Ads (728x90)

GUMZO la wiki hii miongoni mwa Watanzania wengi ni mjadala kuhusu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wapo wanaopongeza hotuba yake bali pia wapo wanaoizungumzia kwa mtazamo tofauti wakielezea msimamo wao juu ya mustakabali wa tume ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya.

Mjadala huu umefikia hatua ya hata watu kuhoji kauli ya JK kubeza wachache waliojitokeza kutoa maoni yao juu ya kuwepo kwa mfumo wa serikali  kama ilivyoeleza taarifa ya tume ya kukusanya maoni ya Katiba ambayo kulingana na hotuba ya Rais kama alivyoisoma Bungeni  kama ifuatavyo;

 ''Taarifa  imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.

 Rais aliendelea kusoma hotuba yake huku akishangiliwa na baadhi ya kundi la wajumbe wa bunge hilo na kuendelea kusema kuwa;

''Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi? 

Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?....

”Hii ni kauli ya Rais  wakati akizungumza kwenye Bunge Maalum la Katiba, hata hivyo mchanganuo huo aliouonesha Rais Kikwete unapingwa na baadhi ya watu ambao kwa sababu zao maalumu hawakupenda kuwekwa hadharani ambao wanaohoji kuwa iwapo Rais kabeza idadi ya wachache miongoni mwa wengi waliotoa maoni kuwa ni idadi ndogo ya wahitaji wa Muundo wa serikali Tatu, basi hata yeye Rais hakidhi kuwa katika nafasi aliyonayo kwa madai kuwa idadi ya waliomchagua haifanani na idadi ya Watanzania wote na hata idadi ya waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2010.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao wamedai kuwa kwa mujibu wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Rais Jakaya Kikwete alipita kwa asilimia 61.7 ya kura zote halali. ambapo idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa ni 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura wote ambao hawakufika hata nusu yake, hivyo Rais anaongoza kwa idadi ya waliomchagua ambao hawakufikia hata nusu ya wapiga kura waliojiandikisha.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kwamba mchanganuo wa idadi ya kura ilikuwa 227,889 ambazo ni asilimia 2.64 ziliharibika,kura halali zilizopigwa zilikuwa 8,398,394 sawa na asilimia 97.37 ya kura zilizopigwa ambapo Rais Kikwete alipata jumla ya kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, ambapo kama ingeelezewa kwa idadi ya waliojiandikisha JK anaongoza idadi ya wachache huku idadi kubwa ya waliojiandikisha hawakumpigia kura.

''Kama tukifuatilia uwiano wa maoni kulingana na mtazamo wa JK kuhusu Katiba, basi hata JK hana sifa ya kuwa Rais kwa kuwa anaongoza idadi kubwa ya watu ambao hawajamchagua kuwa Rais kwa kuwa idadi ya Watanzania wote wanafikia milioni 45,  hata idadi ya waliomchangua ni robo tu ya idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ambao hawakujitokeza, pia hao waliojitokeza kupiga kura hawakuvuka asilimia 50,''amesema mchambuzi huyu wa mambo ya kisiasa.TUJADILI HOJA HII BILA JAZBA HUKU TUKITANGULIZA MBELE UTAIFA WETU NA MASLAHI


Post a Comment