Ads (728x90)



TAARIFA KWA UMMA


RATIBA YA VIKAO VYA UTEUZI WA MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI

Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inatoa taarifa kwa umma kuwa muda wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa wanachama wa CHADEMA wanaowania uteuzi wa chama kugombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki ulimalizika rasmi Februari 25, 2012.

Itakumbukwa kuwa sekretarieti ya chama ilitoa muda wa kutosha kwa shughuli hiyo, tangu Februari 14 hadi Februari 25, 2012, ambapo ndani ya muda huo, jumla ya wagombea saba walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu.

Wagombea hao ni; Anna Mghwira, Godlove Temba, Joshua Nassari, Samueli Shamy, Yohane Kimuto, Rebecca Magwisha na Anthony Musami.

Kukamilika kwa shughuli hiyo bila kuwepo malalamiko yoyote rasmi kwa mujibu wa katiba, kanuni, maadili na itifaki ya chama miongoni mwa wagombea, sasa kunatoa fursa kwa mchakato huo kufuatiwa na vikao vya chama kwa ajili ya uteuzi wa jina la mgombea.

Kama ilivyoelezwa awali, vikao vya chama vinavyohusika na uteuzi wanachama waliochukua fomu na kutimiza masharti kadri inavyoelekezwa, vitakaa kufanya uteuzi na hatimaye kumpata mgombea mmoja, ambaye chama kitamsimamisha na kumsimamia kuwania jimbo hilo, ili ashinde na kuongeza nguvu ya wapambanaji ndani ya wabunge, kuwawakilisha Watanzania.

Hivyo kwa kufuata taratibu, kanuni na katiba ya chama kukamilisha mchakato huo kama ilivyo ada ya CHADEMA, Mkutano Mkuu wa Jimbo unatarajiwa kuketi kesho Jumatano, Februari 29, 2012, kwa ajili ya kura za awali (maoni), kisha kitafuatia Kikao cha Kamati ya Utendaji Wilaya ya Meru, kitakachofanyika Machi 1, 2012, kwa ajili ya kufanya uteuzi wa awali.

Kamati Kuu ya CHADEMA inatarajiwa kuketi mjini Arusha, Machi 3, 2012 kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho wa jina la mwanachama mmoja atakayepeperusha bendera ya CHADEMA, kuwania kuwatumikia watu wa Arumeru Mashariki.

Mpaka sasa mipango ya maandalizi ya awali kuhakikisha CHADEMA inaibuka mshindi katika uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, inaendelea vizuri, ambapo makamanda wote wana ari ya ushindi ili kuongeza idadi ya wapambanaji na utumishi bora ndani ya bunge, kwa maendeleo watu na maslahi ya taifa zima.

Kwa umakini na uimara ambao kimeendelea kuudhihirisha katika kuwatumikia na kuwawakilisha Watanzania kupitia majukwaa mbalimbali, tangu Watanzania walipoonesha dalili zote za kukiunga mkono na kukiamini kuwa kinaweza kupewa dhamana ya uongozi wa nchi hii, ari ya chama hiki imezidi kuongezeka siku hadi siku, kikijiandaa kupokea dhamana kubwa zaidi kadri siku zinavyokwenda.

Hivyo katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki, wanachama na wananchi kwa ujumla wazingatie kwamba CHADEMA itaendelea kutimiza dhima yake ya kuhakikisha uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni dhabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.

Imetolewa leo Dar es Salaam, Februari 28, 2012 na;


Tumaini Makene

Afisa Habari wa CHADEMA

Post a Comment