Ads (728x90)

Baadhi ya Daladala za Jiji la Mbeya  zikiendelea na shughuli zake kama kawaida baada ya mgomo wa siku tatu wakidai kuongeza nauli kutokana na ruti iliyoongezwa na SUMATRA

Tofauti na ilivyokuwa jana eneo hili la Kituo cha Daladala Kabwe kulikuwa na Bajaj, Noah na Canter zilizokuwa zinatoa huduma ya usafirishaji, pichani daladala zikiwa katika utoaji wa huduma kama kawaida baada ya tisho la SUMATRA kuwafutia leseni watakaokaidi amri



Pilikapilika za  usafiri zilirejea kama kawaida katika maeneo mbalimbali ya Jiji
Saa kadhaa baada ya Mamlaka ya Usafirishaji,Udhibiti wa Anga na Majini (SUMTRA) kutangaza kuzifutia Leseni za usafirishaji Daladala zitakazoendelea kugoma kutoa huduma hiyo Jijini Mbeya baadhi ya daladala zimeonekana zikirejea kimya kimya na kuanza kutoa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.
Mwanablogu wetu alitembelea katika maeneo ya Kabwe, Stendi Kuu, Sokomatola na Sae na kuona huduma zikiendelea kama awali huku nauli ya usafiri ikiwa ni ile ya Sh. 400 hadi 450 kati ya Stendi Kuu na Uyole na Sh. 200 kwa wanafunzi kama iliyopangwa na SUMATRA.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia sakata hilo walisema kuwa mgomo wa wasafirishaji hao umeathiri uchumi wa serikali kutokana ushuru wa sh. 500 unaotozwa na Halmashauri ya Jiji kwa kila daladala inayotoa huduma za usafirishaji Jijini.
Walisema kuwa mvutano huo ungeendelea ungeathiri kwa namna moja ama nyingine na kwamba kurejea kwa huduma hiyo kumepunguza hasara ambayo serikali ingeweza kuipata kutokana na mgomo huo.
Nao baadhi ya madereva na makondakta wa daladala zilizogoma wamedai kuwa wamerejea katika utoaji wa huduma kwa masharti ya utatuzi wa mgogoro wao kukamilika keshokutwa.
''Tumeahidiwa baada ya siku mbili tutatatuliwa kilio chetu, vinginevyo, tutaendeleza njia zetu za mwanzo bila kukatisha njia,''alisema mmoja wa kondakta wa daladala linalotoa huduma kati ya Sokomatola na Uyole.
Aidha alisema kuwa mgomo wao wamepata hasara iliyotokana na malengo ya kila siku ambapo gari moja huwa na malengo ya kuanzia sh.45,000 hadi 30,000.

Post a Comment