Ads (728x90)




Na Esther Macha, Mbeya

MAMA na mtoto wakazi wa kijiji cha Iseche kata ya Mwambani Tarafa ya Kwimba Wilayani Chunyani Mkoani Mbeya wanatafutwa na jeshi la polisi Mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua mume wake aitwaye ,Silvester Alphonce Chikondo(55)baada ya kushambuliwa kwa malungu na mke wake kwa kushirikiana na mtoto wake wa  kiume.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Mkoani Mbeya ,Diwani Athuman alisema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 12 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika kijiji cha Iseche wilayani hapo.

Kamanda Athuman alisema kuwa marehemu alikutwa na mauti hayo wakati alipokuwa akitoka kilabuni kunywa pombe ndipo mama huyo kwa kushirikiana na mwanae wa kiume walipoanza kumshambulia kwa malungu kwa kile kinachodaiwa wivu wa kimapenzi.

Hata hivyo Kamanda Athuman alisema kuwa mke wa marehemu na mwanae wa kiume walimshambulia marehemu huyo kwa kumpiga na malungu kichwani,utosini pamoja na ngumi na mke wake aliyejulikana kwa jina la Husulinakornel (42) akiwa na mwanae  Kondo Alphonce Chikondo(19)

Akizungumzia mazingira ya tukio hilo Kamanda Athuman alisema kuwa mbinu iliyotumika ni kumshambulia kwa kumpiga baada ya  kufika nje ya nyumba wakitokea kilabuni kunywa pombe za kienyeji.

Alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa kimapenzi kufuatia marehemu kuongea na mwanamke mwingine wakati wakiwa kilabuni na mkewe walipokuwa wakinywa pombe ndipo mke wa marehemu alipoingiwa na wivu na kuanza kuleta ugombi wakiwa kilabuni. 

Baada ya kipigo hicho kutoka mkewe na mwanae wa kiume marehemu alianguka kisha kufariki dunia papo hapo.

Mama huyo akiwa na mwanae walikimbia na kukimbilia kusikojullikana mara baada ya  kugundua mumewe amefariki dunia na kwamba mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kubainika ubongo kuchanganyika na damu hivyo kusababisha kifo chake.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Mbeya  kamishna msaidizi wa polisi Diwani Athumani  ametoa wito kwa jamii hasa wanandoa kutatua matatizo kwa njia ya  kukaa meza ya  mazungumzo na kujenga hoja badala ya  kujichukulia sheria mkononi na kutumia nguvu  kwani ni kinyume cha
sheria na pia kuepusha matatizo yanayoweza kuepukika.

Aidha Kamanda alisema kuwa mtu yeyote mwenye taarifa juu ya  mahali walipo watuhumiwa azitoe katika mamlaka husika ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake, vinginevyo wajisalimishe wenyewe.

Post a Comment