MECHI ya ligi kuu ya Vodacom iliyowakutanisha maafande wawili Prison ya Jijini Mbeya na JKT Mgambo ya Jijini Tanga imemalizika kwa sare ya Bao 1-1 huku mshika kibendera namba 1 Ephrahim Ndisa akigeuka bondia kwa kumrudi Katibu wa timu ya Mgambo JKT aliyetambulika kwa jina la Antony Mgaya.
Wachezaji wa timu ya Mgambo JKT wakitoka uwanjani wakati wa mapumziko wakiwa kifua mbele kwa bao 1-0 |
Mashabiki wa timu ya Prison wakishangilia baada ya kumalizika wka mchezo kati ya Mgambo JKT na timu yao ambao ulimazika kwa sare ya Bao 1-1 |
Hatua ya Mshika kibendera huyo kumrudi Mgaya ambaye ni Katibu wa timu ya JKT Mgambo ilikuja baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambapo ilidaiwa kiongozi huyo wa Mgambo alimfuata mshika kibendera huyo na kumrushia maneno na kumchapa kibao kutokana na kuongezeka kwa muda wa nyongeza uliyoipatia timu ya Prison bao la kusawazisha.
Alikuwa ni kiongozi wa timu ya Mgambo Mgaya aliyeanza kumshambulia mshika kibendera Ndisa na kumuchapa kibao hali ambayo baada ya Mwamuzi Ndisa alishindwa kuivumilia na kuamua kumrudi kiongozi huyo wa Mgambo kwa kumchapa makonde.
Hata hivyo hali hiyo iliingiliwa na kundi la askari wa JKT na kumfuata mshika kibendera na kujaribu kulipiza kisasi kwa kiongozi wao kupigwa ndipo kundi la watu wakiwemo viongozi wa chama cha Mpira mkoa wa Mbeya (MREFA)waliingilia kati kutuliza vurugu hizo.
Viongozi waliokuwa mstari wa mbele kujaribu kuzuia tafrani hizo walikuwa ni Katibu wa MREFA Suleiman Haruob na Mwenyekiti wake Elias Mwanjala ambaye aliwachukua viongozi wa timu ya Mgambo JKT na kuingia nao ofisini kwake.
Mbali na tukio hilo mchezo huo ambao ulitawaliwa zaidi na timu ya Mgambo JKT ya Tanga kwa kuwakimbiza zaidi wachezaji wa timu ya Prison ambao mara kadhaa walikuwa wakikosa fursa za kufunga magoli wakiwa wamebaki na kipa wa JKT Mgambo Tommy Kavishe.
Goli la kwanza lilipatikana dakika ya 30 lililofungwa na mchezaji wa Mgambo Peter Mwalyanzi ambaye aliwatoka walinzi wa timu ya Prison na kupiga shuti lililomwacha golikipa wa Prison Ben Kakokanya akichupa bila mafanikio.
Hadi kipindi cha mapumziko JKT Mgambo ilikuwa ikiongoza kwa Goli 1 dhidi ya 0 kwa timu ya Prison.
JKT-Mgambo ambayo ilikuwa ikipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Mbeya City ambao walikuwa wakiwashangilia kila hatua,waliumudu vyema mpira kuliko wenyeji Prison ambao kwa muda mrefu walionekana kutoelewana uwanjani.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko ambapo Prison ilimtoa Peter Michael na nafasi yake kuchukuliwa na Bryton Mponzi hali iliyoanza kuonesha uhai kwenye safu ya ushambuliaji.
Goli la kusawazisha kwa timu ya Prison lilipatikana dakika za nyongeza baada ya mchezaji wa timu hiyo Laurian Mpalile kupokea pasi kutoka kwa Salum Kimenya ambapo bila ajizi Mpalile alimtazama golikipa wa timu ya JKT Mgambo alivyokaa na kupiga shuti iliyomwacha golikipa wa timu ya Mgambo Tommy Kavishe akichupa bila mafanikio.
Muda mfupi baadaye refarii Hashim alipuliza kipenga cha kumaliza mchezo huo ndipo sakata la vurugu lilipoanza nje ya uwanja kwa Katibu wa Mgambo Mgaya kupigana na Mshika kibendera Ndisa kwa kile kilichoelezwa malalamiko kutokana kuongeza muda uliosababisha Prison kusawazisha bao.
Post a Comment