Ads (728x90)

Mkurugenzi Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Ananilea Nkya

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Blandina Nyoni

Daktari Mkuu wa Serikali Dkt. Deogratias Mtasiwa

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Hadji Mponda

 Dar es salaam.

SAKATA la mgomo wa madaktari limezidi kuchukua sura mpya baada ya wanaharakati kutoka asasi 12 zisizo za kiserikali kufunga barabara katika Jiji la Dar es Salaam wakishinikiza Serikali imalize mgomo huo haraka ili kuokoa mamia ya Watanzania kuendelea kupoteza maisha.

Tukio hilo lilitokea jana jijini baada ya wanaharakati zaidi ya 60 kuzuia magari katikamakutano ya barabara za Ally Hassan Mwinyi na Ocean Road karibu na daraja la Salender.

Wanaharakati walifunga barabara katika eneo hilo kuanzia saa 8 mchana ambapo shinikizo hilo lilidumu kwa muda wa saa 1 na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara hizo.

Walikuwa na mabango yenye ujumbe tofauti huku wakidai lengo lao ni kuishinikiza Serikali kumaliza mgomo huo kwa kukaa meza moja na madaktari ili kuokoa roho za Watanzania zinazopotea bila kuwa na hatia.

Baadhi ya mabango waliokuwa wamebeba wanaharakati yalionesha kusikitishwa jinsi Serikali inavyoshughulikia suala hilo na kuwataka viongozi wote wakuu wanaongoza Wizara ya Afya wawajibishwe kwa kufukuzwa kazi.

Akizungumza katika eneo la tukio kwa niaba ya wanaharakati hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA), Ananilea Nkya, alisema  wameamua kufanya hivyo ili kufikisha ujumbe kwa Serikali.

Nkya alisema haiwezekani Serikali kukaa kimya wakati wananchi wanakufa na kuongeza mgomo huo ni janga linahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa haraka ili  madaktari warejee kazini.

Mkurugenzi alisema  wanaharakati hao baada ya kuona hatua ambazo zinafanyika katika kushughulikia mgomo huo waliamua kuwasiliana kwa kutumia njia ya simu hadi wakafika na kufunga barabara ili ujumbe wao ufike.

Alisema hatua waliyofanya haikuwa ya kufanya vurugu ndiyo maana Polisi walipofika eneo hilo hawakuwafanya lolote zaidi ya kukaa pembeni.

Nkya alisisitiza kukerwa na namna mgomo huo unavyoshughulikiwa na Serikali na kubainisha kama hakutakuwa na mazungumzo ya kumaliza tatizo hilo watakwenda Ikulu kwa nia njema hadi upatiwe ufumbuzi.
" Hatufanyi vurugu ya aina yoyote hapa tulipo, tumeamua kufunga barabara kwa saa moja na baada ya hapo tutaondoka kwani ujumbe wetu utakuwa umefika kwa Serikali.
Wanaharakati tunataka kuona suala hili linapatiweufumbuzi na kumalizika haraka.

" Tunamshangaa Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye yeye ni mwanamke na anatambua matatizo ya wanawake lakini anaona suala la kufa kwa Mtanzania si jambo la dharura.|Amekataa wabunge wasijadili suala la mgomo wa madaktari, tumeshindwa kumuelewa," alisema Nkya.

Nkya alihoji ingekuwaje kama ni vita halafu Mtanzania mmoja amekufa Serikali ingeendelea kukaa kimya? na kubainisha kuwa maisha ya Watanzania ni muhimu kuliko kitu chochote kile.

Aliongeza kuwa Serikali inatakiwa kutambua kuwa uhai wa Mtanzania ukiondoka hakuna anayeweza kuurudisha na kwamba wanaharakati hawatakaa kimya wakati maisha ya wananchi yapo hatarini.

STORI KWA HISANI YA DOTTO MWAIBALE

Post a Comment