TAFCA MBEYA
CHAMA cha
Makocha mkoani Mbeya (TAFCA)kimepata uomgozi mpya kwa kuwachangua Katibu Mkuu
wa chama hicho na viongozi wengine wanne kwa nia ya kuziba nafasi zilizoachwa
wazi kwa takribani miezi nane.
Viongozi
waliochaguliwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho Joseph Singundali, Katibu Msaidizi
Antony Mwamlima na wajumbe wawili kamati ya Utendaji wa TAFCA Paul
Msyaliha na Oscar Mboma.
Katika
uchaguzi huo uliosimamiwa na Katibu wa chama cha mpira mkoa wa Mbeya Suleiman
Haroub,ulifanyika jana katika Ofisi za Chama Cha Mpira wa Miguu mkoani
Mbeya(MREFA) ambazo zipo katika Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine.
Katika
uchaguzi huo nafasi ya Katibu Mkuu iligombewa na wanachama wawili ambao ni
Singundali na Emmanuel Mgalla ambaye alikaimu nafasi hiyo kwa miezi nane.
Nafasi
hiyo ya Katibu Mkuu iliachwa wazi na Thomas Kasombwe ambaye amehamishwa kikazi
nje ya mkoa wa Mbeya ilhali nafasi ya Katibu Msaidizi iliyochukuliwa na
Mwamlima ilikuwa wazi tangu uchaguzi mkuu uliopita.
Akizungumza
mara baada ya kuchaguliwa kwa viongozi hao msimamizi wa uchaguzi Haroub alisema
kuwa ana imani viongozi hao watasimamia vyema maadili ya kazi zao bila kuibua
migogoro katika mchezo wa soka.
Alisema
kuwa makocha ndiyo dira ya wachezaji na kuwa wachezaji wamekuwa wanaiga kila
kinachofanywa na makocha hivyo iwapo kocha atakosa maadili na wachezaji pia
wataiga tabia hiyo.
‘’Muwe
mfano kwa wachezaji wenu mnaowafundisha, mkikosa maadili ndio mwanzo wa
kuwaandaa vijana wenye vurugu na fujo katika mchezo wa mpira,’’alisema.
Pia
alisema kuwa makocha hawapaswi kusubiri timu za kufundisha bali wao wanatakiwa
kuwa mstari wa mbele kusaka timu za mitaani ili kuibua vipaji vya vijana ambao
ndio wachezaji wa baadaye.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Chama Cha Makocha Juma Mwambusi alisema kuwa dira ya michezo
kwa wachezaji inatokana na makocha bora wenye uwezo na kwamba ni muhimu kwa
makocha kuwaandaa wachezaji vijana ili kupata wachezaji bora.
Akizungumza
mara baada ya kushika nafasi ya Ukatibu Mkuu, Singundali alisema kuwa katika
uongozi wake atahakikisha maadili ya walimu wa michezo yanasimamiwa vizuri ili
kujenga nidhamu ya soka mkoani Mbeya.
Post a Comment