MILIO ya risasi,harufu ya mabomu ya machozi na wananchi kuharibu magari ya serikali ilikuwa ndiyo mandhari ya mji mdogo wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia baada ya askari polisi wa kituo cha Tunduma PC Justin kudaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mfanyabiashara wa Tunduma Bw.Frank Mwachembe(34).
Hali hiyo imeibuka jana majira ya kuanzia saa tano asubuhi ambapo umati wa wakazi wa mji huo ambao ni maarufu kwa biashara za ndani na nje ya nchi kuingia barabarani huku wakisikika wakidai kutaka kulipiza kisasi kwa kitendo cha askari polisi kumuua raia asiye na hatia.
Kundi hilo la wananchi ambalo lilionekana kujawa na hasira huku kila mmoja kati ya wananchi hao akionekana kubeba lundo la mawe mkononi mwake lilianza kurushia mawe kila gari la serikali lililoonekana barabarani na kusababisha baadhi ya magari likiwemo gari la Jeshi la Wananchi na la Ofisi ya Mkuu wa mkoa kuvunjwa vioo vyake vya mbele.
Marehemu ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Sogea mjini Tunduma amedaiwa kuuawa majira ya saa tano usiku wa kuamkia jana baada ya askari polisi kushuku kwamba alikuwa ni jambazi.
Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa tukio hilo limegubikwa na utata kulingana na mazingira ya kifo ambapo marehemu akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Chaser yenye namba za usajili T 888 AEA alikuwa akifukuzwa na gari la kiraia aina ya Escudo lenye namba za usajili T 559 AFA ambalo lilikuwa likiendeshwa na PC Justin.
Taarifa zimedai kuwa askari huyo alikuwa akifuatilia tukio la ujambazi ambalo lilipata kutokea katika mji huo hivi karibuni na kwamba alilishuku gari la marehemu kuwa ni miongoni mwa magari yaliyohusika katika tukio hilo .
Mwenyekiti wa serikali za mtaa wa mtaa wa Sogea Bw,Ali Mwafongo ambako marehemu alikuwa anaishi amesema kuwa marehemu kabla ya kuuawa alikuwa akifukuzwa na gari aina ya Escudo na kwamba yeye pamoja na majirani wa marehemu walisikia milio ya risasi eneo la tukio.
Amesema baada ya kusikia milio hiyo walitoka nje na kuona magari matatu yenye askari likiwemo gari la marehemu na kwamba walimuuliza kama alikuwa akimfahamu marehemu ambaye kwa wakati huo kwa kuwa ilikuwa ni usiku hakuweza kumtambua vyema.
Amesema kuwa alifahamu kuwa aliyeuawa ni jirani yao baada ya kwenda katika kituo cha afya cha Tunduma na kuukuta mwili wake ndipo wananchi walipoanzisha maandamano na kulaani mauaji hayo.
Aidha maandamano hayo yalizimwa na kikosi cha kutuliza ghasia FFU ambao waliwatawanya wananchi huku wananchi hao wakidai kumtaka askari aliyefanya mauaji hayo naye kuuawa kama alivyomfanyia mfanyabiashara huyo.
Mmoja wa ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Bw. Joseph Mwasote ameomba kuundwa kwa tume ili kubaini ukweli wa mauaji huku akitaka uchunguzi wa mwili wa marehemu usifanywe na madaktari wa mkoa wa Mbeya kwamba wanaweza kuhujumu ukweli wa taarifa hizo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Bw. Advocate Nyombi amelazimika kukatisha ziara kukimbiza Mwenge kwa nia ya kufuatilia tukio hilo ambaye amesema kuwa jeshi la polisi litafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo.
Taarifa zaidi za tukio hili baadaye
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment