa blogu hii ambapo mara baada ya kupata ajali alichukua simu ya majeruhi na kutafuta namba za ndugu zake na kupiga ili kuwajulisha ajali hiyo.
‘’Nakushukuru sana kaka yangu Mungu akubariki hatuna cha kukulipa Mungu mwenyewe ndiye anajua umetusaidia sana,’’alisema Jenifer huku akilengwa machozi ya matumaini.
Kwa upande wake Muuguzi mkuu wa hospitali ya Ifisi Bi. Roda Kisongwa anasema kuwa majeruhi huyo alivunjika mguu wa kulia ambapo walimuwekea mawe mazito baada ya kumfanyia upasuaji na kumuweka vyuma pia walimshona nyuzi 18 katika majeraha ya kichwani ambayo kwa sasa yameanza kupona.
‘’Tunawashukuru sana kwani mlifika kwenye eneo la tukio kwa wakati muafaka hakuna alichopoteza pamoja na fedha zake zilikuwa salama kabisa..Mungu awabariki sana vijana,’’alisema Muuguzi huyo.
Bw. Mwampyate alipata ajali baada ya gari lake kugongwa na Lori lililokuwa likielekea Mbeya na yeye akielekea mjini Tunduma katika eneo la Senjele ambapo mara baada ya kugongana uso kwa uso lori hilo lilipinduka barabarani na gari lake lilitumbukia korongoni huku akiwa amebanwa na katika msukano.
Wasamaria wema ambao walikuwa ni abiria katika Coaster lililokuwa likielekea Mbeya walishuka katika gari hilo na kutoa msaada kwa kumnasua katika gari na kumkimbiza katika hospitali ya Ifisi.
(Blogu hii inawashukuru jamaa wote waliochangia kwa namna moja ama nyingine kuokoa maisha ya dereva huyu ikiwa ni pamoja madaktari na wauguzi wa hospitali teule ya Ifisi)
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Ifisi Roda Kisongwa na mke wa Aden Jenifer wakimfariji mgonjwa katika wodi ya hospitali teule ya Ifisi

Dereva Aden akionesha mguu uliovunjika mara tatu katika ajali iliyotokea eneo la Senjele Januari 19 wakati akisafirisha gari kuelekea Tunduma
Siku aliyopata ajali wauguzi na wasamaria wema walimsaidia kumuwahisha hospitali na kupata tiba
Wasamaria wema walipokuwa wakimnasua siku alipopata ajali









Post a Comment