Ads (728x90)


Diwani kata ya Halungu wilayani Mbozi mkoani Mbeya  Samson Simkoko akielezea muongozo juu ya Mkuu wa wilaya kufanya ubadhirifu fedha za Halmashauri ya Mbozi
Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
Mariam Mtunguja Katibu Tawala mkoa wa Mbeya
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe ameingia katika kashfa nzito ya ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya kudaiwa  kulazimisha kulipwa sh. milioni 4 kila baada ya wiki mbili kwa matumizi yake binafsi.
Dkt. Kaedeghe amedaiwa  kudai kulipwa fedha za halmashauri hiyo mara kadhaa ambapo amekuwa akiandika ‘vi-NOTE’ kwa uongozi wa Halmashauri hiyo akihitaji kulipwa fedha kwa madai ya safari za kuitwa na Rais Ikulu Jijini Dar es salaam.
Tuhuma za DC huyo zimeibuliwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo wakati Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)alipokuwa akisoma hoja zipatazo 100 zisizofungwa  na  Halmashauri hiyo kutokana na kushindwa kwa utekelezaji wa utendaji wa watendaji wa Halamshauri hiyo.
Kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro aliyeambatana na Katibu Tawala wa Mkoa Mariamu Mtunguja na wakaguzi wa kutoka (CAG) kiliingia taharuki baada ya mmoja wa madiwani wa Halmashauri hiyo Samson Simkoko (Kata ya Halungu) kuomba muongozo wakati Mkaguzi wa serikali Johnson Mbwile akisoma hoja za halmashauri hiyo.
‘’Mheshimwa Mwenyekiti naomba Muongozo!! Mkuu wetu wa wilaya amekuwa ni kati ya watu wanaoirudisha nyuma Halmashauri yetu kwa ubadhirifu wa fedha, ninao ushahidi mkuu wetu wa wilaya amekuwa akipewa fedha kinyume cha taratibu, anachukua fedha kwa matumizi ambayo si ya Halmashauri yetu,’’alifafanua.
Kauli ya Diwani huyo iliungwa mkono na takribani madiwani wote na kuibua taharuki katika kikao hicho huku  Mkuu wa Mkoa Kandoro akiwa ametahayari kwa ujasiri uliooneshwa na madiwani hao.
Akitoa ufafanua juu tuhuma hizo alizoibua dhidi ya Mkuu wa wilaya hiyo nje ya ukumbi wakati akizungumza na waandishi wa habari,, Simkoko alisema kuwa anao ushahidi juu ya kile alichokibainisha na kuomba iundwe tume kujua ukweli wa jambo hilo na yeye atatoa ushirikiano kuthibitisha madai yake.
Akifafanua alisema kuwa ana ushahidi wa nyaraka za  mwezi Agosti mwaka huu, zinazoonesha kuwa Mkuu huyo wa Wilaya amekuwa akipewa fedha za Halmashauri hiyo kiasi cha shilingi milioni 4 kila mwezi kwa ajili ya kile kilichoelezwa kuwa amekuwa na safari za  kuitwa Ikulu.
“Nipo tayari kuthibitisha hili, nina ushahidi wa kutosha  DC amekuwa akipewa fedha kiasi cha milioni 4 kila mwezi ukizidisha kwa miezi 12 utapata zaidi ya shilingi milioni 100, hata hao wanaompa hizo fedha nao wanapaswa kuwajibika,’’alisema Simkoko.
Hata hivyo wakati Simkoko akiibua hayo ndani ya ukumbi Diwani wa Kata ya Myovizi Cosmas Nzowa yeye alidai kuwa kinachozungumzwa juu ya tuhuma hizo ni majungu na kuwa hana ushahidi wowote juu ya tuhuma alizotoa dhidi ya Mkuu wa wilaya.
Nzowa alisema kuwa iwapo Mkuu wa wilaya atatuhumiwa kupewa fedha bila utaratibu hata wao madiwani wanapaswa kuwajibika kwa kuwa nao walinunuliwa pikipiki zenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 90 bila kufuata utaratibu na kuwa hayo ni majungu ambayo yanapaswa kupuuzwa.
Akizungumzia mvutano huo mkuu wa Mkoa wa Mbeya Kandoro, aliwataka madiwani na watendaji wa serikali kutekeleza majukumu yao kama walivyotumwa kwa maslahi ya umma na kubainisha kuwa yeye hana tatizo iwapo fedha alizopewa Mkuu wa wilaya zilitumika kwa ajili ya matumizi ya Halmashauri hiyo hata kama hazikufuata taratibu.
Aliongeza kuwa hata hivyo iwapo  malipo hayo yalifanyika kwa kificho hatakubaliana nayo kabisa na kuwa matumizi ya fedha za serikali yana utaratibu wake maalumu na hayapaswi mtu mmoja kujiamualia anavyotaka.
‘’Kama malipo haya yalifanyika kwa kificho sitakubaliana nayo,lakini iwapo yalitolewa kwa kazi zinazohusiana na Halmashauri pamoja na kuwa DC ni mtumishi wa serikali kuu hili halina tatizo,’’alisema Kandoro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elick Ambakisye, alihitimisha kikao hicho na kumuomba  Mkuu wa mkoa kulifuatilia kwa umakini suala hilo kutokana na hali mbaya iliyopo wilayani humo na kuwa viongozi hao wamekuwa wakiwindana hata kufikia hatua ya kutishiana kuuwana.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, ubadhirifu na wizi wa fedha hizo umetokea katika miradi ya kilimo, Maji na ujenzi wa maghala na ununuzi wa pikipiki za shilingi milioni 92 bila kuwa na listi wala maelezo.

Post a Comment