Ads (728x90)

Nyoka amtoa baru mbunge

Nyoka amtoa baru mbunge


NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, alitimua mbio kunusuru maisha yake na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Mwanri alikuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kuendesha harambee ya kujenga Kanisa la Kilingi, akiwa na mkewe meza kuu, aliwashangaza waumini alipokimbia akiwa amenyanyua mikono juu huku akitamka maneno ya “shindwa kwa Jina la Yesu wewe shetani, shetani shindwa kwa Jina la Yesu,” na wageni wengine waalikwa wakianguka chini wakijiokoa. Hali hiyo ilitokea baada ya nyoka kutoka kusikojulikana kuingia kanisani huku Naibu Waziri akijiandaa kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa. Waumini walikimbizana na kiumbe huyo kwa mawe na viti bila kujali kama walikuwa ibadani, huku Askofu na wachungaji wengine wakiendelea kusali na waumini kutakiwa kurejesha utulivu katika ibada.
Tukio hilo lilitokea katika ibada ya saa nne iliyokuwa ikiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, ambayo pia ilikuwa ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.


Hata hivyo, jitihada za waumini za kumkimbiza nyoka huyo kutaka kumwua hazikufanikiwa, baada ya kutoweka asionekane tena, jambo lililoacha simulizi la ni kwa jinsi gani alifika mahali hapo.

“Inashangaza sana kwani lazima ujiulize alifikafikaje hapo mbele, wakati nyuma yangu kulikuwa na watu wengi...alikuwa na hasira sana, kwani alikuwa tayari kung'ata, kwa kweli hadi sasa mimi sielewi ni mambo gani haya,” alisema Mwanri. Hata hivyo hakuna madhara makubwa yaliyotokea mbali na mhamaniko uliowapata waumini hao. Nyoka huyo hakuweza kutambuliwa aina yake kutokana na mtafaruku huo.

Post a Comment