Ads (728x90)




Wanafunzi wa sekondari Forest ya Jijini Mbeya ambao walidai kuombwa rushwa ya sh.500 na walimu wao
Wanafunzi wa sekondari Forest wakionesha namna ambavyo walikuwa wakiadhibiwa na walimu baada ya kushindwa kutoa rushwa ya sh.500 katika chumba cha Guantanamo

WALIMU wawili wa shule ya sekondari Forest ya Jijini Mbeya ambao awali walidaiwa kuwalazimisha wanafunzi wa shule ya hiyo kutoa rushwa ya sh. 500 kwa kuchelewa shuleni na kupewa adhabu katika Jela iliyopewa jina la Guantanamo wamehukumiwa kifungo cha miaka mine jela kila mmoja.
Walimu hao Faustin Robert(36) na Simon Mwasote(41) walidaiwa kutenda kosa hilo Machi 4 mwaka 2013 ambao kwa nyakati tofauti waliwalazimishwa wanafunzi kutoa sh. 500 kila mmoja  kwa makosa ya kuchelewa shuleni.
Hukumu ya kesi hiyo iliyofikishwa kwa mara ya kwanza  mahakamani hapo Machi 27 mwaka jana   imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mkoa Michael Mta ite mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU  Joseph  Mulebi.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mtaite alisema kuwa washitakiwa wamekutwa na jumla ya makosa manne kwa pamoja ambapo mshitakiwa wa kwanza  Robert alikutwa na kosa moja la kupokea rushwa y ash.500 kutoka kwa mwanafunzi wa kidato cha Nne Samwel Mbilinyi.
Hakimu Mtaite alisema kuwa mshitakiwa wa pili Mwasote alikutwa na makosa matatu ya kupokea rushwa ya sh.500 kutoka kwa wanafunzi watatu ambao ni Evelina James aliyekuwa akisoma kidato cha Nne wakati huo,Faraja Kasian na Recho Mwasiposya waliokuwa wakisoma kidato cha tatu.
Alisema kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa ikiwa ni kinyume cha kifungu namba 15 (1)(a) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka  2007 ambapo watuhumiwa kila mmoja wanahukumiwa kwenda jela miaka 4 kila mmoja ama kulipa faini ya sh.500,00 kwa kila kosa.
Kulingana na hukumu hiyo mshitakiwa wa kwanza Robert alihukumiwa kwenda jela miaka minne au kulipa faini ya sh. 500,000 ambapo mshitakiwa wa pili Mwasote naye alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa makosa yote ama kulipa faini ya sh,milioni 1.5.
Awali Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Mulebi aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa kutokana na kukosa maadili ya kazi pamoja na kuonywa na Bodi ya shule hiyo na kwamba mmoja wa walimu hao alimpiga na kumvunja mgongo mwanafunzi aliyelazimishwa kuweka kichwa chini miguu juu wakati wa utekelezaji wa hukumu katika chumba kilichopewa jina la  Guantanamo.
Hadi tunakwenda mitamboni washitakiwa hao walikuwa bado hawajalipa faini na hivyo kuanza kutumikia kifungo cha miaka minne jela kwa kila mmoja.

Post a Comment