Ads (728x90)

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA DIWANI ATHUMANI AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA (HABARI HAWAPO PICHANI) KUHUSU MATOKEO YA VURUGU YA WACHINJAJI
BAADHI YA WATUHUMIWA WA VURUGU ZA UCHINJAJI MJINI TUNDUMA WAKISHUSHWA KATIKA KITUO CHA POLISI TUNDUMA LEO MCHANA



DIWANI wa kata ya Tunduma kwa tiketi ya CHADEMA Bw.Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la KKKT Tunduma Gidioni Mwamafupa wamejisalimisha polisi baada ya tamko la jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kuwataka wajisalimishe kutokana na vurugu za uchinjaji.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Bw.Diwani Athumani amesema kuwa Bw. Mwakajoka na Mchungaji Mwamafupa wanahojiwa na polisi kufuatia taarifa za kiintelijensia kwamba viongozi hao wamehusishwa na kuibuka kwa vurugu hizo.
Amesema kuwa mara baada ya kuibuka kwa vurugu hizo ambazo zilisababisha uharibifu wa mali na majeruhi, watu 94 walikamatwa na kufikishwa mikononi mwa polisi na baada ya mahojiano watu 45 walijidhamini kutokana na polisi kujiridhisha na maelezo yao.
Aidha Kamanda Diwani amesema kuwa kati yao watu 45 wamefikishwa mahakama ya wilaya ya Mbozi kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kula njama,kufanya vurugu, uharibifu wa mali, kuvunja msikiti na  kujeruhi  ambapo kesi yao itarudi tena katika mahakama hiyo April 18 mwaka huu.
Akizungumzia mazingira ya kushikiliwa kwa Bw. Mwakajoka na Mchungaji Mwamafupa Kamanda Athumani alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa za kutafutwa na jeshi la Polisi Bw. Mwakajoka amejisalimisha polisi leo asubuhi ambapo hadi sasa anaendelea kuhojiwa ilhali mchungaji Mwamafupa ni miongoni mwa watu 45 walioachiwa kwa dhamana.
Kwa upande wao CHADEMA mkoa wa Mbeya kimetoa tamko la kulaani kukamatwa kwa Diwani wa kata ya Tunduma na kuhusishwa na vurugu za uchinjaji.
Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Bw. Boyd Mwabulambo amesema kuwa jeshi la polisi linatumia mwanya wa vurugu hizo kukidhoofisha chama chao na hivyo kuendelea kuvuruga amani na utulivu wa mji wa Tunduma.



Post a Comment