Ads (728x90)

Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais( Kazi Maalum) Profesa Mark Mwandosya akizungumza na wakazi wa Jiji la Mbeya wakati alipokuwa akitangaza Nia yake ya kugombea Urais kwa tiketi ya CCM kwenye Viwanja vya Ukumbi wa Mkapa.



Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wakimsikiliza Prof. Mark Mwandosya


Baadhi ya wananchi wakijitokeza kumuunga mkono Prof Mark Mwandosya kwa kumchangia, jumla ya sh. milioni 10.7 zilichangwa papo kwa papo ili ziweze kumsaidia katika harakati zake za kuchukua fomu na kuwatafuta wadhamini.

`Mmoja wa wazee maarufu kutoka Kata ya Lufilyo wilayani Rungwe akitoa nasaha zake kwa Prof. Mwandosya

Ifuatayo ni hotuba ya Profesa Mark Mwandosya alipotangaza nia yake ya kuwania Urais kwa tiketi ya CCM kwenye viwanja vya ukumbi wa Mikutano wa Mkapa jijini Mbeya jana.
Nianze kuwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,muweza wa yote kwa rehema nyingi alizotushushia kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo. Kwani hatukustahili zaidi ya wengi waliotutangulia mbele za haki.Nawashukuru ninyi nyote mliofika kuungana nami katika siku hii muhimu katika kukuza,kuimarisha na kuendeleza demokrasia ndani ya Chama chetu,Chama Cha Mapinduzi. Wazee wangu,  Waheshimiwa Maaskofu, Viongozi wa Dini na madhehebu mbalimbali,Waheshimiwa viongozi wa kimila,Waheshimiwa Machifu,akina mama,vijana,WanaCCM wenzangu,Viongozi wa vyama vya siasa,Wananchi,Wana Mbeya,Nawashukuru,Asanteni sana kwa uwepo wenu.
Ndugu zangu,
Kwa muda mrefu na kwa njia mbalimbali za mawasiliano mmekuwa mkinidadisi Mbona kimya kuhusu mwaka 2015? Pamoja nna kwambamliutaja mwaka tu, lakini niliwaelewa.Wengi mliushangaa ukimya wangu.Pamoja na na kwamba ukimya ni sehemu ya haiba yangu na daima nimeupokea kama ni karama aliyonitunuku Mwenyezi Mungu,Muweza wa yote,baadhi yenu niliwajibu " Ukimya una Kishindo"! Kuhusu Sultan Qabus wa Oman,mwandishi mmoja maarufu aitwae Robert Kaplan amemwelezea ifuatavyo: Ni mtu mkimya, mpole, hapendi kuzungumza na waandishi wa habari mara kwa mara, hapendi habari zake ziandikwe kwenye magazeti mara kwa mara,lakini ameibadilisha nchi ya Oman kutoka makundi hasimu ya makabila na kuwa taifa linaloheshimika na linaloendelea kwa kasi sana na kuwa mfano wa kuigwa...." Sijifananishi na Sultan Qabus, la hasha.Isipokuwa najaribu kusisitiza kwamba mara nyingi ni bora katika maisha kuwa mjenga hoja na mtendaji makini kuliko kuwa  mpayukaji na maamuzi ya papo kwa papo yenye matokeo hasi na yenye hasara kwa taifa. Nimeenda nje kidogo ya mada yangu!
Kwa staili ya siku hizi wagombea watarajiwa huwa tunajitokeza na kusema : tutatangaza nia siku hii au ile! Nadhani tunawashangaza na mtuwie radhi.Kwani kwa kusema hivyo tunakua  tayari tumetangaza nia!Basi nami kwa staili hiyo hiyo naomba kutangaza rasmi mbele ya kadamnasi hii kama mashahidi,kwamba  kwa unyenyekevu mkubwa, nitaomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natarajia kuendeleza rasmi safari niliyoianza leo kwa kuchukua fomu za maombi hayo pale Dodoma,Makao Makuu ya CCM, jumatano, tarehe 3 Juni,2015, saa 4 kamili,barabara.
Kipindi cha mpito kutoka awamu moja ya uongozi kwenda awamu nyingine kingekuwa kigumu sana kwa nchi nyingi hasa nchi zetu za kiafrika. Mifano iko wazi.Majirani zetu wamepata shida.Lakini waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume wametujengea misingi imara. Tuna kila sababu ya kuwashukuru na tuna kila sababu ya kujivunia misingi hiyo. CCM haijayumba na CCM haitayumba.Baadhi ya wanachama inawezekana wameyumba. Hebu tuzirudie Ahadi za mwana CCM: binadamu wote ni ndugu zangu na AFrika ni moja, nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma, rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa, cheo ni dhamana sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu binafsi, nitajielimisha kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote, nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu, nitakuwa mwanachama mwaminifu wa ccm na raia mwema wa Tanzania na Afrika nzima. Nitasema kweli daima fitna kwangu ni mwiko. Hii ndiyo CCM na atoaye ahadi mbele za Mwenyezi Mungu ndiye Mwana CCM,na si vinginevyo.
