Ads (728x90)


UMEIBUKA uvumi mkubwa katika miji ya Tunduma na Vwawa wilayani Mbozi ambapo imedaiwa kuwa mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mtu mkazi wa maeneo ya Isangu mjini Vwawa wilayani humo amekutwa akiwa amenasa wakati akifanya mapenzi na mwanamume wa nje.
Mwandishi wa habari hizi alifika mjini humo na kukuta makundi makubwa ya wananchi wakiwa wanaelekea katika hospitali ya Wilaya ya mjini Vwawa huku wakisikika wakisimulia mkasa huo ambao umedaiwa kuwakumba mke wa mtu na mwanaume mkazi wa mjini Tunduma.
Wananchi hao ambao wengi wao walikuwa ni akina mama walisikika wakieleza kuwa mwanamke huyo ni mfanyabiashara wa Maparachichi mkazi wa kijiji cha Isangu kilichopo pembeni kidogo ya mji wa Vwawa wilayani Mbozi ambaye hufanya biashara zake kati ya Tunduma na Vwawa.
Ilielezwa kuwa wapenzi hao mke na mwanaume huyo (majina yao hayakufahamika) walikuwa wakionywa mara kadhaa kutoendelea na maapenzi yasiyo halali ambapo mume wa mke huyo inadaiwa alibaini mahusiano ya wapenzi hao kwa muda mrefu.
Ilidaiwa kuwa alipokuwa akimuonya mumewe alichukua shoka tupu na kulikutanisha na mpini huku akimueleza kuwa kama kweli alikuwa hashiriki mapenzi nje ya ndoa uthitisho utakuwa ni shoka na mpini huo ambao aliuhifadhi chumbani kwao wanakolala chini ya uvungu wa kitanda.
Mashuhuda hao waliendelea kudai kuwa siku ya tukio mke huyo aliondoka kama kawaida kuelekea katika biashara zake za maparachichi huko mjini Tunduma mpakani wa Tanzania na Zambia ambako alikutana na Hawara yake.
Hata hivyo makundi hayo ya watu walishindwa kubainisha ukweli juu ya tukio hilo kwa kueleza majina ya wahusika huku Daktari wa wilaya ya Mbozi Dkt.Charles Mkombachepa alikanusha kuwepo kwa watu hao katika hospitali hiyo na kueleza kuwa ni uvumi uliovumishwa tangu asubuhi.
Dkt. Mkombachepa alisema kuwa makundi  ya watu yamekuwa yakimiminika hospitalini hapo kwa siku nzima ya juzi kuanzia asubuhi hadi jioni wakiulizia tukio hilo lisilokuwa na ukweli.
Aidha baada ya kubaini kuwa hakuna tukio hilo uvumi huo ukaendelea kuenea kuwa watu hao wamehamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana na hospitali ya Vwawa kushindwa kuwatenganisha hali ambayo pia ilikanushwa na wauguzi na wafanyakazi wa hospitali ya Rufaa Mbeya.
Uvumi wa aina hiyo umekuwa ukienea mara kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo mwanzoni mwa miaka ya themanini Buguruni Jijini Dar es salaam uliibuka uvumi wa mwanamke aliyemwekea dawa mumewe na kugeuka Nyoka uvumi ambao hadi sasa uko vichwani mwa watu.
Kadhalika mwaka 2003 Jijini Mbeya uliibuka uvumi wa kukamatwa kwa mganga mmoja aliyekuwa akihusika na kuwakata matiti wanawake jambo ambalo pia halikuthibitishwa.

Post a Comment