Baadhi ya waumini wa Kiislamu wakitoka katika Ibada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa Baraa Bin Azb Isanga Mbeya. |
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa katika Ibada ya swala ya Ijumaa leo mchana. |
MATAJIRI wa
Kiislamu wametakiwa kutojifaharisha kwa utajiri wao bali wametakiwa kuutumia
utajiri waliopewa na Mwenyezi Mungu ili kuwasaidia wasio na uwezo.
Akizungumza katika
ibada ya swala ya Ijumaa katika msikiti wa Baraa Bin Azb uliopo Isanga Jijini
Mbeya Imamu wa Msikiti huo Shekhe Ibrahim Omar Bombo alisema kuwa utajiri na umaskini
umekuwepo ili kuweka uwiano wa maisha.
‘’Kama
wasingekuwepo matajiri na maskini dunia isingeweza kwenda, matajiri wamekuwepo
ili wawasaidie wasio na uwezo, nao matajiri hawawezi kujivunia utajiri wao kama
hakuna wa kuwasaidia,’’alisema Shekhe Bombo.
Alibainisha
kuwa ili kuona matajiri na wasio matajiri wanategemeana ni pale tajiri
anayemiliki magari ya usafirishaji ambaye anatumia fursa hiyo kuwaajiri wasio
na uwezo ili nao wapate kipato kutokana na utajiri wa mmoja.
‘’Hizi ni
kudra za Mwenyezi Mungu kumpa amtakaye na kumnyima amtakaye, asiye nacho
hapaswi kusikitika sana na aliyenacho hapaswi kujifaharisha kwamba ni mjanja
kuliko asiyenacho,’’alisema.
Akinukuu
baadhi ya aya za Koran na Hadith za Mtume Muhammad (SAW) Shekhe Bombo alisema
kuwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani umekuja ili kuwapima watu uchamungu na kujiweka
karibu na Mwenyezi Mungu.
Alisema kuwa
kipindi hiki cha Mwezi wa toba ndicho ambacho waumini wa dini ya Kiislamu
wanatakiwa kuoneana huruma na kukirimiana na kuwa uchamungu unamweka mja karibu
na Mola wake.
Naye
Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Dhiynurayn Shekhe Dormohamed Issa alisema
kuwa, Mwezi wa Ramadhani umewafanya waislamu kuwa pamoja kwa kipindi kirefu
katika ibada hivyo ni fursa pekee kwa waumini hao kutubu madhambi yao kwa
kukithirisha kufanya ibada usiku na mchana.
‘’Hii ni
fursa pekee kwa waumini kutubu madhambi, wapo waliotangulia mbele ya haki kabla
ya Mwezi huu, hakuna aliyetoa hongo kwa Mwenyezi Mungu ili abaki, turejee kwa
mola wetu atusamehe madhambi yetu,’’alisema Shekhe Issa.
Post a Comment