Ahadi ya mwanaCCM ya kuondoa umaskini inanipa nafasi ya kuelezea na kusisitiza kipaumbele muhimu sana cha serikali iliyodhamiria kuwaondoa wananchi wake kutoka lindi la umasikini ni kukuza uchumi,uchumi wa kisasa,uliojikita katika misingi ya sayansi na teknolojia na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo hayo. Kama sayansi na teknolojia  ndio msingi wa uchumi wa kisasa basi naweza kusema,tena kwa unyenyekevu mkubwa kwamba aliye mbele yenu ndiye pekee mwenye ujuzi,uelewa,na uzoefu wa masuala haya. Ninalotaka kusisitiza hapa ni kwamba kukuza na kusimamia uchumi ndio utakuwa kipaumbele namba moja.Jenga kwanza uchumi imara na mengine yatafuata.
Uchumi imara unajengwa hasa pale panapokuwa na lengo la kitaifa.Lengo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ni Tanzania kufikia nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Lengo hilo liliwekwa mwaka 2000. Tudhamiria sasa kwamba ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe nchi  za juu zenye kipato cha kati(High Middle Income),na kwamba ifikapo 2050 Tanzania iwe nchi iliyoendelea.
Tunawezaje kuyafikia malengo hayo? Tunawezaje kukuza uchumi na ukuaji huo uwe endelevu?Hili ndilo swali.
1.Kilimo cha kisasa na cha kisayansi kupitia matumizi zaidi na bora ya mbolea; kuendeleza utafiti kwa kuboresha miundombinu,vifaa,na kuendekeza rasilimali watu;kuboresha mifumo na aina ya mikopo kwa wakulima wadogo;kuboresha barabara za vijijini; kuendeleza ujenzi wa maghala kwa ajili ya kutunza nafaka;kuwa na migumo ya uhakika ya masoko ya mazao;na kuhakikisha kiwanda cha kimkakati cha mbolea itokanayo na gesi asilia kinajengwa haraka iwezekanavyo.
2.Kuanzisha na kuendeleza viwanda,kwa kuanzia viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao na rasilimali asili
3.Kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula.
4.Kuendelea kusimamia kutengemaa kwa uchumi mpana
5.Kuondoa vikwazo vinavyozuia uwekezaji wa ndani na kutoka nje
6.Kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa ipasavyo kwa kufungua fursa nyingi za utalii wa ndani na utalii katika sekta ya kusini.
7.Kuongeza tija katika utendaji wa kazi kwa kuthamini kazi(kufanya kazi kwa bidii,kwa uadilifu,na kwa kujituma), kusimamia kanuni,maadili na miiko ya utumishi wa umma na kuufanya utumishi wa umma usiwe wa mazoea tu bali wa ushindani unaopimika katika kutoa huduma kwa wananchi.Hii itakwenda sambamba na kulinda haki na kuboresha msilahi ya wafanyakazi.
8.Kuchukia,kuzuia na kupambana na ufisadi na rushwa. Kuondoa vikwazo vinavyoonekana kuwepo  kwa matabaka mawili ya wananchi; wale wanaoshughulikiwa na takukuru moja kwa moja,na wale ambao kibali kinahitajika kuwashtaki,kwa kuipa Takukuru uwezo wa kisheria kufanya kazi bila kuingiliwa na chombo chochote,wakati huohuo kuhakikisha haki za wananchi wema zinalindwa kupitia chombo cha kusimamia malalamiko (ombudsman).
9.Kuendeleza na ikibidi kuimarisha uhuru wa Benki Kuu  na uhuru wa vyombo vya udhibiti wa huduma za kiuchumi,mifuko ya jamii,bima.
