Ads (728x90)

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akijadili jambo na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho wilayani humo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye akiwa na baadhi ya madiwani wenzie wakijadiliana mustakabali wao baada ya kutakiwa kutoka nje ya ukumbi wa mikutano ili wajumbe wawajadili.


Madiwani wakijadiliana mustakabali wao baada ya kutakiwa kutoka nje ya ukumbi kupisha kujadiliwa.


Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu CCM Wilaya ya Mbozi wakitoka kwenye ukumbi wa Mkutano.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya Godfrey Zambi akizungumza na Mwandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo kuhusu kikao kilichojadili kuwataka madiwani wa chama hicho wajiuzuru


MSUGUANO mkali umeibuka katika kikao cha Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya ulioshinikiza kujiuzuru kwa Madiwani wote wa Chama hicho kutokana na Halmashauri ya wilaya hiyo kupata hati ya mashaka kwa miaka mitatu mfululizo.
Hatua ya kikao hicho cha chama ilifuatia kuibuka kwa malalamiko yaliyotolewa katika kikao kilichopitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe alihusishwa na ubadhirifu wa fedha za Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa chama hicho wilayani humo uliowahusiha viongozi wa chama wilayani humo na Mwenyekiti CCM mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi Godfery Zambi na Mwenyekiti wa chama wilayani humo Aloyce Mdalavuma.
Madiwani wa chama hicho pamoja na watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo akiwepo Mkurugenzi na wakuu wa idara walionekana kuwekwa kiti moto na chama hicho kwa kile kilichoelezwa kuwa wameshindwa kutekeleza  ilani ya chama tawala na kusababisha kupatikana kwa hati za mashaka kwa miaka mitatu mfululizo.
Kikao hicho ambacho kilivuta hisia za wakazi wengi wa wilayani humo na mkoa kwa ujumka ambapo ambacho waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia,kilidaiwa kumlenga Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elick Ambakisye ajiuzuru nafasi yake kwa shinikizo la viongozi wa chama wilaya kwa kile kilichoelezwa kuwa alishindwa kuisimamia Halmashauri hiyo ipasavyo.
Hata hivyo taarifa zaidi zilidai kuwa kumekuwepo na mvutano wa muda mrefu juu ya viongozi wa chama hicho, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa harakati za kuwania nafasi ya Ubunge kwa mwaka kesho kumeongeza chafu ya kupangua safu ya uongozi wa chama hicho wilayani humo.
Mvutano ndani ya kikao hicho uliibuliwa na wajumbe wa kikao hicho ambao kila mmoja alitoa maoni yake ambapo baada ya kuelekezwa shutuma kwa Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Kadeghe aliyedaiwa kuhujumu fedha za halmashauri hiyo, kibao kiliwageukia Madiwani ambao walielezwa kushindwa kuisimamia vyema Halmashauri hiyo.
‘’Tatizo lipo kwa Madiwani wetu, wameshindwa kuisimamia vyema Halmashauri, ni vyema wangejiuzuru wote ili tujipange upya, hakuna haja ya kuwepo kwa Baraza la Madiwani ambalo halina maslahi na Wilaya na Chama chetu’’alisema mmoja wa wajumbe ambao sauti yake ilisikika hadi nje ya ukumbi.
Mjumbe mwingine wa kikao hicho alielekeza tuhuma zake kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Ambakisye akidai kuwa anapaswa kujiuzuru kwa kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu wa Halmashauri hiyo na kuwa iwapo kungekuwa na usimamizi makini hati za mashaka zisingeweza kutokea.
‘’Kama ni kujiuzuru, meza hiyo hapo mbele wote mnatakiwa kujiuzuru tukianzia na Katibu wa CCM wilaya ndipo wafuate Mwenyekiti na Madiwani, hili jambo ni fedheha kubwa kwa Halmashauri yetu,’’alisema Edward Mwamudi aliyejitambulisha kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu.
Hatimaye maoni mbalimbali ya wajumbe ya Mkutano huo yalisababisha watendaji wa Halmashauri hiyo waruhusiwe kutoka nje ya ukumbi na baadaye Madiwani wote walitakiwa kutoka nje ili wajumbe wajadili aina ya adhabu itakayofaa kwa Madiwani hao.
Baada ya kikao cha takribani saa moja wazee wawili walitoka nje na kumuita pembeni Mwenyekiti wa Halmashauri Ambakisye na kumtaka atumie busara ya kujiuzuru nafasi yake ambaye alikataa na kudai kikao kinapaswa kufuata kanuni ili kuridhia kuondolewa kwake madarakani na si vinginevyo.
Mwandishi: Nasikia umeitwa ili utamke kujiuzuru nafasi yako ya Mwenyekiti wa Halmashauri.
Ambakisye: Wameniita na kunishauri nitamke ili nijiuzuru, nimegoma, wanapaswa kufuata taratibu siwezi kujiuzuru kienyeji, sioni sababu ya kujiuzuru, kwa kosa lipi, kwanini nijiuzuru kuna nini nyuma yake?
