Mkuu wa wilaya ya Mbeya Dkt. Nouman Sigalla |
Washiriki wa Mafunzo katika ukumbi wa VETA jijini Mbeya |
Washiriki wa mafunzo |
ZAIDI ya vijiji 830 vinatarajia kunufaika na miradi endelevu ya huduma za Nishati ikiwa ni mkakati wa serikali kuvisaidia vijiji kuondokana na tatizo la nishati ya umeme nchini.
Hatua hiyo imelenga kusaidia huduma za maendeleo vijijini ambavyo watumiaji wa nishati hiyo wako chini ya asilimia 10.
Akizungumza Jijini Mbeya kwenye mafunzo kwa wawakilishi 29 kutoka mikoa Nane ya Mwanza, Katavi,Arusha,Njombe, Iringa, Ruvuma, Dar es salaam na Mbeya, Oscar Lema kwa niaba ya Mkurugenzi wa REA Dkt. Lutengano Mwakahesya, alisema kuwa lengo la mpango huo ni kuwezesha kufikia asilimia 12-15 ya watumiaji wa Nishati ya umeme na gesi maeneo ya vijijini.
Alisema wananchi wa vijijini ndio ambao wanaathirika zaidi kutokana na kukosekana kwa nishati ya umeme na gesi hali ambayo inachangia kukwamisha maendeleo yao na kwamba huduma hizo zikifika maeneo ya vijijini itarahisisha huduma mbalimbali za kijamii.
''Kukosekana kwa nishati kumepunguza kasi ya maendeleo ya wananchi,mpango huu utasaidia kuboresha hali hiyo'',alisema Lema.
Alifafanua kuwa REA ambayo ni Taasisi iliyoanzishwa na serikali kwa nia ya kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme na gesi imeweka mpango wa kuyawezesha makampuni ya uwekezaji ili yaweze kukopesheka Benki kusaidia uwekezaji wa nishati ya umeme vijijini.
''REA itasaidia asilimia 20-30 kulingana na mradi uliobuniwa na Kampuni sehemu inayobaki itasachukuliwa na Benki itakayozikopesha taasisi kuwezesha miradi ya Nishati,alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Kiteweka Hydro Power Eva Kleruu alisema mafunzo haya yatawawezesha kufika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kuimarisha miradi yao kuviwezesha vijiji kufikiwa na huduma ya nishati ya umeme na gesi.
Alisema mbinu zilizotumiwa na serikali zitawezesha kupiga hatua ya maendeleo kwa maeneo ya vijijini ambao kwa miaka mingi wamekuwa ni wahitaji wa huduma hizi muhimu katika kusukuma maendeleo.
Post a Comment