10.Serikali kuwa injini ya ukuaji wa uchumi lakini kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi,mtu mmoja,vikundi vya wajasiriamali,saccos,na kampuni binafsi kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uchumi unapokua,basi serikali itakuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza vipaumbele katika maendeleo ya jamii: Elimu,maji safi na salama,afya, na miundombinu. Kuhusu elimu,lengo litakuwa ni kuboresha mitaala ili iendane na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ngazi zote;kuhakikisha kila mtanzania ana nafasi sawa ya kujiendeleza kielimu kuanzia ngazi ya awali mpaka elimu ya juu; kuendeleza elimu ya ufundi na kilimo; kuandaa na kutekeleza mipango kwa hatua kuifanya elimu ya msingi ifikie kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato cha sita;kuongeza wingi wa udahili  wa wasichana katika katika ngazi ya elimu ya juu;kuboresha hali na ari ya utendaji wa  kazi kwa walimu,ikiwa ni pamoja na ujenzi nyumba za kuishi na kuongeza ujira.
Katika maeneo mengine ya huduma za kijamii,lengo la serikali litakuwa ni kutekeleza sera zilizopo na kuhakikisha malengo yanatekelezwa na yanapimika.Katika kuleta afya bora kwa wananchi lengo litakuwa ni kuweka mizania katika kuzuia na kupambana na magonjwa.
Uchumi hauwezi kukua pasipokuwa na amani na utulivu. Amani usalama na utulivu ni tunu.Waasisi wetu wametujengea msingi wa tunu hii. Viashiria vya kupotea kwa amani vinaanza kuonekana kutoka ndani na nje.Hali inahitaji kuimarisha vyombo vyetu vya usalama katika maeneo yote hususan mafunzo,vitendea kazi,vifaa, miundombinu na silaha za kisasa.Hatimaye ulinzi wa nchi unaanzia mwananchi mwenyewe.
Nafasi ya Zanzibar katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni kubwa. Hii inatokana na asili na haiba ya nchi zenye visiwa,Zanzibar ikiwa mojawapo. Historia ya Zanzibar inatukumbusha hili.Kwani katika karne ya kumi na tisa Zanzibar iliongoza eneo lote la Afrika ya Mashariki kiuchumi na maendeleo,ukuondoa biashara ya utumwa. Ilisemekana Ikipigwa zumari Zanzibar wanacheza ngoma maziwa makuu. Kila linalowezekana litafanywa kuondoa kabisa hali inayoweza kuikwaza Zanzibar kufikia uwezo wake mkubwa kiuchumi.Muungano utaimarika na uchumi wa Tanzania utakuwa kwa kasi zaidi.
Nahitimisha na suala muhimu la uzalendo.Kwa tafsiri isiyo rasmi,Uzalendo  ni upendo kwa nchi. Tumeanza kushuhudia kupungua kwa uzalendo. Upungufu huo unajionesha katika kuenzi tamaduni za nje,kubeza juhudi za maendeleo yaliyopatikana, viongozi kutoa matamshi yanayo kebehi nchi wakiwa nje ya nchi,kutojivunia historia yetu iliyojikita katika michango ya mashujaa wetu. Hawa ni pamoja na  wale waliopambana na wakoloni,akina Kinjeketile,  Mkwawa ,Mirambo,Chaburuma na wengineo ambao walitoa uhai wao kulinda na kutetea heshima ya mwafrika dhidi ya ukoloni.Aidha waasisi wa TANU,Hayati Mwalimu Nyerere,Sykes,Mzee Kawawa, na wenzao;Waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,Hayati Abeid Amani Karume na wenzake akina Mzee Thabit Kombo,Kanali Seif Bakari,Hais Darwesh,Edington Kisasi,Yusuf Himid,Said Washoto na wengineo;ambao walionesha upendo na uzalendo wa hali ya juu.Vilevile tuna mashujaa wa ukombozi wa Kusini mwa Afrika akina George Magombe na Hashim Mbita.Tutaendelea kuenzi, kuthamini,na kuiendeleza  michango mikubwa ya Marais wetu wastaafu,Mzee Aboud Jumbe, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Hayati Idris Abdukwakil,Dr Salmin Amour,Dr Amani Abeid Karume,na Mzee Benjamin William Mkapa. Kipekee napenda kuwashukuru Marais wetu wa sasa; Mheshimiwa Dr Jakaya Mrisho Kikwete,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,na Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein.ambao wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha uchumi na umoja wa nchi yetu. Daima nitaenzi mchango wao. Tujivunie nvhi yetu na  Kwa pamoja tutaenga nchi tunayoitaka.






Post a Comment