Ads (728x90)


Unapolala na kuamka salama ukajiona wewe umekula na kusaza na vingine kutupia jalalani, unajiona mjaanja kweli,umesahau kwamba kuna binadamu wengine wangependa kuishi kama unavyoishi wewe kwa maisha ya Raha Mustarehe, Mwangalie Mama huyu, anaweza kuwa ni mama wa mmoja wetu hapa hapa nchini au kwingineko katika Bara hili la Afrika, yupo duniani anatafakari maisha yake, anajua ya leo ya jana hayajui na hategemei ya kesho yatakuwaje, kama ambavyo pia wewe hutegemei yajayo.
Ila kwa kiburi cha wengi hudhani kuwa yajayo yapo mikononi mwao, huamua kula na kusaza na kusahau akina mama wa Kiafrika wa aina hii popote walipo kwamba nao hupenda kujua yajayo na mipango ijayo kwa kuziandalia maisha bora familia zao siku zijazo.
Tabu inakuja kwa hawa wenzetu wanaojiona wamekaa juu ya maghorofa na kuwatemea mate watembea kwa miguu peku peku chini huku jua kali liliwachoma miguu yao tena wakiwa vifua wazi, si kukaa juu ya maghorofa tu hata kutembelea magari ya gharama kubwa ambayo hupita katika barabara mbovu zinazohitaji kukarabatiwa kwa gharama zile zile za magari hayo waliyoyanunua tena kwa fedha za walipa kodi WAKIDANGANYIKA.
Haya ni Maisha na yoyote anaweza kupitia hali hii, hivi ni nani anapenda kuwa kama huyu Bi mkubwa aliyeketi hapo juu, unadhani nani anapenda kufikia hali hii, hebu nyie mnaopenda kukaa Ikulu ijaribuni hali hii,namkumbuka MALENGA Mrisho Mpoto, alipokuwa anamwelezea mjomba wake, pale aliposema kuwa 'JARIBU KULA MAJALALANI NA WATOTO WA MITAANI'mie nasema jaribu kukaa na njaa kama Bi mkubwa huyu....thubutu!!!! kama hamtaomba mpelekwa Ulaya kutibiwa tena kwa ghara zetu sisi walipa kodi.
Eee!!! Mungu hivi unaona udhalili huu kwa waja wako wasio na hatia?, hivi unawaacha tu hawa watu wanaokula bila kunawa na kudhulumu haki zetu sisi watu akina yakhe tusio na mbele wala nyuma, tusio na bazi wala kazi, bali tukiahidiwa ajira milioni moja kila baada ya miaka mitano.
Chezeeni tu rasilimali zetu, na pangisheni kila urithi wetu na utajiri wetu chambilecho cha Dada angu Irene Sanga alipokuwa akiwaambia hao wakubwa WAPANGISHE HADI MAKABURI YETU.TIME WILL TELL itafika mahali vizazi vyetu vitakuja piga bakora makaburi yetu na hata kufukua makaburi, kufanyia uchuguzi vichwa vyetu na kupasua kuviingiza maabara na kujiuliza hivi hawa watu wa zama hizi walikuwa na vichwa vyenye kutafakari mambo yajayo?
Nina wasiwasi mkubwa na uamuzi unaochukuliwa na viongozi wetu kama umelenga kutunufaisha sote, mie nadhani kila linaloamriwa lina nia ya kunufaisha wachache,mbona enzi zile za Mwalimu halihaikuwa hivi, au tuseme watu wameelevuka sana, au zama hizi kila mmoja anajua kujinufaisha mwenyewe!!!!
Mhhh ngoja niishie hapa nisije kuonekana mie nachonga wakaniziba kilomolomo changu.
Wakatabahu

Post a Comment

  1. Kusema kweli hiyo picha kwa kweli inasikitisha sana kwani usemayo ni kweli kuna watu wanatupa chakula kila siku na kuna wengine wanalala njaa kila siku. Huwa nawaambia wanangu habari hii. Kwani kama huna njaa ya nini kuchukua chakula au kupika chakula kingi na halafu kutupa. Kuhusu nguo hapa niishipo mimi watoto pia watu wazima wanatupa nguo kila siku na pia viatu kisa hawataki, wanataka mpya au wamechoka tu nayo. Kwa hiyo ukiona watu wanatembea nusu uchi na wengine wanachumwa na jua roho inauma sana.

    ReplyDelete