Aidha Ambakisye alisema kuwa tuhuma hizo zimeelekezwa kwake binafsi na si vinginevyo na kuwa hii inatokana maslahi ya kisiasa ya baadhi ya viongozi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbozi Mdalavuma alisema kuwa kikao hicho kiliketi kujadili mustakabali wa chama kuelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa mwezi Octoba na uchaguzi mkuu 2015 na kuwa dosari za kuwepo kwa hati za mashaka zingeweza kukipunguzia uaminifu kwa wananchi.
Alisema baada ya kutafakari kwa kina waliamua kuwaita madiwani pamoja na watendaji ili kuwekana sawa ambapo yaliibuka mengi yanayoonesha udhaifu wa usimamizi wa madiwani hao hivyo wajumbe walitoa mapendekezo mbalimbali juu ya hatima ya madiwani hao.
Alifafanua kuwa wapo waliotaka Madiwani hao wajiuzuru na waapo waliosema kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na madiwani wote wanapaswa kujiuzuru lakini wilaya ilishindwa kuchukua maamuzi hayo kwa kuwa haina mamlaka ya kufanya hivyo.
Mwandishi: Hebu nieleze Mheshimiwa Mwenyekiti wa Wilaya, kikao chenu  kilimalizika kwa msimamo upi juu ya hatima ya mwenyekiti na Madiwani wa chama chenu.
Mdalavuma:Kulikuwa na mjadala mrefu juu ya suala la kujiuzuru kwa Mwenyekiti na Madiwani, lakini tulibanwa na kanuni, kikao hakina mamlaka ya kuwasimamisha bali kina uwezo wa kutoa mapendekezo kwenye kikao cha juu cha Halmashauri ya Mkoa na baadaye mkoa utapeleka kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ili ijadili.
Mwandishi:Kulikuwa na taarifa za kutaka kujiuzuru kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na baadhi ya wazee walitoka nje na kumuomba Mwenyekiti ajiuzuru, utaratibu huu ukoje?
Mdalavuma: Kama nilivyokueleza awali taratibu na kanuni zetu zinatubana, Mwenyekiti hawezi kulazimishwa kujiuzuru labda aamue mwenyewe kufanya hivyo, mwanzo alikiri kuwa Madiwani walishindwa kuisimamia Halmashauri, lakini kitendo cha yeye kuamua kujiuzuru kingethibitisha kuwa ana makosa, hivyo taratibu zinapaswa kufuatwa ili kuweka uhalali wa kujiuzuru kwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa Godfrey Zambi alisema kuwa mkutano huo ulitokana na yaliyojiri kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichopita ambacho kilikuwa kikipitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG) ambapo Halmashauri hiyo ilipata hati ya mashaka miaka mitatu mfululizo.
Zambi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Mbozi Mashariki na Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika alisema kuwa kumekuwa na maneno yanayozungumzwa yanayoelezea hisia za viongozi wa chama kuwa na maslahi yao na kuwa uzushi huo si wa kweli bali kilichoendelea ni utendaji na uwajibikaji wa kawaida ndani yaa chama.
‘’Kikao cha leo tumechukua mapendekezo tutayapeleka kwenye kikao cha Maadili, hakuna maslahi ya yeyote kati ya viongozi wa kisiasa, mimi binafsi sijamshambulia kwa maneno Mwenyekiti wa Halmashauri nilishawahi kumsimamia asiondoke wakati wa mgawanyiko wa wilaya za Mbozi na Momba,’’alisema Zambi.
Alisema wapo walioonesha nia yao ya kugombea Ubunge kama vile Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM wilaya hiyo George Mwenisongole,na kuwa yeye hajawahi kulalamika popote ijapo kuwa anachokifanya kiko kinyume na taratibu za chama.
Mwandishi:Mheshimiwa Mwenyekiti wa Mkoa, Zipo taarifa kuwa wewe umekuwa chanzo cha migogoro ndani ya Chama, tangu uingie madarakani chama kimekuwa katika migogoro na hivi karibuni kuna baadhi ya viongozi wa Ileje na Tunduma mmewasimamisha, hili unalisemaje?
Zambi: Kwanza naomba niseme kuwa si kweli kuwa mimi nimekuwa chanzo cha Mgogoro, mie nimesimamia vizuri chama, huko nyuma watu walizoea kufanya kazi kwa mazoea, ufuatiliaji wangu wa karibu umesababisha baadhi ya watu kuona kero.
Mwandishi: Zipo taarifa kuwa jambo hili limetokana na msukumo wa kisiasa, kwa baadhi ya watu walioonesha nia ya kuwania nafasi ya Ubunge ambayo wewe unayo hadi sasa hapo mwakani, hili nalo unalisemaje?
Zambi:Mimi ni Mbunge wa Jimbo hili vipindi viwili, iwapo wananchi wataona nimefanya vyema Chama kinaweza kunisimamisha tena kipindi cha tatu, suala la jambo hili kuwahusisha wanaotaka kuwania Ubunge si la kweli, bali wanayo nafasi ukifika muda kuingia katika kinyang’anyiro atakayefaa ndiye atakayepeperusha bendera ya chama chetu.
Kadhalika katika kikao hicho ambacho kilianza majira ya saa 2:30 asubuhi na kumalizika majira ya saa 12:00 jioni kiliamua madiwani hao wafikishwe kwenye kamati ya maadili ya chama hicho ili hatimaye ikiwezekana maamuzi magumu ya kuwaengua madiwani hao yapitishwe.
Jimbo la Mbozi Mashariki limebakiwa na Kata 18,baada ya kumegwa kwa wilaya mpya ya Momba ambazo ni Msiya, Halungu, Itaka, Bara, Nyimbili, Isansa, Igamba,Myovizi, Ihanda, Ipunga, Isandula,Mlangali,Ruanda, Iyula,Nanyala na Nambizo ambazo zipo chini ya Madiwani wa CCM na kata mbili zilizopo kwenye kata za mjini za Vwawa na Mlowo zinashikiliwa na CHADEMA.



Post a Comment