Ads (728x90)KAHAMA:
AMA hakika duniani kuna mambo! Na lisemwalo lipo kama halipo basi laja.  Ni jambo ambalo ni vigumu kuliamini lakini ukweli wa mambo ni kwamba limetokea mjini Kahama, Mkoa wa Shinyanga,  kiasi cha kuleta mtafaruku kwa jamii.
Ni  baada ya vikongwe viwili vinavyosadikiwa ni vichawi kunusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali kufuatia kudondoka kutoka angani.
 Tukio hili la aina yake ambalo mbali na kustaajabisha limeleta hofu kwa baadhi ya wakazi mjini Kahama, lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 3 mwaka huu katikati ya Kata za Majengo na Mhongolo zilizo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Vikongwe hivyo vilikutwa vikiwa taabani huku vikiwa vimetapakaa kinyesi.
Vikongwe hivyo, Mwajuma Samaka Mponi (70) mkazi wa kijiji cha Nduku katika Kata ya Kinaga na Shija Nkwabi (80) mkazi wa kijiji cha Nyashimbi pia mkazi wa Kata ya Mhongolo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, vilikumbwa na dhoruba la kudondoka baada ya kugongana na wanga wenzao wengine watatu waliokuwa katika shughuli zao angani.
 Afisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo, Emmanuel Kalolo,  anasimulia kuwa vikongwe hivyo vilionekana vikiwa hoi havijitambui vikiwa vimelala ambapo kimoja kilikuwa eneo la Kindi’s Bar katika barabara ya kwenda Mhongolo huku mwingine akiwa mtaa wa Bariadi karibu na Café Latino.
Kalolo alisema kuwa Waendesha bodaboda (pikipiki) walianza kumshuhudia kikongwe Mwajuma Mponi tangu alfajiri lakini hawakumjali kwa kudhani kuwa huenda ni mlevi ama mwendawazimu.  Hali iliendelea hivyo hadi alipotokea mtu mmoja ambaye aliingiwa na mashaka  baada ya kumwona akiwa uchi wa mnyama tena akiwa ametapakaa kinyesi.
 Msamaria huyo, Kulwa Samson,  kwa jina maarufu’ KR’ ambaye ni Meneja wa Café Latino, baada ya kumuona bibi huyo aliamua kumpatia msaada kwa kumuombea nguo katika nyumba za jirani.
 Samson alisema alibaini hilo wakati kienda Mhongolo kufuatilia kreti  za bia.  Baada ya kumsaidia, bibi huyo alimweleza kuwa kuna mwenzake mtaa wa pili. Walipomfuatilia  walimkuta akiwa amezingirwa na watu waliokuwa wamemshangaa.
Baada pia ya kumsitiri alimchukua hadi kwa mwenzake na kuwafanyia mpango wa chakula.
 Baada ya huduma hiyo aliwakabidhi kwa Kamanda wa Wanawake Kata ya Majengo, Kuluthum Bujiku, ambapo walianza kuwasaili chanzo cha kuwa katika madhia hayo.  Nao bila kupepesa macho, vikongwe hivyo vilidai vilidondoka vikiwa katika shughuli zao za kawaida za kila siku usiku.
 Mashuhuda hao walisema kuwa vikongwe hivyo vilidai vilikuwa vikitoka katika makao yao ya shughuli zao huko Nduku wakiwa na wenzao watano wakielekea Dodoma kuhitimisha kilele cha sherehe za Pasaka.  Walisema wakiwa angani walipata ajali ya kugongana na wenzao waliokuwa wakitoka eneo jingine hivyo wakajikuta wamedondoka ardhini.
Vikongwe hao vilieleza kuwa safari yao ya Dodoma ilikuwa ya kwenda na kurudi usiku huohuo mara baada ya kukamilika kwa tafrija yao hiyo ya Pasaka.  Kwa bahati mbaya, walidai,  wakiwa njiani kuelekea Dodoma walikumbwa na dhoruba hiyo na kudai baada ya kugongwa “pikipiki” yao iliishiwa mafuta.
Walisema kuwa wenzao watatu ambao waliishawahi kukumbwa na dhoruba hiyo mara nyingi, walitoweka katika mazingira ya kutatanisha na kuwaacha wao wakitapatapa.  Waliongeza kwamba shughuli hiyo  ya usangoma imewafikisha maeneo mbalimbali hapa nchini  na walikuwa hawajawahi kudondoka.
 Baada ya maelezo hayo ambayo waliyatoa huku kukiwa na umati wa watu ambao walitaharuki na kutaka kuwashushia kipigo, sangoma hao walinusurika baada ya Samson kuwa tayari amewapigia simu polisi ambao hawakufanya ajizi kufika eneo la tukio na kuwakuta watu wenye hasira wakiwa wamejipanga kuwatoa uhai vikongwe hao.
 Watu hao walipandishwa katika karandinga huku kikongwe Mwajuma akigoma kuachia kifuko cheusi alichokuwa amekishika mkono wa kulia ambacho alidai ni hazina yao muhimu.  Vilevile, gari la oolisi lilipata wakati mgumu  kuondoka hapo kwani lilionekana kama vile gurudumu zake zinataka kuzama ardhini bila sababu.
 Polisi wilayani Kahama imethibitisha kuwa inawashikilia watu hao.

Post a Comment